MakalaSiasa

JAMVI: Wito wa Atwoli watikisa msingi wa chama cha Jubilee

May 6th, 2018 3 min read

Na BENSON MATHEKA

WITO wa kutaka mabadiliko ya katiba ili Rais Uhuru Kenyatta aendelee kuhudumu serikalini baada ya kumaliza kipindi chake cha pili 2022, ni pigo kwa ustawi wa demokrasia nchini na linaweza kusambaratisha chama cha Jubilee.

Na ingawa baadhi ya washirika wa rais wanapinga pendekezo lililotolewa na katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Cotu Francis Atwoli, kwamba katiba ibadilishwe kubuni wadhifa wa waziri mkuu kumwezesha Rais Kenyatta kuendelea kushiriki siasa baada ya 2022, wadadisi wanasema hatua kama hiyo itavunja chama cha Jubilee.

“Pendekezo la Atwoli sio hewa tupu. Katika siasa mambo hubadilika haraka sana. Usisahau washirika wa rais, hasa kutoka ngome yake wanahisi hawana mtu wa kumrithi na wangetaka aendelee kuwa serikalini kwa sababu wanahisi anawakilisha maslahi yao. Siasa za Kenya ni telezi sana,” asema Bw Alloys Mwangi, mdadisi wa masuala ya siasa.

Kulingana naye, mjadala kuhusu kubadilisha katiba kuhakikisha Rais Kenyatta ataendelea kuhudumu baada ya 2022 umekuwepo kwa muda, japo chini kwa chinichini.

“Nahisi kuna mikakati ambayo imekuwa ikiendelea chini kwa chini katika mrengo mmoja wa Jubilee. Hofu ya wakereketwa wa mabadiliko hayo ni azma ya Naibu Rais William Ruto ya kugombea urais 2022.

Rais mwenyewe pia aliahidi kustaafu baada ya kumaliza kipindi chake cha pili na kumuunga Bw Ruto. Hata hivyo, inaonekana kuna shinikizo mpya zilizojiri na muafaka wa Rais Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga,” alisema Bw Mwangi.

 

Uhuru awe Waziri Mkuu 2022

Akiongea kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni katika bustani ya Uhuru Park Jumanne, Bw Atwoli alipendekeza katiba ifanyiwe mageuzi ili kubuni wadhifa wa waziri mkuu utakaoshikiliwa na Rais Kenyatta baada ya 2022.

Kulingana na Bw Atwoli, Rais Kenyatta atakuwa bado na nguvu atakapomaliza kipindi chake cha pili 2022 na anafaa kuendelea kushiriki siasa.

“Tubadilisheni katiba hii na kutumia rasimu ya Bomas ili kuhusisha watu wote kwa sababu sio kila mtu anaweza kuwa rais. Kufanya hivi kutamshirikisha Rais Kenyatta ambaye angali bado chipukizi. Tusipofanya hivyo, tutampeleka wapi?” alihoji Bw Atwoli.

“Nawaambia kwamba hata mtu mwingine akiongoza Kenya, ni lazima atashirikiana na watu wa Mlima Kenya na huo ndio ukweli wa mambo,” alisema Bw Atwoli.

Kulingana na rasimu ya katiba ya Bomas, Kenya ingekuwa na wadhifa wa waziri mkuu ambaye angechaguliwa na bunge na kuwa na na mamlaka makuu.

Wadadisi wanasema pendekezo hilo ni njama ya kuzima azima ya Naibu Rais William Ruto ambaye  amepinga mabadiliko yoyote ya katiba yanayolenga kubuni nyadhifa mpya serikalini. Wanasema si ajabu mabadiliko hayo yalikuwa miongoni mwa masuala ambayo Rais Kenyatta na Bw Odinga walikubaliana katika muafaka wao.

Mchanganuzi Barack Muluka anahisi suala la kuhakikisha Rais Kenyatta ataendelea kuhudumu kama waziri mkuu lilijadiliwa kwenye mikutano iliyotangulia muafaka wake na Bw Odinga.

