MakalaSiasa

JAMVI: Sifuna atadhibiti ngalawa kwenye bahari ya kisiasa iliyofurika papa?

April 8th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

KATIBU Mkuu wa Chama cha ODM, Bw Edwin Sifuna, ana mlima wa kukwea anapojaribu kudhibiti ngawala ya upinzani nchini kwenye bahari iliyojaa papa, nyangumi na mawimbi makali ya kisiasa.

ODM ndicho chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini na kufikia sasa, kuna kila ishara kuwa huenda chombo hicho kikazamishwa na dhoruba kali zilizosababishwa na hatua ya kiongozi wa chama hicho Raila Odinga kuamua kushirikiana na aliyekuwa hasimu wake mkuu wa kisiasa, Rais Uhuru Kenyatta.

Kwa kuwa chama hicho ndicho kina ushawishi mkubwa zaidi, katibu mkuu ambaye ndiye msemaji rasmi humlikwa zaidi. Kila hatua na matamshi huchukuliwa kama msimamo rasmi wa chama.

Hivyo basi, hatua za Bw Sifuna zitaangaziwa kwa kina chama kinapojiandaa kumtafuta mwaniaji urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 hasa baada ya Bw Odinga kutangaza kwamba hatawania urais tena.

Wakati Bw Sifuna alipokezwa mamlaka hayo mwishoni mwa Februari mwaka huu, aligonga vichwa vya habari kwa matamshi yake makali dhidi ya wanasiasa walio na mipango ya kuvuruga chama hicho cha chungwa.

“Marafiki wetu wanafaa kujua unapoanza safari mkiwa watatu na mmoja wenu ni mrefu kuliko wengine, hafai kuambiwa atembee kwa magoti ili wote waonekane wenye kimo sawa. Anafaa kuambiwa abebe wale wafupi,” akasema kwenye hatua iliyozidisha hamaki ya vyama tanzu katika Muungano wa NASA ambavyo vilikuwa vikilalamika kudhulumiwa na ODM.

Ushirikiano wa chama hicho na vyama vingine vya upinzani kwa sasa umedhoofika pakubwa, hasa baada ya Bw Odinga kukutana na Rais Kenyatta. Chama hicho pia kimo hatarini kupoteza ushirikiano muhimu na mashirika ya kijamii ambao umekuwepo kwa miaka mingi, endapo muafaka kati ya ODM na Jubilee utamfanya Bw Odinga kupuuza ukiukaji wa sheria serikalini.

Mratibu wa muungano wa mashirika ya kijamii nchini, Bw Suba Churchill, alimshauri Bw Odinga ajihadhari sana na asisite kubatilisha msimamo wake wa ushirikiano na serikali iwapo ukiukaji wa sheria serikalini utaendelea.

 

Kibarua kigumu

Bw Sifuna kama msemaji wa chama atakuwa na kibarua kizito kudumisha ushirikiano huo muhimu hasa baada ya baadhi ya wanaharakati kudai kusalitiwa na hatua ya Bw Odinga kushirikiana na rais.

ODM pia kimelaumiwa kwa kumng’oa Bw Wetang’ula kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti na mahala pake kuchukuliwa na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo, mwanachama sugu wa ODM.

Hii si mara ya kwanza kwa chama hicho kushutumiwa kudhulumu wanachama katika muungano wa NASA na ndani ya chama.Miongoni mwa viongozi mashuhuri ambao walihama ODM kwa madai ya kukosa demokrasia ni Naibu Rais William Ruto, na aliyekuwa Mbunge wa Budalang’i, Bw Ababu Namwamba, ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Bw Namwamba alipohama ODM, alilalamika kuwa ingawa cheo cha katibu mkuu ni cha mamlaka makubwa, hakupewa uwezo na nafasi kutekeleza majukumu yake na hivyo akajitaja “jenerali bila silaha”.

Mwingine ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa chama, Bw Magerer Langat, na mwanaharakati wa upinzani, Bw Miguna Miguna, mshauri wa Bw Odinga kabla wakosane wakati wa utawala wa serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais Mwai Kibaki, kuanzia mwaka wa 2008 hadi 2013.Je, Sifuna atahimili changamoto hizi hadi mwisho?