Makala

JANE NYAMBURA: Mhariri mahiri wa filamu

May 21st, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

KILA Mja hujipa matumaini mema kwa anachofanya ambapo huwa ni hali ya kutarajia. Ni katika kutumainia na kuvumilia ambapo anaamini nyota yake itang’aa na kuibuka kati ya waigizaji watajika duniani.

Anasema anaendelea kukuza kipawa chake katika tasnia ya uigizaji maana ndiyo iliyokuwa ndoto yake tangu akiwa mdogo.

Japo hajapata mashiko, Jane Waria Nyambura analenga kufikia hadhi ya kimataifa kama mwenzake mzawa wa Kenya, Lupita Nyong’o anayendelea kutesa katika filamu za Hollywood.

Binti huyu ni mwigizaji chipukizi, mhariri wa filamu, video vixen bila kuweka katika kaburi la sahau mwanamitindo.

Bila shaka kisura huyu anaorodheshwa kati ya waigizaji wanaolenga kufanya makubwa katika ulingo wa filamu miaka ijayo.

”Nafanya na kundi la Do Art Centre ninalodhamiria kutumia kufikia upeo wa juu katika masuala ya uigizaji,” alisema na kuongeza kuwa kupitia kundi hilo wamefaulu kuzalisha filamu fupi nyingi tu. Mrembo huyu amesomea masuala ya uigizaji katika Taasisi ya Shang Tao School of Arts alikojifunza mengi kuhusu kazi ya kuediti filamu.

”Kusema kweli napenda sana kuediti filamu ndiyo maana zimezamia kupiga shughuli hizo katika kundi la Do Art Centre ambapo hushirikiana na wasanii wengine kadhaa,” alisema.

Kama video vixen mwigizaji huyu mwenye umri wa miaka 21 anasema mapema mwaka huu alibahatika kuhusika katika nyimbo za msanii wa kizazi kipya iitwayo ‘faded’ utunzi wake mwimbaji chipukizi anayefahamika kama Flexx.

Mwigizaji chipukizi, Jane Waira Nyambura anayelenga kuibuka kati ya mastaa mahiri duniani katika uigizaji. Picha/ John Kimwere

Anajivunia kushiriki filamu mbili na kuediti moja zilizorushwa kupitia runinga ya Mt Kenya TV. Pia ameshiriki kipindi cha Perfect Match ambacho hurushwa kupitia Ebru TV. Katika kundi la Do Art Centre kando na masuala ya kuhariri filamu amewahi kushiriki filamu fupi kwa jina ‘Bachellors Life.’

Katika mpango mzima chipukizi huyu anasema anapenda kutazama filamu za Kinigeria (Nollywood) za waigizaji kama Genevieve Nnaji ambaye ameshiriki filamu nyingi tu ikiwamo ‘Blood sister,’ ‘Sisters with one heart,’ ‘Half of a yellow sun,’ na ‘Lionheart,’ kati ya zingine. Vile vile anadokeza kuwa hupangawishwa na usanii wake Mercy Johnson anayejivunia kushiriki filamu tele pia kutwaa tuzo tofauti.

”Ninaamini wakenya tunaouweza wa kufanya filamu nzuri kuliko wenzetu wa Nollywood ila ndiyo waliotangulia na wamepiga hatua kutuliko ndiyo maana tunapenda kutazama kazi zao,” alisema na kuongeza kuwa Wakenya wamo mbioni kupaisha sekta ya uigizaji.

Anakiri kwamba hukosefu wa soko ndio hutatiza sekta ya uigizaji hapa nchini. Kipusa huyu anashauri wenzake kutia bidii na kutovunjika moyo kwenye juhudi za kusaka ajira ya uigizaji mbali wamwaminie Mungu nyakati zote ambapo wakati utakapofika wa milango kufunguliwa hamna atakayezuia.