JAMVI: Wandani wauma Raila kichwa huku 2022 ikibisha hodi

JAMVI: Wandani wauma Raila kichwa huku 2022 ikibisha hodi

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anakabiliwa na kizungumkuti kikubwa kuamua wagombeaji atakaowaunga mkono katika viti mbalimbali 2022 hususan katika ngome yake ya Nyanza.

Hii ni baada ya kubainika kwamba wandani wake wa karibu katika eneo hilo wanamezea mate viti vya ugavana katika kaunti nne za Homa Bay, Migori, Siaya na Kisumu kwa tiketi ya chama hicho cha chungwa.

Kwa mfano, katika kaunti ya Homa Bay, kiti cha ugavana kimevutia mwenyekiti wa ODM John Mbadi (Mbunge wa Suba Kusini), Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Gladys Wanga (mwenyekiti wa ODM Homa Bay) na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero.

Katika kaunti ya Migori wandani wa Bw Odinga wanaomezea mate kiti cha ugavana ni Seneta wa kaunti hiyo Ochilo Ayacko na mbunge wa Suna Mashariki ambaye pia ni mkurugenzi wa uchaguzi katika chama cha ODM, Junet Mohamed.

Huku Profesa Anyang’ Nyong’o akipania kutetea kiti chake Kisumu, anakoseshwa usingizi na seneta wa kaunti hiyo Fred Outa ambaye pia ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga.

Katika kaunti ya Siaya anakotoka Waziri huyo Mkuu wa zamani, amejipata katika njia panda aunge nani kati ya Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Seneti Seneta James Orengo na mkurugenzi wa masuala ya siasa katika ODM, Mbunge wa Ugunja James Opiyo Wandayi.

Ni kutokana na hali ambapo wadadisi sasa wanaonya kwamba hali hii huenda ikavuruga uthabiti wa ODM katika ngome hiyo hasa ikizingatiwa kuwa tayari inakabiliwa na ushindani kutoka kwa chama cha People Democratic Party (PDP), chake Gavana wa Migori Okoth Obado.

Mbali na PDP, chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto pia kimeanza kupenya Luo Nyanza kupitia juhudi za mwanasiasa Eliud Owalo. Hii ni kando na vyama vinginevyo ikiwemo Ford Kenya ambacho kilitwaa ubunge wa Kisumu Mjini Magharibi 2017 kupitia Bw Olago Aluoch.

“Kwa misingi hii, wagombeaji ambao watahisi kuwa hawatapata haki wakati wa mchujo wa ODM bila shaka watagura na kusaka tiketi za vyama vingine au waamue kuwania kama wagombea huru,” anasema Dkt Tom Mboya.

Kwa mujibu wa mchanganuzi huyu wa masuala ya siasa za Nyanza, Bw Odinga anakabiliwa na kibarua kikuu kuhakikishia wagombeaji kuwa haki itatendeka wakati wa mchujo wa chama hicho.

Ugavana

“Hata hivyo, kibarua kikubwa kitakuwa katika kiti cha ugavana hasa ikizingatiwa kwamba tayari wandani wake wameanza kavutana inavyodhihirika katika kaunti ya Siaya baina ya Orengo na Wandayi huku ugavana wa Homa Bay uking’ang’aniwa na Mbadi, Wanga, Kidero miongoni mwa wengine,” anaeleza Dkt Mboya ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maseno.

Itakumbukwa kwamba katika chaguzi kuu za miaka ya 2013 na 2017, baadhi ya wanasiasa waligura ODM na kujiunga na vyama vingine baada ya kutendewa hiana katika kura za mchujo. Wengine waliamua kuwania nyadhifa mbalimbali kama wagombeaji huru.

Kwa mfano, mnamo 2013 Obado aligura ODM na kuwania ugavana kwa tiketi ya PDP baada ya kunyimwa tiketi ilhali alimwangusha Profesa Edward Oyugi katika mchujo wa ODM. Baadaye Bw Obado alimbwaga Profesa Oyugi katika uchaguzi mkuu na kuwa gavana wa kwanza wa Migori.

Wanasiasa wengine kama vile Bw Olago, Onyango K’Oyoo na James Opiyo walifaulu kushinda viti vya ubunge vya Kisumu Mjini Magharibi, Muhoroni na Awendo, mtawalia kwa tiketi za vyama vya Ford Kenya na PDP baada ya kupokonywa ushindi katika mchujo wa ODM.

Wilson Agenya ambaye ni mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi anasema itakuwa muhimu zaidi kwa Bw Odinga kuhakikisha kuwa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) haiingiliwi itakapokuwa ikiendesha kura za mchujo haswa za viti vya ugavana.

“Wananchi wapewe nafasi ya kuteua wagombeaji bora watakaoisaidia ODM kuvuna ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2022. Wagombeaji nao wasitumie ukaribu wao na Odinga kuwahadaa wapiga kura ili wawateue,” akasema Profesa Agenya.

Hata hivyo, msomi huyo anabashiri kuwa kivumbi kitashuhudiwa katika mchujo wa ugavana ambapo wagombeaji wanatarajiwa kutumia mbinu zote, ikiwemo kutumia fedha kupata tiketi ya ODM.

Kwa mfano, katika kaunti ya Homa Bay inaaminika kuwa Dkt Kidero atatumia utajiri wake kuboresha nafasi yake ya kupata tiketi ya ugavana huku Bi Wanga akitarajiwa kutumia cheo chake cha mwenyekiti wa ODM katika kaunti hiyo na uungwaji kutoka kwa wanawake kufanikisha ndoto zake.

Vile vile, kuna minong’ono kwamba Bw Mbadi atategemea wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM kupata tiketi ya chama hicho kuwania ugavana wa Homa Bay.

“Hii ndio maana, Bw Odinga akiwa kiongozi wa ODM ana kazi kubwa kuhakikisha kuwa bodi ya NEB inaendesha majukumu yake kwa njia huru na haki bila kuingiliwa kwa njia yoyote. Watakaoshindwa wakubali matokeo na kuunga mkono washindi ili kudumisha umoja ndani ya chama hicho,” akasema msomi huyo.

You can share this post!

Watoto 3 milioni katika kaunti 13 kupokea chanjo ya polio

MALENGA WA WIKI: Mwangi Wanjiru ni miongoni mwa vijana...