 

Raila na Uhuru wana maoni sawa

“Odinga anaamini kwamba atakuwa rais pengine akiwa na naibu kutoka  Rift Valley na mwingine kutoka Pwani. Kenyatta anaweza kuwa waziri mkuu akiwa na manaibu wawili kutoka Magharibi na Mashariki. Hawa wawili wana maoni sawa,” Bw Muluka alisema.

Kwenye makala yaliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini kabla ya tamko la Bw Atwoli, Bw Muluka  alisema viongozi hao wawili watawaagiza wabunge na madiwani wa vyama vyao kuunga mabadiliko ya katiba wakisingizia wanalenga kuunganisha nchi.

“Kuna wale watakaopinga mabadiliko hayo na kwa hivyo kutazuka makabiliano ya kisiasa na kikatiba nchini Kenya,” alitabiri Bw Muluka.

Kulingana na kiongozi wa wengi katika seneti Bw Kipchumba Murkomen, ambaye ni mshirika wa Bw Ruto, katiba haiwezi kubadilishwa ili kubuni nyadhifa kwa sababu ya watu binafsi.

“Rais ameshughulikiwa ipasavyo katika katiba na hahitaji kutengewa wadhifa,” alisema Bw Murkomen na kuungwa mkono na mwenzake katika bunge la taifa, Aden Duale ambaye pia ni mwandani wa Bw Ruto.

“Rais Kenyatta ametangaza wazi kwamba, atafurahi kustaafu siasa baada ya kumaliza kipindi chake cha pili,” alisema Duale.

Wadadisi wanasema njama zozote za kumzuia Bw Ruto kugombea urais 2022 zinaweza kuvunja chama cha Jubilee.

“Bw Ruto atahisi kuwa amesalitiwa baada ya kumuunga Rais Kenyatta tangu 2013. Amekuwa akilenga urais 2022 na yeye na washirika wake hawatachukulia hatua yoyote ya kuzima ndoto yake kwa urahisi,” asema Bw Doris Chebet wakili na mdadisi wa siasa.

Anasema pendekezo la kumtaka Rais Kenyatta kuendelea kuhudumu ni njama za watu binafsi wanaomzunguka na ambao wanataka kuendelea kufurahia mamlaka.

 

Kuongezwa kwa muhula

“Usishangae kusikia baadhi yao wakipendekeza muda wa kipindi cha rais kuhudumu uongezwe kutoka miaka mitano hadi saba,” alisema Bi Chebet.

Bw Atwoli alisema kwa sababu Rais Kenyatta atakuwa na umri wa miaka 60 atakapomaliza kipindi chake cha pili, ngome yake ya kisiasa haitakubali astaafu.

Wanaopinga pendekezo hilo wanamhimiza Rais Kenyatta kuiga viongozi wanaoheshimiwa kote ulimwenguni kwa kukataa kukwamilia mamlakani.

Bw Mwangi anasema Bw Atwoli hakuwa wa kwanza kutoa pendekezo kama hilo.

“Nakumbuka mapema mwaka huu, David Murathe, ambaye ni afisa mkuu wa chama cha Jubilee (naibu mwenyekiti) alinukuliwa akisema kuna watu wanaotaka Uhuru astaafu akitimiza miaka 60 ilhali Raila anataka kuwa rais akiwa na miaka 75.

Hii inaonyesha huenda kuna njama pana zinazopikwa kuhakikisha Uhuru anasalia serikalini baada ya 2022” alisema Bw Mwangi na kuongeza kuwa washirika wa Bw Ruto wanaweza kuondoka Jubilee iwapo hilo litatendeka.

Kulingana na  Bi Chebet, mswada wa mbunge wa Tiaty, Kassait Kamket unaopendekeza katiba ibadilishwe Rais ahudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba na kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka makuu, haufai kupuuzwa.

“Marais wengi wametumia mabadiliko ya katiba ili waendelee kuhudumu, hasa wakiwa na idadi kubwa ya wabunge. Jubilee ina wengi katika bunge na seneti na hata wanaomuunga Ruto wakikosa kuunga mabadiliko, wale wa ODM wanaweza kuyaunga kufuatia muafaka wa Uhuru na Odinga,” alisema.