JAMVI: Utata wa BBI tishio kwa Handisheki

JAMVI: Utata wa BBI tishio kwa Handisheki

Na LEONARD ONYANGO

UTATA ambao umegubika Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) umegawanya wandani ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wandani wa Bw Odinga wanashuku kuwa wenzao wa upande wa Rais Kenyatta walihusika katika kupeleka mswada bandia kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Lakini wandani wa Rais Kenyatta wamekana madai hayo huku wakiitaka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kuchunguza kiini cha mswada bandia wa BBI. Utata huu ulitokea baada ya kamati ya wataalamu waliotwikwa jukumu la kukagua Mswada wa BBI kubaini kuwa mabunge ya kaunti 30 yalijadili na kupitisha mswada bandia.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, ni mabunge ya kaunti 13 pekee ambayo yalijadili mswada halisi wa BBI. Wataalamu hao pia walibaini kwamba mswada wa BBI una dosari za kisarufi.

Hata hivyo, aliyekuwa Katibu wa Jopokazi la BBI Paul Mwangi amesema kuwa makosa hayo yatarekebishwa baadaye na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki baada ya mswada huo kupitishwa na Bunge.

“Kazi ya Bunge ni kusema ‘Ndiyo’ au ‘La’. Sheria ya Kenya inampa mamlaka Mwanasheria Mkuu kuandika mswada kwa lugha inayoeleweka na kuondoa makosa ya kisarufi katika mswada,” alisema Bw Mwangi.

Baadhi ya mawakili wamesema kuwa ikiwa tofauti iliyopo kati ya mswada bandia na mswada halisi wa BBI ni ndogo, haitaathiri mchakato wa kutaka kubadilisha Katiba ya 2010.

Lakini tofauti ikiwa kubwa haswa katika masuala muhimu kama vile muundo wa serikali, safari ya kutaka kurekebisha Katiba ya 2010 kupitia mswada wa BBI iliyoanza 2018, itakuwa imefikia kikomo.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala anasema kuwa mswada unaoshughulikiwa na Seneti ni tofauti na ulioko mbele ya Bunge la Kitaifa.

“Tunashughulikia miswada miwili tofauti. Iwapo tutafanya kosa la kuipitisha, watu wataenda mahakamani na korti itabatilisha mchakato mzima wa BBI,” ameonya Bw Malala.

Wakili wa masuala ya sheria Bobby Mkangi naye anasema kuwa ikiwa kweli kaunti 13 pekee ndizo zilijadili na kupitisha mswada halisi, huo ndio mwisho wa BBI.

Bw Mwangi ambaye ni mmoja wa wawakilishi wa Bw Odinga katika jopokazi la BBI, Alhamisi, alionekana kulaumu tume ya IEBC kwa kupeleka mswada bandia kwa mabunge 30 ya kaunti.

Lakini mwenyekiti wa IEBC alipuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa alipeleka katika mabunge ya kaunti nakala alizopewa na sekretariati ya BBI inayoongozwa na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru.

Katibu wa Masuala ya Kisiasa wa ODM Opiyo Wandayi anasema kuwa huenda mswada bandia ulipenyezwa katika Kamati ya Sheria iliyopewa jukumu la kutathmini mswada huo na watu wanaopinga BBI.

Bw Wandayi analaumu kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Kangema Muturi Kigano na Seneta wa Nyamira Okongo Omogeni kwa kujaribu kusambaratisha BBI.

Lakini wandani wa Bw Odinga waliozungumza na Taifa Jumapili na kuomba majina yao yabanwe wanasema kwamba kujitokeza kwa mswada bandia ni ‘mchezo mchafu ambao tunachezewa na wenzetu ambao ni wandani wa Rais’.

“Kabla ya kuwasilishwa kwa IEBC, Mswada wa BBI ulikuwa ukibadilishwa mara kwa mara na watu wenye ushawishi serikalini. Kwa mfano, kumekuwa na ripoti kwamba mswada wa BBI ambao Bw Odinga na Rais Kenyatta walikabidhiwa katika Kaunti ya Kisii ni tofauti na uliozinduliwa wakati wa kuanza kwa ukusanyaji wa saini katika jumba la KICC. Kuna uwezekano watu wenye ushawishi serikalini wamehusika katika usambazaji wa mswada bandia,” akasema mmoja wa viongozi wa ODM.

Mwanaharakati wa haki za kibinadamu Ndung’u Wainaina naye anasema kwamba mchakato wa BBI umekuwa na mambo tele yenye utata tangu ulipozinduliwa miaka mitatu iliyopita.

“BBI ilitokana na maafikiano ya viongozi wawili; Rais Kenyatta na Bw Odinga, bila Wakenya kuhusishwa. Jopokazi la BBI lilitumia mamilioni ya pesa za walipaushuru bila bajeti kuidhinishwa na Bunge. BBI ni mradi wa viongozi wakuu serikalini na wala hauna manufaa kwa Wakenya,” asema Bw Wainaina.

You can share this post!

Wanafunzi 3 wa chuo kikuu waliotekwa nyara wauawa

JAMVI: Katika hizi ziara zake Oparanya ni ‘fuko’ au ni...