MakalaSiasa

JAMVI: Ziara za Ruto zageuka siasa za 2022 licha ya kusisitiza huu si wakati wa kampeni

June 13th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Ziara za Naibu Rais William Ruto maeneo mbalimbali nchini kuzindua au kukagua miradi ya maendeleo zimegeuka kuwa kampeni za uchaguzi wa urais 2022 licha ya yeye binafsi kuwasuta wanaopiga siasa badala ya kuhudumia Wakenya.

Kila eneo ambalo Bw Ruto amekuwa akitembelea, siasa zimekuwa zikipewa nafasi ya kwanza na hata kufanya baadhi ya wanasiasa kugombana vikali kuhusu siasa za 2022.

Katika eneo la Pwani, ambako amekuwa akizuru mara kwa mara mwaka huu, siasa za 2022 zimechacha huku mpasuko kati ya gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi ukipanuka.

Japo wote ni wa chama cha ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, magavana hao waliokuwa wandani na wakosoaji sugu wa Bw Ruto mwaka jana wamemchangamkia ingawa wamekuwa wakitofautiana kuhusu iwapo watamuunga mkono 2022.

Japo Bw Ruto amekuwa akikosoa viongozi wa upinzani wanapozungumzia siasa za 2022 akisema Jubilee haina wakati wa siasa mbali inazingatia maendeleo, mwenyewe ameonekana kukomesha wanasiasa anaofuatana nao katika mikutano yake.

Duru zinasema Bw Ruto ameweka mikakati kabambe kujenga umaarufu wake kuelekea uchaguzi wa 2022 na nafasi inapomjia amekuwa akiikumbatia kikamilifu kinyume na matamshi yake kwamba uchaguzi ulipita na ni wakati wa kuhudumia wapiga kura.

Kiranja wa wachache katika Bunge la Taifa, Junet Mohammed ameeleza kushangazwa na Bw Ruto akisema ziara zake ni sawa na za kipindi cha kampeni za uchaguzi wa 2022.

“Ninaungana na Wakenya wengi kushangaa. Ni kama kipindi rasmi cha kampeni za uchaguzi wa urais 2022 kimetangazwa na IEBC. Hii ni hesabu mbaya,” Bw Junet aliandika kwenye Twitter.

Mikakati ya Bw Ruto imekuwa ni kupokea jumbe za viongozi kutoka maeneo tofauti mtaani Karen, Nairobi kujadili anachokitaja kama maendeleo. Mikutano hiyo imekuwa ikifuatiwa na ziara katika maeneo husika ambapo siasa zimekuwa mada kuu.

Tangu wiki jana, Bw Ruto alizuru pwani mara tatu “kukagua” miradi ya maendeleo ambapo siasa zilitawala. “Bw Ruto anajua kupanga mikakati yake ya kisiasa na moja ya mbinu hizo ni kuwasha moto katika ngome za upinzani na kugawanya wafuasi sugu kwa manufaa yake.

Amefaulu eneo la pwani ambako amekuwa akizuru mara kwa mara na unaweza kutarajia ziara kama hizi kuendelea maeneo mengine nchini siku zijazo,” alisema mshirika mmoja wa Bw Ruto ambaye hakutaka tutaje jina lake.

Bw Ruto amekuwa akisisitiza kuwa ziara zake mashinani sio za kumangamanga akifanya siasa, mbali ni za kuendeleza ajenda za serikali ya Jubilee. Kila eneo, amekuwa akizindua miradi na kuahidi mingi ya mamilioni ya pesa bila kubagua ngome za upinzani au za Jubilee. Kwa kufanya hivi, wadadisi wanasema, Bw Ruto amekuwa akijijenga kisiasa.

Akiwa pwani wabunge wengi waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM walitangaza kuwa watakuwa nyuma yake 2022, jambo lililozua mzozo baina yao na ofisi kuu ya chama hicho.

Alipozuru maeneo ya Nyeri, Kirinyaga, Murang’a na Kiambu, wanasiasa walichukua fursa hiyo kumhakikishia watamuunga mkono kuwania urais huku wachache tu wakikataa kutangaza msimamo.