MakalaSiasa

JAMVI: Vizingiti vya Ruto ndani ya Serikali

July 21st, 2019 4 min read

Na LEONARD ONYANGO

IDADI ya watu serikalini ambao Naibu wa Rais William Ruto anaona kuwa kizingiti kwake kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022 inazidi kuongezeka.

Kundi la Tangatanga ambalo linaunga mkono Dkt Ruto kwenye kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi ujao sasa limegeukia Msemaji wa Ikulu Kanze Dena-Mararo.

Kwa mara ya pili sasa Msemaji wa Rais amekuwa akitoa msimamo wa serikali unaoonekana kumkwaza Dkt Ruto.

Mapema mwezi huu, Dkt Ruto alimtaka Rais Kenyatta kuandaa mkutano wa Jubilee ili kutafutia ufumbuzi mgawanyiko ambao umejitokeza ndani ya chama hicho tawala.

Kulingana na Naibu wa Rais, vyama vya Upinzani vimeanza kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa 2022 ilhali chama cha Jubilee kikizidi kufifia kutokana na mgawanyiko.

Lakini Bi Dena alipokuwa akihutubia wanahabari mwanzoni mwa mwezi huu, alisema Rais Kenyatta anashughulikia miradi ya maendeleo na hana wakati wa kufanya siasa.

“Mkutano wa Jubilee ni suala la kisiasa. Rais hatajiingiza katika masuala ya kisiasa,” akasema Bi Dena.

Msemaji wa Ikulu pia amejipata pabaya baada ya kutetea Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju baada ya kusema kuwa ni mtumishi wa serikali ambaye amekuwa akimwakilisha Rais Kenyatta katika hafla mbalimbali.

Naibu wa Rais Dkt Ruto pamoja na wandani wake wanataka Bw Tuju kujiuzulu baada ya ripoti kudai kwamba amegeuka kuwa mshauri wa kisiasa wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wanasiasa wa Tangatanga wamemtaka Bi Dena kukoma kuingilia siasa ya chama cha Jubilee.

“Kanze Dena ameshindwa kutekeleza majukumu yake ndani ya Ikulu. Mtu amshauri aachane na masuala ya chama cha Jubilee hajui chochote,” akasema Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot.

Bw Tuju pia amegeuka kuwa hasimu wa kisiasa wa Naibu wa Rais. Mbali na kudaiwa kuwa mshauri kwa Bw Odinga, Bw Tuju pia anaonekana kushirikiana na wanasiasa wanaopanga njama ya kumzuia Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Hii ni baada ya kanda inayodaiwa kuwa mazungumzo baina ya Bw Tuju na mwanasiasa wa Kiambu George Nyanja wakipanga namna ya kumnyamazisha Dkt Ruto.

Bw Nyanja amewahi kunukuliwa katika vyombo vya habari akionya kundi la Tangatanga dhidi ya kwenda Kiambu.

Dkt Ruto amekuwa akimshutumu Bw Tuju kwa kusema kuwa analenga kuchochea migawanyiko ya kikabila nchini.

Kambi ya Naibu wa Rais pia inaona Katibu wa Wizara ya Masuala ya Ndani Karanja Kibicho kuwa mwiba kwa ndoto ya Dkt Ruto kuwania urais katika uchaguzi ujao.

Kundi la Tangatanga limekuwa likidai kuwa Dkt Kibicho amekuwa akifadhili vijana kuzomea viongozi wanaounga mkono Naibu wa Rais katika maeneo ya Mlima Kenya.

Tangatanga pia wanadai kwamba Dkt Kibicho ndiye alifadhili mikutano iliyohudhuriwa na mawaziri wanne kutoka eneo la Mlima Kenya kupanga njama ya kutaka kumdhuru Naibu wa rais.

Lakini Dkt Kibicho amejitokeza na kupuuzilia mbali madai hayo.

”Nasikia madai kuhusu mauaji…Nani amelalamika? Sijasikia malalamishi yoyote. Hayo ni madai yasiyokuwa na msingi,” akasema Dkt Kibicho.

