MakalaSiasa

JAMVI: Wabunge wa Mlima Kenya wanavyohadaa watu kuhusu BBI

November 24th, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

MALALAMISHI ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya kwamba eneo hilo litapoteza katika ugavi wa mapato ya kitaifa na uwakilishi sawa endapo ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) litapendekeza mfumo wa utawala wa ubunge hayana mantiki, wadadisi wanasema.

Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa matokeo ya sensa iliyofanyika mnamo Agosti mwaka huu, kaunti za eneo hilo ndizo zilibainika kuwa na idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na zile za maeneo mengine nchini.

Kaunti hizo, bila shaka, zitapata mgao mkubwa wa fedha kutoka Hazina ya Kitaifa kwa sababu chini mfumo mpya wa ugavi rasilimali ulitangazwa mwaka huu na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), kaunti zilizo na idadi kubwa ya watu zitapata mgao mkubwa zikilinganishwa na zile zenye watu wachache.

Kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo Dkt Jane Kiringai, utaratibu wa ugavi wa Sh316 bilioni zilizotengewa serikali za kaunti katika mwaka huu wa kifedha wa 2019/2020 ni kwamba kigezo cha idadi ya watu kitachukua asilimia 45 ya fedha hizo.

Na ugavi sawa utachukua asilimia 26, kiwango cha umasikini (asilimia 18), ukubwa wa kieneo (asilimia 8) na usimamizi wa kifedha (asilimia 2).“Hii ina maana kwa kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya mwaka huu, kaunti zilizoorodheshwa kuwa na idadi ya kubwa ya watu zitapata mgao mkubwa wa fedha.

Nadhani hii ndio maana kabla ya zoezi hilo kuanza wanasiasa wetu, haswa magavana, walikuwa wakiwahimiza watu kutoka kaunti zao warejee nyumbani ili wahesabiwe huko,” akaambia safu hii kwenye mahojiano na safu.

Kwa hivyo, hii ina maana kuwa kando na Nairobi ambayo inaongoza kwa kuwa na watu 4.39 milioni, kaunti za Mlima Kenya kama vile Kiambu, Murang’a, Meru, Nyeri, Nyandarua na Kirinyaga pia ziliorodheshwa kuwa na watu wengine kulingana na matokeo ya sensa ya mwaka huu.

Kaunti ya Kiambu ina watu 2.4 milioni, Meru (1.5 milioni), Murang’a (1.06 milioni) Nyeri (759,164), Nyandarua (638,289) na Kirinyaga (610,411).Kwa hivyo, chini ya mfumo na vigezo vilivyotangazwa na tume ya CRA kaunti kama Kiambu itapokea Sh15 milioni kutoka hazina ya kitaifa, Murang’a (Sh8.8 milioni) na Meru (Sh9.01 milioni) katika mwaka huu wa matumizi ya fedha za serikali.Isitoshe, kwa mfano, kaunti za Kiambu na Meru ambazo zina maeneobunge 12 na tisa, mtawalia zitapokea kiwango kikubwa cha fedha za hazina ya maendeleo ya maeneobunge (CDF).

Hii ni kwa sababu katika mwaka huu wa kifedha (2019/2020) kila moja ya maeneobunge yote 290 litapokea Sh137 milioni.

Dkt Karingai anasema kuwa uchambuzi huu unaashiria kuwa hata kama ripoti ya BBI itapendekeza mfumo wa ubunge lakini idadi ya kaunti na maeneo bunge isalie ilivyo sasa, bado eneo la Mlima Kenya litapata mgao mkubwa wa rislimali za umma katika kwa Hazina ya Kitaifa.

Wabunge hao, zaidi ya 40, sasa wametisha kukataa ripoti hiyo ambayo itapokezwa Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumanne, endapo mfumo huo ambapo rais atachaguliwa na wabunge.

Wanadai kuwa jamii za Mlima Kenya hawajapewa uwakilishi sawa kulingana na idadi yao na idadi yao na idadi ya wapigakura kutoka eneo hilo.

“Tukiongea kuhusu kuhusishwa kwa eneo hili katika uongozi, sharti hali ya hitaji hilo lifikiwe bungeni na katika asasi nyinginezo. Sharti tuwe na idadi sahihi ya maeneobunge ili watu wetu wapate uwakilishi bora na ugavi sawa wa rasilimali za kitaifa,” anasema mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni.

Huku akifafanua kuwa kauli yake inawakilisha ya wenzake kutoka eneo hilo la Mlima Kenya, Bw Kioni anasema watapinga mfumo kwa ubunge kwani utapendekeza kuwa rais achaguliwe na wabunge.

“Kwa sababu, maeneobunge yetu ni machache ikilinganishwa na idadi ya watu wetu, ikiwa wabunge ndio watachagua rais, eneo letu litakuwa na usemi finyu ikilinganishwa na maeneo mengine yenye watu wachache. Tunataka mfumo wa mtu mmoja, kura mmoja,” anasema Mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Utekelezaji wa Katiba (CIOC).

Eneobunge la Tiaty Naye mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua anasema haiwezekani kwamba eneobunge lake ambalo lina wapigakura 130,000 linawakilishwa na mtu mmoja bunge sawa na eneobunge la Tiaty lenye wapigakura 9,000 pekee.

Lakini kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale anapuuzilia kauli ya wabunge hawa akisema katiba ya Kenya inatambua Kenya kwa misingi ya eneo na idadi ya watu.

“Ikiwa wanashikilia kauli mbiu ya mtu mmoja kura moja, sisi kutoka kaskazini mwa Kenya pia tutataka mpango wa kura moja kwa umbali wa kilomita moja kwa sababu maeneo yetu ni pana,” anasema mbunge huyo wa Garissa Mjini.

Kulingana na Duale mfumo wa utawala wa ubunge utatoa suluhu kwa kile anachokitaja kama udikteta wa makabila makubwa matano nchini.

“Mfumo wa ubunge utasambaza mamlaka na kutoa nafasi kwa mtu kutoka jamii ya wafugaji kupata vyeo vya juu uongozi. Huu udikteta wa makabila matano makubwa utakoma,” anasema.

Naye mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora anawakosoa wabunge wa Mlima Kenya kwa kulalamika ilhali eneo hilo ndilo “limepata maendeleo makubwa tangu uhuru kwa sababu ya kutoa marais watatu.

“Huu mfumo wa utawala wa urais wanaoupinga utawafaidi wao wenyewe kwa sababu rais atachaguliwa na wajumbe ambao watateuliwa kulingana na idadi ya watu katika maeneo mbalimbali. Maeneo yenye watu wengi yapata idadi kubwa ya wajumbe jinsi hali ilivyo nchini Amerika,” anasema mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi.