MakalaSiasa

JAMVI: Uhuru akanganya wanasiasa kwa karata wasioelewa

June 7th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta anaendelea kuwashangaza wengi kuhusu karata anayocheza kwenye urithi wake hapo 2022, ikiwa si dhahiri hadi sasa kuhusu kiongozi anayempendelea kuwa mrithi wake.

Katika siku za hivi karibuni, Rais Kenyatta amekuwa akikutana, kucheka na hata kutangamana na viongozi wakuu wa siasa nchini, hali ambayo wadadisi wanasema huenda imewaacha kwenye njiapanda.

Kufikia sasa, wale wanaoonekana kuwa wagombea wakuu wa wadhifa huo ni Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) usalia Mudavadi, Seneta Gideon Moi (Baringo) na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Tangu kubuni handisheki na Rais mnamo Machi 2018, Bw Odinga amekuwa akifasiriwa kuwa kiongozi anayependelewa na Rais Kenyatta kuwa mrithi wake kutokana.

Upeo wa ukaribu wao ulikuwa mnamo Jumanne wiki hii, ambapo wawili hao walinaswa kwenye video wakisafiri kwenye gari moja jijini Nairobi usiku, duru zikieleza walikuwa wakikagua miradi inayoendeshwa na Baraza Jipya la Kusimamia Jiji (NMS).

Mnamo Jumatatu, kwenye sherehe za Sikukuu ya Madaraka katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta na Dkt Ruto walionyesha ukuruba wa karibu, huku hata wakivalia mavazi yaliyofanana.

Hili ni licha ya uhusiano wao unaoonekana kudorora kila siku.Mnamo Desemba mwaka uliopita, Rais Kenyatta alisafiri pamoja na Bw Mudavadi kwenye ndege yake rasmi katika hafla ya kijeshi mjini Garissa, hali iliyoibua maswali kwamba huenda anamjenga Bw Mudavadi kuwa mrithi wake.

Mapema mwezi uliopita, Chama cha Jubilee (JP) kilibuni mkataba na Kanu, hali iliyofasiriwa kama njia ya Rais Kenyatta kumwandaa Seneta Moi kuwa mrithi wake, ili “kurejesha mkono” kwa familia ya Mzee Daniel Moi.

Mzee Moi ndiye aliyemwidhinisha Rais Kenyatta kuwa mgombea wa urais wa Kanu mnamo 2002, baada yake kustaafu rasmi kama rais.

Na baada ya mkataba ya Jubilee na Kanu, Bw Musyoka alisema kuwa Wiper imempa kibali kuanza mazungumzo na Rais Kenyatta kuhusu uwezekano wa kubuni muungano kama huo.

Ataunga nani mkono?

Na kufuatia mwelekeo huo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa ingawa nia ya Rais Kenyatta ni kuwaleta wanasiasa wote kwenye kapu moja, anafahamu lengo lake la mwisho.

Kwenye mahojiano, Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, anamtaja Rais Kenyatta kama mwanasiasa mjanja, anayefahamu kwa undani kuhusu karata anayocheza.

Hata hivyo, anawataja wanasiasa wengine, hasa Mabw Odinga na Ruto, kama wanasiasa werevu pia, ikizingatiwa wote walilelewa kisiasa na Mzee Moi.

“Rais Kenyatta alilelewa kisiasa na Mzee Moi. Hivyo, anafahamu kuhusu karata anayocheza. Yuko katika mazingira magumu, yanayomhitaji kuwa mwerevu sana. Walielewana na Bw Odinga kwa msingi wa kuleta utulivu wa kisiasa nchini, hivyo lazima ahakikishe kuwa hajamtenga kwa vyovyote vile. Pia, waliungana na Dkt Ruto kwa msingi wa ‘deni’ la kisiasa mnamo 2012. Hivyo, hawa ni kama watoto wawili ambao ni vigumu kuwatenga,” asema Prof Munene.

Na ingawa taswira iliyopo ni kuwa Rais amekosana na Dkt Ruto, anasema kuwa itabidi Rais azime dhana hiyo kijanja, kwani kikatiba, Dkt Ruto bado ni naibu wake na mwanasiasa ambaye pia ni mwanafunzi wa Moi.

Wadadisi wanasema kuwa 2022 ingali mbali ambapo kama mwanasiasa, Rais Kenyatta anafahamu kwa undani kuwa wanasiasa wanaweza kubuni miungano licha ya tofauti zao.

“Huu ni mwelekeo tutamwona Rais akizingatia kwani anataka kubuni mazingira ambapo atatekeleza ajenda yake ya maendeleo huku akiangalia mbele kuhusu mchakato wa urithi wake,” asema Prof Munene.