MakalaSiasa

JAMVI: Tangatanga na Kieleweke wazua uadui kati ya wazee na makanisa

June 16th, 2019 3 min read

Na WANDERI KAMAU

TOFAUTI za kisiasa kati ya mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ sasa zimewagawanya wazee na makanisa kuwili katika ukanda wa Mlima Kenya, hali inayozua hofu kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo.

Migawanyiko hiyo imeenea kiasi kwamba, baadhi ya wanachama hao wametusiwa au hata kushambuliwa wanapozuru ngome za wapinzani wao.

Katika kisa cha Jumapili iliyopita, Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kiambu, Gathoni wa Muchomba, alizomewa katika kanisa moja katika Kaunti ya Murang’a, alipomkosoa mbunge wa Kandara, Alice Wahome kwa “kumtukana.”

Bi Wamuchomba ni wa kundi la ‘Kieleweke’ huku Bi Wahome akiwa wa kundi la ‘Tanga Tanga’ ambalo linamuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022.

Katika tukio jingine, zaidi ya wazee 2,000 walikutana katika uwanja wa Kabiru-ini katika Kaunti ya Nyeri Ijuma iliyopita, ambapo walipitisha kauli ya pamoja kutounga mkono azma ya Dkt Ruto, wakilalama kuwa “anazichukulia jamii za GEMA (Agikuyu, Aembu na Ameru) kwa urahisi.”

Mkutano huo, ambao ulipangwa kwa siri kubwa, unadaiwa kufadhiliwa na maafisa wakuu serikalini, ambao wanapinga azma ya Dkt Ruto kuwania urais.

Washiriki wake wakuu walikuwa wanachama wa Baraza la Wazee la Jamii ya Agikuyu (KCE) linaloongozwa na Bw Wachira Kiago.

“Wazee wamepitisha kwa pamoja lazima eneo hili litoe uamuzi huru kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa bila kushurutishwa kwa namna yoyote ile,” akasema Bw Kiago.

Kando na kundi hilo, kumekuwa na makundi mengine ya wazee ambayo yamekuwa yakiwatembelea Dkt Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ambapo yote yamekuwa yakimwahidi kuwa jamii za GEMA zitawaunga mkono ikiwa watawania urais kwenye chaguzi hizo.

Wiki mbili zilizopita, kundi moja la wazee kutoka kaunti ya Nakuru lilimtembelea Bw Odinga katika makazi yake ya Oponda, Siaya, na kumwahidi uungwaji mkono wa eneo hilo. Wazee hao waliongozwa na aliyekuwa mbunge wa Molo, Bw Njenga Mungai.

Ni matukio ambayo wachanganuzi wa kisiasa wanaonya kuwa yanaendelea kufifisha umoja wa kisiasa na kuondoa uwezekano wa uwepo wa sauti moja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Hali ya sasa ni ya kutia wasiwasi. Kwa mara ya kwanza, huenda eneo hili likashuhudia mgawanyiko mkubwa zaidi wa kisiasa, tangu mwanzo wa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mnamo 1992,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha USIU, Nairobi.

Kulingana na mchanganuzi huyo, kugawanyika kwa wazee huenda kukahatarisha upatikanaji wa umoja wa kisiasa, hata ikiwa ukanda huo unatarajiwa kutoa mwelekeo wake rasmi wa kisiasa kwenye kongamamo la Limuru III, lililopangiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

“Kwa mara ya kwanza, kuna hatari ya ukanda huo kutotii uamuzi ambao utatolewa katika kongamano la Limuru III. Ikumbukwe kuwa ingawa migawanyiko ya kisiasa huwa inashuhudiwa, ni nadra kwa wazee kugawanyika kama ilivyo sasa,” asema Prof Munene.

Makongamano hayo huwa muhimu katika kutoa mielekeo rasmi ya kisiasa ya ukanda huo, kila wakati unapojipata katika njiapanda ya kisiasa.

Kongamano la kwanza lilifayika mnamo 1963, wakati Mzee Jomo Kenyatta alitangaza kuvunjwa kwa nafasi ya makamu wa rais wa chama cha Kanu, na kubuni nafasi nane za uwakilishi katika mikoa yote minane.

Kongamano la pili lilifanyika mnamo 2012, wakati Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kujiondoa katika Kanu na kubuni chama cha TNA, ambacho kiliibuka kama chama rasmi cha ukanda huo kwenyeu uchaguzi mkuu waa 2013.

Wachanganuzi wanasema kuwa katika nyakati zote mbili, ukanda huo ulitii maamuzi yaliyofikiwa kwani uliwaunga mkono kikamilifu Mzee Kenyatta na mwanawe, Rais Kenyatta.

“Hali ni tofauti sasa. Kuna uwezekano wa baadhi ya makundi ya wazee na makanisa kuzingatia maamuzi yao huru, kwa kisingizio cha kutojumuishwa, kutengwa ama kutofaidika kwa maamuzi yaliyofikiwa awali,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Baada ya kuzomewa kwa Bi Wamuchomba, Kanisa la Kianglikana (ACK) katika Dayosisi ya Murang’a Kusini lilitangaza kuwapiga marufuku wanasiasa kuhutubu katika makanisa yake, hatua ambayo baadhi ya viongozi wameitaja kuegemea mrengo mmoja wa kisiasa.

“Uamuzi huo bila shaka unaonyesha mapendeleo ya kisiasa kwa mrengo wa Tanga Tanga. Mbona kanisa hilo limetoa agizo hilo tu baada ya kuzomewa kwa Bi Wamuchomba, ambaye ni wa mrengo wa ‘Kieleweke’? Hili ni dhihirisho wazi kuwa kanisa lenyewe linachangia katika migawanyiko ya kisiasa inayoendelea,” akasema mbunge mmoja wa kundi la ‘Kieleweke’ ambaye hakutaka kutajwa.

Lakini katika juhudi za kuzima migawanyiko hiyo, wachanganuzi wanasema kuwa ni lazima Rais Kenyatta avunje kimya chake, kwani kinachangia pakubwa.

“Kama kiongozi na msemaji wa kisiasa wa ukanda huo, Rais Kenyatta lazima ‘arudi nyumbani’ na kurejesha hali ya kawaida. La sivyo, kelele hizo zitazidi kuongezeka, hali inayohatarisha upatikanaji wa mwafaka maalum wa kisiasa,” asema Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.