Habari za Kitaifa

Janga jipya la mafuriko

April 15th, 2024 1 min read

WINNIE ATIENO NA JURGEN NAMBEKA

GAVANA wa Tana River Dhado Godhana, ameonya kuwa kaunti yake inakodolea janga lingine la mafuriko kufuatia mvua inayoendelea kunyesha maeneo kadhaa nchini.

Gavana huyo amewasihi wahisani na wadau kujitokeza kusaidia kaunti yake ambayo inaendelea kuathirika na mafuriko.

Tayari watu wawili wameaga dunia eneo hilo baada ya kusombwa na mafuriko huku serikali ya Kaunti na Serikali Kuu ikihimiza wakazi wa nyanda za chini kuhamia zile za juu.

Bw Godhana alitoa wito huo, huku Serikali ikisema kuwa imeweka mikakati kabambe kukabiliana na janga la mafuriko katika sehemu nyingi za humu nchini na haswa Pwani.

Akizungumza jijini Mombasa msemaji wa Serikali, Bw Isaac Mwaura alieleza kuwa Serikali imetenga fedha kusaidia Wakenya ambao wataathirika na mvua, ambazo kulingana naye zingeathiri sana sehemu ya Pwani ambako maji ya mito mingi huishia.

“Tulipokuwa na mvua za El Nino iliathiri masuala mengi nchini ikiwemo kilimo, kuharibu makazi na hata kusababisha magonjwa. Mvua hizi za Machi hadi Mei zimeanza kwa fujo na kupita viwango vya kawaida. Serikali inafuatilia changamoto ambazo itashughulikia. Serikali inapanga nyumba za kuhakikisha kuwa wale ambao makazi yao yataharibika wamepata sehemu ya kujisitiri,” akasema bw Mwaura.