JAMVI: Tetesi za vinara wa NASA kukutana kisiri na Ruto zilivyoyeyusha misimamo mikali

JAMVI: Tetesi za vinara wa NASA kukutana kisiri na Ruto zilivyoyeyusha misimamo mikali

MKUTANO wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga wiki iliyopita ulianza kuandaliwa hata kabla ya hafla ya kumuapisha Bw Odinga kama “rais wa wananchi” mnamo Januari 30.

Imefichuliwa kuwa wawili hao walianza kuzungumza moja kwa moja  kwa simu na kukutana mara kadhaa kwa siri kuweka mikakati ya kuzika tofauti zao.
Duru zinasema kuwa mazungumzo ya wawili hao kushirikiana yalianza punde tu baada ya uchaguzi wa marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26 mwaka jana ambao Bw Odinga alisusia.

Juhudi za kuwapatanisha wawili hao ziliendelezwa na mabalozi, viongozi wa kidini na Umoja wa Mataifa, japo baadhi ya washirika wa kisiasa wa viongozi hao walishikilia misimamo mikali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, alikiri kwamba shirika hilo lilimtuma aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obassanjo kuwapatanisha viongozi hao.

Imefichuliwa kuwa muafaka wao ulicheleweshwa kwa kuwa awali, kulikuwa na kutoaminiana.

“Kulikuwa na kutoaminiana hasa baada ya Bw Odinga kujiapisha kama rais wa wananchi. Hata baadhi ya washauri wa rais ambao hawakuwa wakifahamu mazungumzo hayo walitaka akamatwe kwa kujiapisha nao wale wa Bw Odinga hawakutaka mazungumzo.

Baadhi walitaka aunde serikali mbadala. Hii iliweka breki mazungumzo ambayo yangekamilika mapema Januari,” alisema mmoja wa waliohusika  kwenye mazungumzo hayo ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Inasemekana kuwa, wawili hao walikuwa wakizungumza kwa simu na hata kukutana usiku mara kadhaa baada ya marudio ya uchaguzi wa urais kufuatia shinikizo za jamii ya kimataifa.

 

Walivyozika tofauti

Kabla ya mkutano wa Ijumaa wiki iliyopita, walikutana katika nyumba ya afisa mmoja mkuu wa Mahakama ambapo waliamua kutangaza kuzika tofauti zao.

Watu wa familia zao na wazee wa jamii za Waluo na Wakikuyu pia walitekeleza wajibu muhimu kwenye mazungumzo hayo hadi viongozi hao wawili wakaamua kuacha tofauti zao za kisiasa na kushirikiana.

Mchango wa balozi wa Amerika Robert Godec pia ulitajwa kuwa mkubwa kupatanisha mahasimu hao wa kisiasa ambao tofauti zao zilizidi baada ya uchaguzi wa mwaka jana ambapo Raila anadai alipokonywa ushindi.

“Kwamba walitangaza kupatana saa chache kabla ya aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Amerika, Rex Tillerson kuwasili Kenya ilichukuliwa kwamba Amerika na jamii ya kimataifa ilihusika kuandaa muafaka huo,” asema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Geff Kamwanah.

Anasema muafaka huo ulimfaidi Bw Odinga ambaye uhusiano wake na jamii ya kimataifa ulikuwa umedorora tangu alipojiapishwa kuwa rais wa wananchi.

Duru zinaeleza kuwa, ni walipokutana kisiri mara ya mwisho katika nyumba ya afisa mmoja wa mahakama mtaani Karen ambapo waliafikiana kushirikiana na kukubaliana kuweka wazi uamuzi wao.

 

Kuepuka kulemaza mazungumzo 

Waliopanga mikakati ya kuwapatanisha wawili hao walihisi kwamba kuwashirikisha washauri wao wa kisiasa walio na misimamo mikali kungekwamisha mazungumzo.

Waliamua kuacha nje wanasiasa wenye misimamo mikali wakiwemo  vinara wenza wa Bw Odinga na naibu rais William Ruto. Hata hivyo, japo vinara wenza wa NASA Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula wamesema wazi kwamba hawakuhusishwa kwenye mazungumzo hayo, Bw Ruto hajasema wazi hakuyafahamu.

Wanamikakati hao walihisi kwamba,  mvutano kati ya serikali na upinzani ulikuwa hatari kwa uchumi na usalama wa nchi, hasa serikali ilipoanza kuwaandama viongozi wa upinzani.

Raila aliandamana na binti yake Winnie, wakili Paul Mwangi na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed naye Rais Kenyatta aliandamana na balozi Martin Kimani.

 

Siri

Imebainika kuwa mazungumzo ya simu kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta yaliwekwa siri chini ya usimamizi wa mkurungenzi wa ujasusi Philip Kameru ambaye inasemekana alitekeleza wajibu muhimu kupatanisha wawili hao.

Kulingana na duru za kuaminika, ni Bw Kameru aliyemshauri Rais Kenyatta kutomkamata Bw Odinga alipojiapishwa kuwa rais wa wananchi.

Kukubali kwa Bw Odinga kushirikiana na Rais Kenyatta kulichochewa na tetesi kwamba, vinara wenza katika NASA, ambao walisusia hafla ya kumuapishwa, walikuwa wakizungumza na Bw Ruto kuunda muungano wakilenga uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya kuhisi kwamba chama cha ODM cha Bw Odinga kilipanga kujitenga na muungano huo.

Wadadisi wasema hatua ya wawili hao kupatana itabadilisha mwelekeo wa kisiasa nchini katika siku chache zijazo.

“Kwa sasa, huenda ni vinara wenza wa NASA wanaolalamika lakini ukweli ni kwamba,  muafaka wa Raila na Uhuru utayumbisha Jubilee,” alisema Bw Sila Tirop, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

You can share this post!

JAMVI: Mkataba wa Raila na Uhuru wazalisha mayatima wa...

Aapa kuadhibu mume wake kwa kumchunguza kama ana mpango wa...

adminleo