JAMVI: Yaelekea huu ndio mwanzo mpya EAC

JAMVI: Yaelekea huu ndio mwanzo mpya EAC

Na WANDERI KAMAU

MSISIMKO mpya wa urafiki kati ya Kenya na Tanzania umeibua maswali kuhusu ikiwa mataifa hayo yamefungua ukurasa mwingine kwenye mahusiano yake ambayo yalikuwa yamedorora.

Hilo pia limezua maswali ikiwa hatimaye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeanza safari mpya kwenye mahusiano na mwingiliano wao.

Hilo linafuatia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania nchini Jumanne na Jumatano wiki hii, ambapo uwepo wake ulizua msisimko wa aina yake nchini.

Kwenye ziara hiyo, Rais Suluhu na mwenyeji wake, Uhuru Kenyatta, walitia saini mkataba wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mombasa hadi Dar es Salaam, utakaogharimu Sh63 bilioni.

Viongozi hao vile vile waliziagiza wizara za Mashauri ya Kigeni na zile za Biashara na Viwanda katika mataifa hayo kuanza mchakato wa kutatua vikwazo vya kibiashara ambavyo vimekuwepo katika maeneo ya mipakani.

Upeo wa ziara ya Rais Suluhu ulikuwa ni kulihutubia Bunge la Kitaifa na Seneti, ambapo alisisitiza kuhusu haja ya nchi hizo kusahau “yaliyopita na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika masuala muhimu kama biashara.”

Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa, ingawa lengo kuu la Bi Suluhu lilikuwa kuondoa uhasama uliokuwepo kati ya nchi hizo wakati wa utawala wa mtangulizi wake, Dkt John Magufuli, huenda hilo likaashiria mwanzo mpya kwa jumuiya hiyo.

Wachanganuzi wa mahusiano ya kimataifa wanaitaja Tanzania kuwa kikwazo kikuu kwa ukuaji wa jumuiya hiyo tangu miaka ya sitini, kutokana na mitazamo yake hasi, hasa kuhusu Kenya.

Hivyo, wanataja mwelekeo huo kuwa muhimu kwa mustakabali wa jumuiya hiyo.

“Tanzania ndio imekuwa kikwazo kikuu kwa juhudi, mipango na mikakati yote ya kuunganisha wanachama wa EAC kutokana na misimamo yake ya kisiasa. Ikiwa hilo litabadilika, basi huenda mipango ambayo imekuwepo, kama vile kubuniwa kwa sarafu moja miongoni mwa wanachama ikafaulu,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa.

EAC iliasisiwa mnamo 1967 kati ya Kenya, Uganda na Tanzania, ikilenga kuzisaidia nchi hizo kuunganisha na kuwianisha masuala muhimu kama vile afya, biashara na miundomsingi.

Viongozi waliokuwepo wakati wa kuanzishwa kwake ni hayati Mzee Jomo Kenyatta (Kenya), Julius Nyerere (Tanzania) na Milton Obote (Uganda).

Sambaratika 1977

Licha ya kuwa na malengo makubwa, muungano ulisambaratika mnamo 1977, kutokana na ushindani miongoni mwa wanachama kudhibiti baadhi ya sekta muhimu.

Hilo pia linatajwa kuchangiwa na hatua ya Kenya kuomba nyadhifa nyingi katika taasisi kuu za kufanya maamuzi kuhusu mwelekeo wa jumuiya hiyo, hali ya kutoelewana miongoni mwa wanachama na tofauti kwenye mifumo ya utawala katika nchi hizo, hasa Kenya na Tanzania.

Hata hivyo, jumuiya hiyo ilifufuliwa upya mwaka 2000. Hilo lilifuatia mkataba uliotiwa saini miongoni mwa nchi hizo tatu jijini Arusha mnamo Novemba 1999, kuhusu haja ya kuufufua upya.

Kulingana na Dkt Sang’, sababu kuu ya kuvurugika kwa jumuiya hiyo kati ya 1977 na 2000 ilitokana na hatua ya viongozi waliokuwepo kukosa kuanza mazungumzo kutathmini haja ya ufufuzi wake.

“Marais Daniel Moi (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda), Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa (Tanzania) walikosa kubuni utaratibu maalum ambao ungerejesha upya ushirikiano kati yao. Walingoja hadi mwaka 2000 kurejesha mahusiano hayo. Hilo lilikuwa kosa kubwa,” asema.

Dkt Geoffrey Musila, aliye mdadisi mahusiano ya kimataifa, anailaumu Tanzania kuwa sababu kuu ya kuvurugika kwa “awamu ya kwanza ya EAC.”

“Kutokana na mfumo wa kisiasa wa Ujamaa, ambao ulisisitiza kuhusu haja ya raslimali za nchi kumilikiwa na wananchi wenyewe, viongozi na raia wa Tanzania waliwaona wenzao walioegemea mfumo wa kibepari kama Kenya na Uganda kama ‘maadui’ na ‘wabinafsi.’ Hilo ndilo lililoifanya nchi hiyo kutilia maanani uanachama wake katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),”akasema Dkt Musila.

Msimamo wa Magufuli

Wachanganuzi wanasema kuwa hata baada ya jumuiya kufufuliwa upya, Tanzania ndio ilichangia tofauti zilizoibuka, hasa wakati wa utawala wa Rais Magufuli.

“Kutokana na msimamo wake mkali, Rais Magufuli alivuruga tena uthabiti ambao ulikuwepo baada ya jumuiya hiyo kufufuliwa tena. Utawala wake uliathiri vikali ujirani mwema ambao ulikuwepo awali kati ya Tanzania na majirani wake. Kwa namna moja, hilo liliathiri sana mafanikio ambayo yalikuwa yamefikiwa katika ukuaji wa jumuiya hiyo,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni msomi wa historia.

Hivyo, anasema kuwa mwelekeo mpya ambao Rais Suluhu ameonyesha ni “suluhisho” la “kosa” ambalo alifanya Magufuli, kwani lilivuruga sana ukuaji wa jumuiya hiyo.

“Ikiwa Rais Suluhu ataepuka makosa ambayo yalifanywa na watangulizi wake, basi kuna uwezekano mkubwa kwa jumuiya hii kuwa na mwanzo mpya. Ni mwanzo ambao utaiwezesha kutimiza baadhi ya malengo yaliyokuwepo awali,” akasema Prof Munene.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa bado ni mapema kuanza “kusherehekea”mwelekeo wa jumuiya hiyo, ijapokuwa Bi Suluhu ameonyesha dalili za kuridhisha.

You can share this post!

Polo atorokwa na demu juu ya msoto

Kimya cha Kiunjuri kuhusu 2022 chazua gumzo