MakalaSiasa

JAMVI: Ukabaila ulivyowapasua UhuRuto

July 19th, 2020 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

IMEIBUKA kuwa shinikizo za kibiashara, ukabila na unabii wa Mugo wa Kibiru wa Karne ya 18/19 ndio kiini cha utengano wa sasa wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto.

Kwa mujibu wa wachanganuzi, mikutano ya mabwanyenye wa jamii ya Agikuyu pamoja na mabaraza ya wazee na Rais Uhuru yalimwekea presha za kuchukulia suala la uchumi wa Mlima Kenya pamoja na ushawishi wa eneo hilo kisiasa kiasi kwamba Dkt Ruto alitambuliwa kama asiye na uwezo wa kuyalinda maslahi hayo.

Katika mikutano hiyo ambayo ilianza punde tu baada ya Rais Uhuru kuchaguliwa mwaka wa 2013, makundi hayo mawili yalikuwa na wasiwasi kwamba Dkt Ruto alikuwa ametunukiwa urithi wa urais mapema sana na pia kwa urahisi bila kuzingatia masuala nyeti ya kijamii eneo la Mlimani.

“Ni katika mikutano hiyo ambapo Rais Uhuru alikumbushwa kuhusu unabii wa mwendazake Mzee Kibiru ambaye ameorodheshwa katikia kumbukumbu za jamii hiyo akisema kuwa “Urais wa Kenya baada ya mwanzilishi hayati Mzee Jomo Kenyatta (1963-1978) utamwendea mtu mwingine wa jamii ndogo (Daniel Moi 1978-2002) na ukisharejea kwa Agikuyu (Rais Mwai Kibaki na Uhuru (2002-2022), hautawahi kutoka huko tena,” afichulia Jamvi la Siasa mmoja wa aliyeshiriki mikutano hiyo.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mkuu wa mikoa kadhaa kwa muda mrefu Joseph Kaguthi, “Rais alikumbushwa kuwa yalikuwa makosa kumuahidi Dkt Ruto urais kwa urahisi na pia mapema hata kabla ya majadiliano ya kina kutekelezwa kati ya wadau wa kijamii.”

Mwaka wa 2013 na 2017 Rais Uhuru alinukuliwa kwa kiwango kikuu akitangaza kuwa angetawala kwa kipindi cha miaka 10 na kisha Dkt Ruto achukue usukani kwa kipindi cha miaka 10.

Kaguthi aliambia ukumbi huu kuwa wandani wengi wa Rais hawakuridhishwa na suala hilo kwa kuwa hisia za urais wa Mzee Daniel Moi wa miaka 24 za jinsi alivyofukarisha eneo hilo zilikuwa zingalipo na machungu yake.

“Rais alikumbushwa kuwa wakati urais ulipowatoka watu wa eneo la Mlimani, hata tekenye/funza ziliwavamia wenyeji kutokana na umasikini na hawakuwa tayari kuona urais ukiwatoka kwa urahisi jinsi Uhuru alikuwa akiupokeza Ruto,” asema.

Rais anasemwa kuwa alikubaliana na ushauri huo na ndipo akawaagiza wote wasubiri Dkt Ruto awasaidie kujipa awamu ya pili Ikuluni na baada ya hapo mikakati iwekwe ya kulinda maslahi hayo ya kibiashara (kikabaila), kikabila na kiuchumi.

Na ndipo baada ya uchaguzi wa 2017 ambapo baada ya Dkt Ruto kumsaidia Uhuru kushinda, masaibu ya uhasama, kutengwa na kudharauliwa yakaanza kutekelezwa hadi sasa ambapo wandani wake wametimuliwa kutoka kwa nyadhifa za hadhi katika kamati za bunge na pia wakitengwa kutoka makao makuu ya chama cha Jubilee.

Kwa mujibu wa mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, maslahi hayo ya ukoloni mamboleo yakitetewa na mabwanyenye wenye ukwasi mkuu nchini kutoka Mlima Kenya yalichochea pia uhasama kati ya Rais na Dkt Ruto.

