MakalaSiasa

JAMVI: Uhuru pabaya kwa kusahau baadhi ya maeneo ya Gema katika uteuzi wake

February 11th, 2018 3 min read

Na WANDERI KAMAU

Kwa Muhtasari:

  • Mirengo mitatu inang’ang’ania ushirikishi zaidi wa kisiasa serikalini, hasa baada ya wanasiasa wenye ushawishi kukosa kutajwa mawaziri
  • Kuchipuka kwa mirengo hiyo mitatu kunaashiria kibarua kipya kwa Rais Kenyatta
  • Rais Kenyatta anakejeliwa kwa kutomteua Bi Martha Karua kama waziri, licha ya kuahidi kwamba angemteua
  • Wanasema kuwa mwelekeo huo ni hatari, ambao huenda ukazua mgawanyiko mkubwa, hasa anapojitayarisha kung’atuka uongozini

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kukosa kuwateua baadhi ya wandani wake imezua uasi wa kichinichini katika ukanda wa Mlima Kenya, hali ambayo imegawanya eneo hilo katika mirengo mitatu ya kisiasa.

Mirengo hiyo inang’ang’ania ushirikishi zaidi wa kisiasa serikalini, hasa baada ya wanasiasa wenye ushawishi kukosa kutajwa katika baraza la mawaziri na Rais Kenyatta.

Mrengo wa kwanza unahusisha kaunti za Meru, Embu, Tharaka-Nithi na Kirinyaga. Mrengo wa pili unahusisha kaunti za Kiambu na Murang’a, huku mrengo wa tatu (Aberdare Group) ukishirikisha kaunti za Nyeri, Nyandarua, Laikipia na Nakuru.

Kulingana na wachanganuzi, kundi la kwanza linadai kutengwa na Bw Kenyatta, hasa baada ya kukosa kuteuliwa kwa Seneta Kithure Kindiki (Tharaka-Nithi) ambapo walimpigania kuteuliwa kama waziri.

Baadhi ya viongozi wa kaunti hizo wamejitokeza kuelezea kutoridhishwa kwao na uteuzi wa gavana wa zamani wa Meru, Peter Munya, wanayedai kutowakilisha maslahi ya wakazi hao.

 

“Ukiritimba wa kisiasa”

Chini ya uongozi wa Gavana Muthomi Njuki wa Tharaka-Nithi, kundi hilo linaamini kwamba kuteuliwa kwa Bw Munya ni uendelezaji wa “ukiritimba wa kisiasa” wa jamii ya Ameru.

“Tunahisi kutengwa kabisa na utawala wa Jubilee, licha ya kujitokeza pakubwa kumpigia kura Rais Kenyatta,” akalalama Bw Njuki.
Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, kundi la Kiambu-Murang’a linaonekana kuridhika na uteuzi wa watu kadhaa katika baraza hilo.

Miongoni mwa walioteuliwa ni James Macharia (Uchukuzi) ambapo anatoka katika Kaunti ya Murang’a na Joe Mucheru (anayetoka katika Kaunti ya Kiambu) ila ana makazi yake katika Kaunti ya Nyeri.

Kundi la tatu, maarufu kama ‘Aberdare Group’ halijafurahia kuteuliwa kwa Bw Mwangi Kiunjuri kama Waziri wa Kilimo.

Kulingana na Profesa Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa, kuchipuka kwa mirengo hiyo mitatu kunaashiria kibarua kipya kwa Rais Kenyatta, ikizingatiwa kwamba msingi wake mkuu ni kushinikiza uteuzi wa watu maarufu ambao waliachwa nje.

“Tathmini ya ndani inaonyesha kuwa msingi mkuu wa makundi hayo ni ung’ang’aniaji wa mamlaka, hasa kwa wanasiasa ambao waliachwa nje,” asema Prof Njoroge.

