Siasa

JAMVI: Ruto kutumia kura ya Msambweni kujipima uzito

September 27th, 2020 4 min read

Na MOHAMED AHMED

IFIKAPO mwaka wa 2022 wakati nchi hii itakapokuwa inaelekea katika uchaguzi mkuu wa urais, baadhi ya wawaniaji wa kiti hicho watakuwa wamejipima nguvu vya kutosha.

Mmoja kati yao ni Naibu Rais, Dkt William Ruto ambaye ameamua kutoacha nafasi yoyote kumpita katika mipango yake ya kumwezesha kujipima nguvu zake za kisiasa katika maeneo tofauti.

Siku za hivi karibuni, Bw Ruto ameonekana zaidi kulenga maeneo yanayotambulika kuwa ngome za hasimu wake wa karibu kinara wa ODM, Bw Raila Odinga.

Haya, kulingana na wachanganuzi wa siasa, ni kuhakikisha kuwa Dkt Ruto anajizolea kura hata kama ni chache kwenye maeneo hayo.

Mwaka 2019 licha ya kupata pingamizi kuhusiana na uchaguzi mdogo wa Kibra, Bw Ruto alihakikisha kuwa amemdhamini mwaniaji wa eneobunge hilo ambaye pia ni mwanasoka mstaafu, Bw Donald Mariga kupitia tiketi ya chama cha Jubilee.

Katika kinyang’anyiro hicho, Bw Ruto aliongoza kampeni hizo licha ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye ndiye kiongozi wa chama hicho kutohusika kama inavyotarajiwa.

Uchaguzi huo ulikuja wakati Rais Kenyatta pomoja na Bw Odinga walipokuwa wamesalimiana na kukubaliana kudumisha amani nchini kupitia muafaka maarufu kama “handshake”.

Katika uchaguzi huo, licha ya chama cha ODM kushinda kiti hicho, kupitia mgombeaji wake, Bw Imran Okoth, Dkt Ruto alitambua kuwa sasa anaweza kumtikisa Bw Odinga katika ngome zake.

Kwa mara nyingine tena wadadisi wa wanasema kuwa Dkt Ruto anataka kujipima nguvu zake tena katika uchaguzi mdogo ambao umeratibiwa kufanyika katika ukanda wa Pwani.

Licha ya azma yake ya kutaka kuweka mwaniaji wa ubunge katika uchaguzi mdogo wa Msambweni kuzimwa, amehakikisha kuwa bado atahusika katika uchaguzi huo.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa za Pwani, Prof Hassan Mwakimako, ung’ang’anizi wa Bw Ruto kuhakikisha kuwa anahusika katika uchaguzi huo ni kutaka kujipima uzani wake huku akijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

“Ruto anajenga mpango wake wa kuwania kiti cha urais na kwa ajili hiyo ni lazima ‘apime maji’ kila anapopata nafasi hiyo. Mashindano ya uchaguzi mdogo wowote sasa yatatoa fursa mwafaka ya kujipima misuli kwa wale wanaotaka kiti cha urais,” akasema Prof Mwakimako.

Jubilee ilisema kujiondoa kwake kwenye uchaguzi huo ni kutokana na muafaka wa amani baina ya Rais Uhuru na Bw Odinga, lakini ni wazi kuwa Bw Ruto haungani na hilo.

“Imejitokeza wazi kuwa Ruto sasa anajenga Jubilee yake ambayo haiambatani na ile ambayo inaendeshwa tofauti na maoni yake. Ni wazi kuwa anaweka mikakati ambayo itampa nafasi ya kujijenga yeye binafsi,” akasema Prof Mwakimako.

Mnamo Jumatano, baada ya kusema kuwa amekubaliana na uamuzi wa chama cha Jubilee kuwa hakitaweka mwaniaji wa kiti hicho, Bw Ruto sasa ameibuka na njia mbadala ya kuhakikisha kuwa anapimana ubabe na Bw Odinga.

Sasa, kupitia kwa wabunge wa Pwani wanaomuunga mkono, Bw Ruto alikutana na mwaniaji mwengine Feisal Bader ambaye atapigania kiti hicho kama mgombeaji huru.