“Tunaongea kuhusu wafanyabiashara ambao haja yao kuu ni pesa katika kila kona ya maisha yao hapa duniani. Hawana fikira zozote za mwananchi wa kawaida na vile angetaka kuishi maisha yake ya kisiasa na kiuchumi. Kwao, maisha ya watu ni ya kuchuuzwa pesa,” asema.

Anasema mabwanyenye hao walimwendea Rais Uhuru na njama fiche kuwa ni lazima angeacha taifa hili katika mikono inayoaminika kuwa haitasambaratisha biashara zao kupitia njia za kupora na kuhangaisha.

Hapo ndipo kulizinduliwa njama za kumwangazia Dkt Ruto kama mwizi na mnyakuaji ili Rais aelekeze vitengo vya kupambana na makosa ya jinai na pia ufisadi dhidi ya Dkt Ruto.

“Nia kuu ya mabwanyenye hao ilikuwa kupenyeza biashara zao katika ngome nyingine za nchi hii kwa kuwa tayari wamejipenyeza Mlima Kenya. Kwa kuwa Raila Odinga ndiye mwanasiasa anayeorodheshwa wa pili katika uwezo wa kuwaleta pamoja raia wengi kwa mrengo wake wa kisiasa, wakamshawishi Rais amkumbatie.”

ndio awasaidie kupenya maeneo yanayoorodheshwa kama ngome zake. Ndio sababu unapata kwamba mabweanyenye wengi wa Mlima Kenya hujumuika katika siasa za Raila,” akasema.

Aidha, mabaraza ya wazee yalimkumbusha Rais kuwa alikuwa akifanya makosa kwa kumtwika DP Ruto makuu ya kiserikali bila ya kuzingatia masilahi ya Mlimani.

Kwa mujibu wa Mwakilishi wa wanawake wa Murang’a Bi Sabina Chege, kuliibuka siasa za “ni nani amejengwa katika Mlima Kenya ili hata ikiwa Dkt Ruto angeibuka na urais, asimamie masilahi ya Mlimani katika serikali hiyo.”

Bi Chege anasema kuwa “Dkt Ruto mwenyewe ako na viungo vyake thabiti, Raila ako na wandani wake aliowajenga na pia maeneo mengine yako na wao ambao wanatambulika kama wawakilishi wao katika hali za kisiasa 2022.”

Anahoji ni kwanini Mlima Kenya hakuna amejengwa na Rais na ndipo, Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi anafichua, kulizuka haja ya kumjenga msimamizi wa Mlimani katika siasa za 2022.

“Hapo ndipo unapata kwa sasa tukiwa mbioni kumweka aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth katika siasa za urithi. Ni lazima sasa tuwe na atakayetuwakilisha katika siasa hizo za 2022. Pia, ni katika hali hii ambapo kumeibuka haja kubwa ya kusukuma mpango wa, na ripoti ya, maridhiano (BBI) ili serikali ipanuliwe pale juu na kuwe na vyeo vya kugawanwa kulingana na kura za kimaeneo,” asema.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau anakiri kwamba “rais ameshinikizwa kuona kwamba alikuwa amenoa kuahidiana urais kwa urahisi hivyo na sasa tuko katika mkondo wa kurekebisha hali. Hatuko na Dkt Ruto ikiwa hatakubali kwanza kura zetu 8 milioni haziwezi zikamwendea ndio aongeze zake 2 milioni na kisha awe rais ambaye hata hajatwambia atatupa nini kama fidia ya kura hizo.”

Anasema kuwa masuala hayo yote ndiyo yamechangia uhasama wa kimaoni kati ya Rais Uhuru na Dkt Ruto “lakini sio eti tuna shida na mtu yeyote, bali tunataka tu eneo la Mlima Kenya lilindwe lisijipeleke kwa ndoa ya kisiasa 2022 ambayo itarejesha funza katika maisha ya wenyeji kupitia utawala wa kutoka nje ya Mlima Kenya.