Makala

JAMVI: Uhuru, Raila wana njama gani BBI?

November 8th, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

MKONDO ambao juhudi za kubadilisha katiba kupitia mchakato wa Maridhiano (BBI) umechukua, unaonyesha kwamba kuna njama fiche katika mpango huo.

Wadadisi wa siasa wanahisi kwamba ingawa vinara wa mchakato huo, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wamekuwa wakisema kuwa nia yao ya kuasisi mpango huo ni kuunganisha Wakenya, mkondo ambao wamechukua utaufanya usitimize malengo ya kufaidi umma kikamilifu na kuzua migawanyiko zaidi.

“Kuna sababu ambazo hawakufichua ambazo wanataka kutimiza kupitia mpango huo na watakaoumia ni Wakenya. Kuna siri waliyonayo na ndio sababu wamekuwa wakiendesha mpango huo wakiwa wawili na kuwashinikiza viongozi wengine wauunge. Wakenya wanafaa kuwa makini,” asema Bi Lucia Ayiela mwanachama wa vuguvugu la Kongamano la Mageuzi (KLM).

Wadadisi wanasema kuwa kufunga milango ya mazungumzo kuhusu ripoti ya mwisho ya BBI, Rais Kenyatta na Bw Odinga walionyesha kuwa wameridhika kwamba ilivyoandikwa itawasaidia kutimiza malengo yao hata kama hayaungwi na Wakenya wote.

Mchanganuzi wa siasa Kelly Kirathe anasema kuwa hatua hiyo imeonyesha kuna lengo tofauti la BBI bali na kuunganisha Wakenya kwa sababu kuna makundi mengi yanayolalamika kwamba ripoti hiyo haikutilia maanani maslahi yao.

Wakulima, wanawake, mawakili, watu walio na ulemavu na jamii ya wafugaji ni miongoni mwa makundi ambayo yanataka ripoti hiyo ijadiliwe zaidi.

Naibu Rais William Ruto na washirika wake wa kisiasa pia wamekosoa baadhi ya mapendekezo ya ripoti hiyo wakisema yanahujumu ugatuzi, mfumo wa uchaguzi, mahakama na haki ya Wakenya.

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Gavana wa Kitui Charity Ngilu pia walipendekeza ripoti ifanyiwe mageuzi ili kuhakikisha itatimiza lengo la kuunganisha Wakenya na ushirikishi serikalini.

Wadadisi wanasema maoni kuhusu mapendekezo ya ripoti ya mwisho sio sawa na yaliyotolewa wakati wa kuiandaa wanavyodai wanaokataa ijadiliwe.

Kwenye mkutano uliohudhuriwa na wabunge walioalikwa kujadili mchakato huo huko Naivasha mapema wiki hii, iliamuliwa kuwa hakutakuwa na mazungumzo zaidi kuihusu na mapendekezo yatawasilishwa kwa kura ya maamuzi yalivyo.

Hatua hii itafanya kuwe na kampeni kali ambazo zinaweza kugawanya nchi badala ya kuunganisha.

Kulingana na Kirathe, kukataa mabadiliko katika ripoti hiyo kunawafanya Wakenya kuamini kwamba Uhuru na Raila wana mipango tofauti na wanayoambia Wakenya.

“Wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti hiyo wiki mbili zilizopita, Uhuru na Odinga walisema kwamba hawataki kura ya maamuzi kugawanya Wakenya jambo ambalo linawezekana kwa kukumbatia maoni ya wasioridhishwa na mapendekezo ya mwisho ya ripoti hiyo. Hata hivyo, inashangaza hatua waliyochukua imefungua milango ya kampeni kali ya kuipinga. Hii inaibua maswali kuhusu lengo lao,” asema Bw Kirathe.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen anashikilia kuwa nia ya wawili hao itadhihirika wakati wa utekelezaji wa ripoti hiyo ikiwa itapitishwa kwenye kura ya maamuzi.

“Mswada wa mabadiliko ya katiba wa BBI ni mzuri sana kwa wagombeaji wa urais pekee lakini ni mbaya sana kwa uthabiti wa nchi,” asema Murkomen na kuongeza kuwa itanufaisha wanasiasa huku raia wa kawaida wakipoteza.

Kulingana na KLM, mabadiliko yaliyopendekezwa kwenye BBI sio muhimu kwa Wakenya. Kundi hilo linasema kwamba mchakato huo ni siri ya watu wawili pekee na ndio wanajua ukweli kuhusu.

“Ibainike kuwa ni Uhuru na Odinga walioteua kamati iliyoongoza mpango huu na kuandika ripoti hii. Kuna kila sababu ya kuamini kwamba wana njama ambayo Wakenya hawajui,” kundi hilo linaloongozwa na mwanaharakati mashuhuri John Githongo linasema.

Kuna wanaohisi kwamba kuna juhudi za kuua demokrasia na kupokonya mahakama uhuru wake. Mchanganuzi wa siasa na masuala ya utawala Ndungu Wainaina anasema kwamba kuna njama ya kutumia BBI kufanya mahakama, polisi, bunge na Idara ya mashtaka ya umma kuthibitiwa na rais.

“Ikiwa Wakenya hawataweza kukomboa mahakama, polisi,bunge na ofisi ya mashtaka ya umma kutoka mikono ya wanasiasa wanaoongoza serikali, utawala wa demokrasia inayoongozwa na sheria utabaki kuwa ndoto. Hatuhitaji katiba mpya. Kinachohitajika ni kutekeleza katiba ya 2010,” asema.

Wadadisi wanasema kufunga milango ya mazungumzo kuhusu mapendekezo ya ripoti hiyo, kunalenga kuzuia njama isifichuke.

“Hii ndio sababu wanajaribu kusiwe na mdahalo kabla ya kura ya maamuzi,” asema Kirathe.

Wataalamu wa masuala ya katiba wanasema kwamba ingawa ina mapendekezo mazuri hasa kuongeza pesa kwa serikali za kaunti, ngoma itakuwa utekelezaji wake ikipitishwa kwenye kura ya maamuzi.

“Hapo ndipo shubiri iliyopakwa sukari kwa sasa itabainika kuwa ni sumu,” asema Victor Okere, mwanaharakati wa katiba.

“Kuna vifumba macho kuhusu mchakato huu. Utakuwa pigo kwa katiba ya 2010 ambayo haijatekelezwa. Kuna gharama kubwa ya kuutekeleza ukipita kwenye kura ya maamuzi na ni wakati huo ambapo Wakenya watabaini ukweli,” asema.

Wandani wa Ruto wamekuwa wakidai BBI inalenga kuzima azma yake ya kugombea urais, wanaharakati wanasema inalenga kuhujumu mahakama na utawala wa sheria lakini uamuzi wa kufunga mdahalo umewaacha nje ya wito wa kuunganisha Wakenya.