Siasa

JAMVI: Siasa fiche za Waiguru, Kibicho kuhusiana na Kemri

February 23rd, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

MVUTANO mkali unatokota kati ya Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga na Katibu wa Wizara ya Usalama Dkt Karanja Kibicho, kuhusu udhibiti wa siasa wa kaunti hiyo na ukanda wa Mlima Kenya kwa jumla.

Hilo limechangiwa na utata kuhusu uendeshaji wa mradi tata wa Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu Kenya (Kemri) wenye thamani ya Sh15 bilioni. Mradi huo tata umo katika ardhi ya ekari 100 katika eneo la Makutano, eneobunge la Mwea.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa sababu kuu ya vita hivyo baina yao ni ushindani wa udhibiti wa siasa za Mlima Kenya, hasa urithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hili ni baada ya kuibuka kwamba Dkt Kibicho anapanga kuwania ugavana katika kaunti hiyo, hatua inayoonekana kumpa wasiwasi Bi Waiguru.

Kando na Dkt Kibicho, wadhifa huo umewavutia watu kadhaa wenye ushawishi mkubwa, baadhi yao wakiwa balozi wa Kenya nchini Amerika Bw Njeru Githae, kiongozi wa Narc-Kenya Bi Martha Karua, aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Bw Joseph Ndathi, Mwakilishi wa Wanawake Bi Wangui Ngirichi kati ya watu wengine maarufu.

Na kwa kuwa Bi Waiguru anapania kuwania mojawapo ya nyadhifa kuu za kitaifa ikiwa Wakenya watapitisha ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), wadadisi wanasema kuwa tashwishi kuhusu hatima ya mchakato huo ndiyo inaonekana kumpa wasiwasi wa kisiasa.

“Bi Waiguru ametangaza wazi kwamba analenga kupata mojawapo ya nyadhifa kuu ambazo ripoti ya BBI imependekeza kubuni; baadhi zikiwa Waziri Mkuu ama Naibu Waziri Mkuu. Hata hivyo, lazima ahakikishe kuwa ametetea na kulinda nafasi yake ya ugavana ikiwa mpango huo hautafaulu,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Ingawa ni mapema, ujio wa Dkt Kibicho, Bw Githae na Bi Ngirichi umetajwa kumnyima usingizi Bi Waiguru, ikizingatiwa kwamba kando na ushawishi mkubwa wa kisiasa, wana uwezo mkubwa kifedha.

Tangu kuanza kuhudumu kama gavana, Bi Waiguru amekuwa akifanya mikakati kujinadi kama mrithi wa kisiasa wa Rais Uhuru Kenyatta kama kiongozi wa Mlima Kenya, ikiwa atastaafu uongozini mnamo 2022.

Mara tu baada ya kuchaguliwa kama gavana, alichaguliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), akiwa mwanamke wa kwanza kuchukua nafasi hiyo.

Baadaye, alianza harakati za kuipigia debe ripoti ya BBI kupitia kundi la ‘Embrace’ lililowashirikisha viongozi wa kisiasa wanawake, waliodai kuunga mkono handisheki kati ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Bw Raila Odinga.

Wachanganuzi wanasema kuwa lengo la Bi Waiguru kutwaa nafasi ya Uwaziri Mkuu ama naibu wake, ndiyo sababu kuu ambapo anamkabili kiongozi yeyote anayeonekana kuwa tishio ama kuingilia karata zake kisiasa.

Wiki iliyopita, gavana huyo alijibizana vikali na Dkt Kibicho kuhusu mradi wa Kemri, huku akimlaumu (Dkt Kibicho) kwa “kutumia ushawishi wake kuingilia kati utendakazi wa serikali ya Kirinyaga.”

Utata huo ulianza baada ya Bi Waiguru kusema kwamba lazima wenyeji wa kaunti hiyo watengewe angaa asilimia 30 ya nafasi za ajira mradi huo utakapokamilika, la sivyo serikali yake haitatoa hatimiliki ya ardhi hiyo.

Bi Waiguru alisema kuwa lazima hilo lifikiwe kupitia mwafaka utakaoandikwa kati ya serikali yake na taasisi hiyo.

Hata hivyo, Dkt Kibicho alimjibu kwa kusema kuwa ndiye kikwazo kikuu kwa mradi huo kuanza, kwani hautawafaa wenyeji wa kaunti hiyo pekee.

“Tusianze kumwaga tunapojaza. Ni ujinga. Sasa tunasema hawa (Kemri) waandike muafaka wao. Hata mkikosa kuajiriwa, si ni nyiyi mtakuwa mkuwauzia chakula? Si wale wanakunywa pombe watanunua kutoka kwenu? Hata yule angetaka kuoa, si ataoa hapa tu?”

Kauli hiyo ilimkasirisha vikali Bi Waiguru, akisema Dkt Kibicho anaingiza siasa kwenye suala hilo ili kujifaidi.

“Dkt Kibicho sasa amemzidi mamlaka Rais Kenyatta? Mbona anaingiza maslahi yake binafsi kwenye mradi huu? Ikiwa anataka kujiingiza kwenye siasa, basi anapaswa kujiuzulu wadhifa wake na kujiunga na wengine kwenye kampeni za mapema. Kwa sasa, anapaswa kuhakikisha kuwa kila Mkenya ana usalama wa kutosha,” akasema.

Januari 2020 Rais Kenyatta aliagiza suala hilo kusuluhishwa mara moja, kwa pande hizo kutia saini mwafaka ambao utakubaliwa na kila mmoja.

“Sisi hatuna shida na mradi huu. Ni mradi mkubwa. Hatutaki kuchelewesha ujenzi wake. Kwako gavana (Waiguru), maliza kutayarisha mwafaka ambao utatiwa saini na pande zote. Huu ni mradi utakaoifaa Kenya yote,” akasema Rais Kenyatta.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wanamlaumu Bi Waiguru kwa “kupotoshwa” na baadhi ya washirika wake wa karibu.

Miongoni mwa viongozi hao Bi Ngirichi, wabunge Kabinga Thayu (Mwea), Gichimu Githinji (Gichugu) kati ya wengine.

Wabunge hao wanaegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao unamuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022.

Duru zinaeleza kuwa makabiliano zaidi ya kisiasa yanatarajiwa, kwani mabwanyenye kadhaa wamekita kambi katika kaunti hiyo ili kuwafadhili wanasiasa watakaoendeleza maslahi yao.