JAMVI: Vizingiti vya Raila kugeuzwa kuwa mradi wa Uhuru

JAMVI: Vizingiti vya Raila kugeuzwa kuwa mradi wa Uhuru

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta ya kushirikisha kiongozi wa ODM Raila Odinga katika ziara zake za kuzindua na kukagua miradi inayofadhiliwa na serikali kuu maeneo mbalimbali nchini imesawiriwa kama hatua ya kupiga jeki azma ya mwanasiasa huyo mkongwe ya kumrithi.

Lakini wadadisi wanatilia shaka kufaulu kwa mkakati huu kutokana na pingamizi kutoka viongozi wa maeneo husika kando na kuendeleza dhana kwamba Odinga ni “mradi wa serikali”.

Kwa mfano, hivi majuzi, kiongozi wa taifa aliandamana na Bw Odinga katika ziara yake, ya siku moja, katika eneo la Ukambani, hatua ambayo iliwakera zaidi viongozi kutoka eneo hilo.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema hakuwa na habari kwamba Waziri huyu Mkuu wa zamani angeandamana na Rais Kenyatta katika ziara hiyo.

Kwa upande wao maseneta; Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na mwenzake Kitui Enock Wambua walimwonya Bw Odinga dhidi ya kutaka “kuvuna asichopanda.”

Vile vile, baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya wamepiga wazo la kumshirikisha Bw Odinga katika ziara ya Rais Kenyatta katika eneo hilo. Katika ziara hiyo ya siku tatu, Rais Kenyatta ameratibiwa kuzindua na kukagua miradi kadha ya maendeleo katika Kaunti za Kakamega, Trans Nzoia, Vihiga, Bungoma na Busia.

“Raila hafai kuandamana na Rais Kenyatta kwa sababu kiongozi wa taifa atakuwa akishughulikia masuala yanayowahusu watu wa eneo letu pekee. Akae kando kwa sababu mwezi jana, vigogo wetu kama Musalia Mudavadi na Moses Wetangula hawakumfuata Rais katika ziara yake ya Luo Nyanza,” akasema mbunge mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake.

Lakini Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alimlaumu Gavana wa eneo hilo Wycliffe Oparanya (Kakamega) kwa kuwatenga maseneta na wabunge katika maandalizi ya ziara hiyo “huku wakishirikisha wageni katika masuala yetu ya nyumbani,”

“Ziara ya Rais eneo la magharibi haifai kutumiwa kuendeleza masilahi ya kibinafsi ya mwanasiasa fulani kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Badala yake hii ni fursa yetu kama viongozi kuelezea rais matatizo yetu kama jamii,” akasema Bw Malala.

Akiongea alipozuru Kaunti ya Murang’a Jumanne, Odinga alithibitisha kuwa atazuru eneo hilo mara kadhaa akiandamana na Rais Kenyatta “kupalilia umoja kwa kitaifa kwa moyo wa handisheki tukielekea uchaguzi mkuu ujao.”

“Tumefika hapa na mnaona wazi kwamba Kenya yote imewakilishwa hapa. Mwamko mpya umeanza hapa nyumbani kwa S. K Macharia, mwanzo mpya wa kuunganisha Wakenya wote,” Odinga akasema.

“Kutoka hapa tutaelekea Magharibi mwa Kenya, kisha Nyanza ikifuatwa na Pwani na sehemu zote za nchini huku Uhuru akisimama upande mmoja nami nikisimamia upande mwingine,” akaongeza alipohudhuria hafla moja ya wanamuziki nyumbani kwa mmiliki wa shirika la habari la Royal Media Service, maeneo ya Ndakaini, eneobunge la Gatanga.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismus Mokua. itakuwa vigumu kwa Bw Odinga kukubalika katika ngome za wapinzani wake ambao vile vile wametangaza nia ya kuwania urais. Hii ni endapo Rais atafeli kushawishi waliokuwa washirika wa Odinga katika NASA, Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetangula kumuunga Raila mkono tena.

“Hii ni kwa sababu tayari tumeona kuwa muungano wa NASA umesambaratika baada ya vyama vya ANC na Wiper kutangaza kujiondoa. Isitoshe, mnamo Alhamisi ODM pia ilifuata mkondo huo na kutangaza kujiondoa. Kwa upande mwingine chama cha Jubilee kimesalia vigae baada ya Naibu Rais William Ruto na wandani wake kuhamia chama kipya cha UDA ambacho kinaibua msisimko mkubwa katika ulingo wa siasa,” anasema Bw Mokua.

“Vile vile, kuna hatari ya hatua ya Rais Kenyatta kuandamana na Raila katika ziara zake za kikazi nchini kumfanya kiongozi huyo wa ODM kuonekana kama mradi wa serikali katika kinyang’anyiro cha urais 2022. Hali hii itamwathiri pakubwa kisiasa ikizingatiwa kuwa Raila ni mwanasiasa mwenye historia ya kujisimamia kivyake,” anaongeza.

Naibu Rais Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa mambo yalianza kwenda mrama katika serikali ya Jubilee baada ya Bw Odinga “kuingia serikalini” kupitia handisheki mnamo Machi 9, 2018.

“Kwa hivyo, Raila na wenzake katika NASA waliojiunga na serikali na sisi wengine tukawekwa kando wanafaa kubebeshwa makosa yote ambayo yametokea katika serikali ikiwemo wizi wa pesa za kuwanunulia dawa wagonjwa wa corona,” akasema mwezi jana baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa moja mtaa wa Umoja, Nairobi.

Lakini Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa katika ODM Opiyo Wandayi amepuuzilia mbali madai kuwa ziara za pamoja kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga zinalenga kumfaidi kisiasa waziri huyo mkuu wa zamani kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Raila amesema kila mara kwamba hatategemea uungwaji mkono kutoka kwa Rais Kenyatta endapo ataamua kuwania urais. Lakini ninavyoelewa ni kwamba msururu wa ziara ya pamoja ya vigogo hao wawili unalenga kuleta umoja nchini chini ya mwavuli wa Handisheki baada ya migawanyiko iliyosababishwa na vuguvugu la hasla,” anasema mbunge huyo wa Ugunja.

Kauli hii inakinzana na yake Mbunge wa Lugari Ayub Savula ambaye anashikilia kuwa Rais Kenyatta anapania kutumia ziara hizo kama jukwaa la kupigia debe azma ya Odinga ya kuingia Ikulu 2022.

“Ningependa kumwonya Raila kwamba njama hii itafeli kabisa. Kwanza asahau kabisa kura za eneo la Mlima Kenya kufuatia kushindwa kwa Jubilee katika chaguzi ndogo kadha, mmoja wa hivi punde ukiwa uchaguzi mdogo wa Kiambaa. Mojawapo ya sababu ya kushindwa kwa Jubilee ilikuwa ni dhana kwamba kimeungana na ODM kwa ajili ya kufanikisha ndoto ya Raila za kuingia Ikulu 2022,” anaeleza.

You can share this post!

Shirika laangazia dhuluma, mahangaiko ya wasichana kipindi...

JAMVI: Joho atuliza boli uwanja wa siasa ukialika Nassir,...