Katika mtandao wake wa kijamii, Bw Ruto mnamo Alhamisi aliweka picha baada ya kukutana na wabunge hao katika afisi yake ya Karen jijini Nairobi akiwemo Mohammed Ali (Nyali), Athman Shariff (Lamu Mashariki), Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na Khatib Mwashetani (Lunga Lunga) ambao walikuwa wameandamana na Bw Bader.

Bw Ali, hata hivyo aliweka picha hizo hizo na kueleza kuwa watakuwa debeni kwenye uchaguzi huo.

“Msambweni iko sawa. Team Mgombea-huru – Feisal Abdallah Bader. Wacha watu waamue,” akasema Bw Ali kupitia mtandao wake wa kijamii wa Facebook.

Bw Ali alisema kuwa kuwekwa kwa mwaniaji huyo ni kuhakikisha kuwa kasumba ya watu fulani kuwa vigogo wa ngome inaondolewa.

Sasa ni rasmi kuwa Bw Bader ambaye alikuwa msaidizi wa aliyekuwa mbunge wa Msambweni marehemu Suleiman Dori atapambana na Bw Omar Boga ambaye kulingana na wadokezi atapata tikiti ya chama cha ODM.

Mariam Sharlet

Ikiwa wazi kuwa Bw Ruto atampigia debe Bw Bader baada ya mgombeaji mwengine, Bi Mariam Sharlet, kukosa nafasi ya tiketi ya Jubilee, kutakuwa na siasa kali kati ya Naibu Rais na Bw Odinga.

Kabla ya Bi Sharlet kutaka tiketi hiyo, alikuwa katika chama cha ODM lakini akajiuzulu na kutegemea tiketi ya Jubilee.

Kujiuzulu kwake kulifuatia kujiondoa kwa afisa wa fedha za Kaunti ya Kwale, Bw Bakari Sebe ambaye alikuwa anapigiwa upatu na Gavana Salim Mvurya ambaye wadokezi walieleza kuwa alikuwa anapata msukumo kutoka kwa Bw Ruto.

Kubadilika kwa mambo hayo kulijiri siku tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutembelea eneo la Kwale na kukutana na Bw Mvurya.

Hapo awali Bw Bader ambaye ni mtu wa familia ya Bw Dori alikuwa amepigiwa debe kupata tiketi ya ODM.

Mnamo Jumatano, Bw Odinga alikuwa ametoa shukrani zake kwa chama cha Jubilee kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho licha ya Bw Ruto kusema alikuwa na maoni tofauti kuhusiana na hilo.

“Mimi nilikuwa na maoni tofauti kuhusiana na suala hili lakini tumekubaliana kama chama. Hata hivyo, ninasema kuwa mwaniaji yeyote ambaye anataka nimsaidie, basi aongee nami vizuri na nitatekeleza hilo,” akasema Bw Ruto baada ya kukutana na katibu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju.

Bw Tuju alitangaza kuwa Jubilee haitoweka mwaniaji kwenye uchaguzi huo kwa sababu ya ushirikiano wao wa amani na ODM.

Sasa ikiwa bayana kuwa Bw Ruto amepata upenyo wa kujitosa katika siasa hizo za eneo la Msambweni, itasubiriwa kuonekana namna kivumbi kati yake na Bw Odinga kitakavyojisuka wakati uchaguzi huo utakapokaribia.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Disemba 15 kama ilivyotangazwa na IEBC.

Bw Ruto na wabunge hao wa Pwani wanatarajiwa kutumia kigezo cha Bw Bader kuwa mtu anayeelewa kazi ambayo iliachwa na marehemu pamoja na yeye kuwa mjuvi wa kazi hiyo.

Hata hivyo, Prof Mwakimako anasema kuwa hilo halitatosha kuhakikisha Bw Bader anapata nafasi hiyo.

Alisema kuwa ni wazi kuwa Bw Odinga ana ushawishi mkubwa Pwani ambao atatumia kushinda kiti hicho.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho anatazamiwa kuwa miongoni mwa wale ambao wataongoza kampeni za ODM kumpigia debe Bw Boga ambaye aliwahi kuwa diwani wa Gumbato.

Mipango ikianza kushamiri kuhusiana na uchaguzi huo, itasubiriwa kuonekana jinsi mashindano hayo yatakavyokwenda.