Siasa

JAMVI: Vita vya ubabe kati ya Uhuru na Ruto vyahamia Magharibi

June 14th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

VITA vya ubabe wa kisiasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto sasa vimehamia katika eneo la Magharibi baada ya viongozi hao kugawana wanasiasa wa eneo hilo.

Ubabe huo ulijitokeza wazi Ijumaa ambapo kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula pamoja na wabunge wapatao 20 kutoka Magharibi kuandaa mkutano wa wanahabari na kumshambulia Rais Kenyatta.

Walidai kuwa Rais Kenyatta ametelekeza ukanda wa Magharibi na amekuwa akielekeza miradi yote ya maendeleo katika eneo la Mlima Kenya.

Kulingana na duru za kuaminika, viongozi hao wa Magharibi walihutubia wanahabari baada ya baadhi yao kukutana na Dkt Ruto.

Naibu Rais Ruto alikiri kwamba alikutana na wanasiasa wa chama cha Ford-Kenya na ANC afisini kwake katika mtaa wa Karen, Nairobi.

“Tulifanya majadiliano kuhusu miradi ya maendeleo nchini na viongozi wa Magharibi kutoka chama cha Jubilee, Ford Kenya na ANC,” akasema Dkt Ruto kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kulingana na Wetang’ula, wabunge na maseneta 27 kutoka Magharibi waliandaa mkutano kujadili suala la maendeleo katika ukanda wa Magharibi kabla ya kuhutubia wanahabari.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni mbunge Charles Gimose (Hamisi), Petronila Were (Seneta Maalumu) Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Justus Murunga (Matungu), Injendi Malulu (Malava), Janet Nangabo (Mwakilishi wa Kike, Tans Nzoia), Mwambu Mabonga (Bumula) na John Waluke (Sirisia).

Wengine ni Chris Wamalwa (Kiminini), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Alfred Agoi (sabatia), Sakwa Bunyasi (Nambale), Tindi Mwale (Butere), Didmus Barasa (Kimilili), Catherine Wambilianga (Mwakilishi wa Kike, Bungoma), Ayub Savula (Lugari), Omboko a (Emuhaya), Ferdinand Wanyonyi (Kwanza) na Edward Oku Kaunya wa Teso Kaskazini.

“Bajeti iliyosomwa Alhamisi na waziri wa Fedha, Ukur Yatani, haikutenga mradi wowote kwa ajili ya eneo la Magharibi. Sekta ya sukari imesambaratika. Sekta za pamba, mahindi na kahawa zimeporomoka,” akasema Bw Wetang’ula.

“Benki ya Dunia iliipa Kenya mabilioni ya fedha kuinua sekta ya kahawa. Lakini Rais Kenyatta amepeleka fedha zote katika eneo la Mlima Kenya na kuacha eneo la Magharibi ambalo linakuza pamba,” akaongezea.

Bw Wetang’ula alidai kuwa fedha zilizotengewa kilimo cha pamba zimewekwa katika utanzu wa serikali badala ya kuwapelekea wakulima.

Bw Mudavadi alimshutumu Rais Kenyatta na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya kwa ‘kuwahadaa’ wakazi wa eneo la Magharibi kuhusu ufufuaji wa sekta ya sukari.

“Rais Kenyatta alibuni jopokazi lililochunguza kiini cha kuporomoka kwa sekta ya sukari katika eneo la Magharibi. Jopo hilo lililoongozwa na Gavana Oparanya, lilitoa ripoti yake na imefichwa wala hakuna chochote kinachoendelea,” akadai Bw Mudavadi.

Hiyo si mara ya kwanza kwa Naibu Rais kukutana na viongozi wa vyama hivyo viwili vyenye ufuasi mwingi kutoka magharibi mwa Kenya. Mnamo Juni 1, 2020, viongozi wa vyama hivyo walikutana nyumbani kwa Dkt Ruto mtaani Karen.

Watatu hao walikutana kabla ya Dkt Ruto kuelekea katika Ikulu kwa ajili ya sherehe ya Madaraka. Siku hiyo, Seneta Wetang’ula na Bw Mudavadi walienda kufanya kikao na wanahabari ambapo walimshutumu Bw Odinga kwa kupanga njama ya kujaribu kusambaratisha chama cha Ford Kenya ambacho sasa kinakumbwa na mvutano.

Dkt Ruto, Bw Wetang’ula na Bw Mudavadi wamekuwa wakiunda mpango wa kuanzisha kampeni ya kumaliza ushawishi wa Bw Odinga katika eneo la Magharibi kwa kumtaja kama msaliti na mlaghai wa kisiasa aliyetelekeza watu wa eneo hilo.

Viongozi hao walimshambulia Rais Kenyatta na Gavana Oparanya, Alhmaisi, siku moja baada ya Bw Odinga kukutana na viongozi wa Magharibi na Nyanza kujadili jinsi ya kuboresha sekta ya sukari ambayo imekuwa ikidorora kila uchao.

Viongozi waliokutana na Raila ni magavana Oparanya, Sospeter Ojaamong (Busia), Obado Okoth (Migori), Prof Anyang’ Nyong’o, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) Oburu Odinga na Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala.

Rais Kenyatta amekuwa akitumia Bw Odinga, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli, Gavana Oparanya na Waziri wa Ugatuzi, Bw Eugine Wamalwa kupenya katika eneo la Magharibi.

Katika mkutano wa viongozi wa Magharibi uliofanyika nyumbani kwa Bw Atwoli katika Kaunti ya Kajiado, Bw Oparanya na Wamalwa waliteuliwa kuwa wawakilishi wa jamii ya Waluhya watakaozungumza na serikali ili kupeleka miradi ya maendeleo katika eneo la Magharibi.

Duru zinasema kuwa Rais Kenyatta alimua kutenga Bw Mudavadi na Wetang’ula baada ya kukataa kushirikiana na serikali huku nchi ikijiandaa kwa kura ya maamuzi kurekebisha Katiba kwa kuzingatia mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kulingana na duru za kuaminika, Naibu wa Rais, Bw Mudavadi na Seneta Wetang’ula wanaelekea kuafikiana kubuni kamati ambayo itatafuta nani atakuwa mwaniaji-mwenza wa Dkt Ruto mwaka wa 2022.

Lakini wadadisi wanaonya kuwa iwapo Dkt Ruto atachukua mwaniaji-mwenza wa urais kutoka eneo la Magharibi huenda akapoteza kura katika eneo la Mlima Kenya.

“Wafuasi wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya huenda wakamkimbia ikiwa atachukua mwaniaji-mwenza kutoka eneo tofauti,” anasema wakili Felix Otieno.