Mbunge Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Kikuyu Kimani Ichung’wa ambao ni wandani wa Dkt Ruto, wiki iliyopita, walidai kuwa wanasiasa wa Tangatanga wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu serikalini katika kile walionekana kurejelea Dkt Kibicho.

“Tumekuwa tukipokea vitisho vya mara kwa mara kwa sababu tunaunga mkono mtu fulani kuwa rais 2022. Maafisa wa ukaguzi wa fedha za umma wamekuwa wakitumwa kila siku katika eneobunge langu kwa lengo la kutafuta makosa wanikamate. Hawa wakitoka, wengine wanatumwa lakini hawajapata ubadhirifu wa fedha,” akadai Bw Ndindi.

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) George Kinoti ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta anaonekana kuwa kizingiti kwa Naibu wa Rais Ruto.

Naibu wa Rais pamoja na wandani wake wamekuwa wakidai kuwa Bw Kinoti anatumiwa na baadhi ya wakuu serikalini kusambaratisha ndoto ya Dkt Ruto kuwania urais 2022.

Naibu wa Rais alikataa kuandikisha taarifa kwa Bw Kinoti licha ya kudai kuwa mawaziri wanne kutoka Mlima Kenya wanapanga njama ya kutaka kumuua.

Waziri wa Biashara Peter Munya amejitokeza kuwa miongoni mwa mahasimu wakuu wa Dkt Ruto.

Bw Munya ni miongoni mwa mawaziri wanne kutoka eneo la Mlima Kenya waliodaiwa kupanga njama ya kumuua Dkt Ruto.

Wikendi iliyopita, Bw Munya alimtaka Naibu wa Rais kukoma kufanya kampeni za mapema na badala yake aheshimu agizo lililotolewa na Rais Kenyatta la kuwataka wanasiasa kufanya miradi ya maendeo badala ya kuzungumza siasa kila uchao.

“Ikiwa unataka kuwania 2022, tumikia wananchi kwanza ndipo wanone kazi yako badala ya kuzunguka huku na huko,” akasema Bw Munya.

Rais Kenyatta ameonya wanasiasa dhidi ya kufanya siasa za mapema huku akitishia kuanzisha kampeni dhidi ya wanasiasa wa Tangatanga ili wakataliwe katika uchaguzi 2022 kwa kufanya kampeni za mapema.

“Ikiwa wewe ni mheshimiwa, nenda vijijini uwasaidie watu kupata umeme shuleni. Acha kurandaranda ukiambia watu namna unavyotaka kupata mamlaka. Hamtaenda popote,” akafoka Rais Kenyatta.

“Hawa wahalifu wanazunguka huku na huko wakipiga siasa wasifikiri kwamba mimi ni mtoto wao, watakiona,” akaongezea rais Kenyatta alipokuwa akizungumza kwa lugha ya Wakikuyu.

Wadadisi wa siasa pia wametofautiana kuhusu hatua anayofaa kuchukua Dkt Ruto ili kuhakikisha kuwa anaibuka mshindi katika uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Herman Manyora iwapo Ruto anataka kushinda urais hana budi kujiuzulu kutoka serikalini.

“Wakati wa Dkt Ruto kujiuzulu serikalini ni sasa kwa sababu akiendelea kuwa serikalini ataendelea kufinywa na hatapata fursa ya kuendesha kampeni zake,” anasema Bw Manyora.

“Kukamatwa kwa afisa wa mawasiliano wa Dkt Ruto, Dennis Itumbi ni ishara kwamba upande wa serikali uko tayari kufanya lolote kuzima naibu wa rais na hana budi kujiuzulu ili pate fursa ya kufanya kampeni,” anaongezea.

Lakini mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi Profesa Kisiang’ani anasema iwapo Dkt Ruto atapojiuzulu kutoka serikali atakuwa atakuwa amefanya kosa kubwa la kisiasa na ndoto yake ya kutaka kuwa rais 2022 itasambaratika.

“Naibu wa Rais amekuwa akihusishwa na madai mbalimbali yakiwemo ya ufisadi. Akijiondoa serikalini basi ataanza kuandamwa na mwishowe hatataweza kuwania,” anasema Prof Kisiang’ani.