 

Mgawanyiko

Aidha, anatoa mfano wa kutotajwa kwa aliyekuwa mbunge wa Kigumo, Jamleck Kamau kama waziri ama naibu waziri, kama jambo ambalo huenda likazua uasi na mgawanyiko katika kundi linaloshirikisha kaunti za Murang’a na Kiambu.

“Kuna hatari kubwa ya Bw Kamau kujiunga na wanasiasa wengine waasi kama aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, hivyo kufanya kipindi cha pili cha Bw Kenyatta kuwa kigumu.

Ni wakati wa yeye (rais) kuwatafutia mahali baadhi ya wanasiasa hao, ili kuepuka uwezekano wa msambao wa uasi wa kisiasa,” asema Prof Njoroge.

Msukumo wa ukanda wa Mlima Kenya Mashariki (Embu, Meru na Tharaka-Nithi) ni hisia kwamba Rais Kenyatta ‘aliwazawidi’ watu ‘wasiofaa.’

Mchanganuzi wa kisiasa Daudi Mwenda anasema kuwa uteuzi wa Bw Munya kama Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki ni ishara ya wazi kwamba ni kama Rais Kemyatta hatambui mchango wao katika ushindi wake.

“Matarajio ya wengi yalikuwa kwamba angaa Bw Kenyatta angaliwazingatia baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Tharaka. Hii ni kwa kuwa tayari ‘amezituza’ jamii za Meru na Embu, kupitia uteuzi wa Bw Munya na Bi Cecily Mbarire kama mbunge maalum,” asema Bw Mwenda.

 

Kutomteua Bi Karua

Wengi pia wanamkosoa Bw Kenyatta kwa kutomteua Bi Martha Karua kama waziri, licha ya kuahidi kwamba angemteua, ikiwa angeshindwa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana wa Kirinyaga na Bi Anne Waiguru.

Malalamishi kama hayo ndiyo yaliyo katika kaunti zilizo katika kaunti zinazojumuisha kundi la ‘Aberdare Group.’

Wachanganuzi na viongozi katika eneo hilo wanapinga uteuzi wa Mabw Joe Mucheru na Mwangi Kiunjuri, wakiwataja kuwa “wageni” na kutofaa katika eneo lao.

Baadhi ya viongozi wa Nyeri wamejitokeza kulalamika kwamba Bw Mucheru si mmoja wao, huku Bw Kiunjuri akidaiwa kuwa mwakilishi wa Kaunti ya Laikipia.

“Kwa mara nyingine, Rais Kenyatta ameisahau Kaunti ya Nyeri, licha yake kujitokeza pakubwa kumpigia kura. Hatuna waziri hata mmoja katika baraza lake.

Aliowachagua (Mucheru na Kiunjuri) si wakazi asilia wa Kaunti ya Nyeri. Tunamtaka kutimiza ahadi yake,” akasema mbunge wa Kieni Kaniini Keega.

Mchanganuzi na wakili Wahome Gikonyo anawataja wawili hao kutokuwa “wawakilishi wa kisiasa wa eneo hilo.”

 

Hawapendezi

“Mabw Kiunjuri na Mucheru wamehudumu katika kipindi cha kwanza cha rais, ambapo imedhihirika kwamba hawapendezi. Hawajaonekana kumjenga Rais Kenyatta. Ni wakati rais anafaa kutathmini msimamo wake,” asema Bw Gikonyo.

Wakosoaji wa Bw Kenyatta wanataja uteuzi wake kuwa unaoendeleza “ukiritimba wa kisiasa wa Kaunti ya Kiambu” kama alivyofanya babake, marehemu Mzee Jomo Kenyatta.

Wanasema kuwa mwelekeo huo ni hatari, ambao huenda ukazua mgawanyiko mkubwa, hasa anapojitayarisha kung’atuka uongozini.

“Ni wakati mwafaka azibe nyufa zote ambazo huenda zikaleta mgawanyiko katika ngome yake,” asema mwanaharakati wa kisiasa Linford Mutembei.