Kimataifa

Janga la moto ladhibitiwa Australia

February 13th, 2020 1 min read

Na AFP

SYDNEY, Australia

MIKASA ya moto katika jimbo la New South Wales nchini Australia imedhibitiwa, maafisa wa kupambana na moto walisema Alhamisi kuashiria mwisho wa janga hilo ambalo limesababisha vifo vya watu 33 nchini humo.

“Kufikia leo (Alhamisi) adhuhuri visa vyote vya moto kuteketeza mali vimedhibitiwa,” msemaji wa Shirika la Rural Fire Service aliambia AFP.

Hii ni baada ya mvua kubwa iliyoanza kunyesha nchini humo majuzi kusaidia kuzima mioto ambayo imekuwa ikiteketeza maeneo ya mashariki mwa Australia tangu Septemba mwaka jana.

“Ni habari njema,” msemaji huyo ambaye hakutambuliwa kwa jina akaongeza.

Tangu Septemba 2019 eneo la ukubwa wa hekta milioni 10 limeteketezwa na moto katika maeneo ya Mashariki na Kusini mwa Australia na kuangamiza watu 33 na mifugo mingi.

Vilevile, zaidi ya nyumba 2, 500 imeharibiwa katika mioto hiyo.

Moshi mkubwa ulifunika anga ya miji mikuu kama vile Sydney kwa wiki kadhaa na kutatiza shughuli za kawaida katika miji mingine.

Moto huo ulichochewa na kiangazi cha muda mrefu kilichoshuhudiwa nchini humo mwaka 2019 kutokana na mabadiliko ya tabianchi.