HabariMichezo

Japan yadunga Malkia Strikers msumari wa mwisho na kuibandua Olimpiki

Na JOHN KIMWERE August 3rd, 2024 1 min read

TIMU ya taifa ya voliboli ya wanawake Malkia Strikers imeaga Michezo ya Olimpiki mikono tupu baada ya kuangushiwa kichapo kingine chungu na Japan jijini Paris, Ufaransa.

Vipusa wa kocha Japheth Munala na msaidizi wake James Barasa kwa mara nyingine walijipata pabaya waliponyukwa seti 3-0 katika ukumbi wa South Paris Arena 1 hapo Agosti 3, 2024.

Japo Malkia walijikakamua kwa saa moja na dakika tatu – kinyume na mechi mbili zilizotangulia ambapo walinyolewa bila maji katika muda wastani wa dakika 58 – bado walifinywa kwa alama za 25-17, 25-22 na 25-12.

Pamela Adhiambo alichangia alama 17 naye Belinda Barasa akaleta alama 11 katika mechi hiyo.

Kilikuwa kichapo cha tatu katika mechi yao ya tatu na ya mwisho kwenye Kundi B, baada ya kusalimu amri ya Brazil na Poland kwa seti hizo hizo 3-0.

Kazi ngumu!

“Tulipambana kwa udi na uvumba angalau kuwinda seti moja hasa ile ya pili. Lakini wachezaji wangu waliteleza nao wapinzani wetu wakatupiku,” kocha Munala alisema.

Alikiri kwamba bado Kenya ina kibarua kigumu kuunda timu inayoweza kuhimili makali ya timu zingine duniani, licha ya kufana kwenye mashindano ya bara Afrika.

Kwenye mechi hizo za Kundi B Malkia ilimaliza nambari nne bila alama yoyote. Kundi hilo lilijumuisha wakali Brazil wanaoshikilia nafasi ya pili duniani, nambari nne Poland na nambari saba Japan huku Kenya ikiwa katika nafasi ya 20.

Timu ya taifa inatarajiwa kushika mkia katika nafasi mbili za mwisho – 11 au 12 – baada ya shughuli ya kuorodheshwa kwa timu mechi za makundi zikishatamatika. Kwenye makala yaliyopita ya mwaka 2020 jijini Tokyo, Japan, Malkia waliburuta mkia nambari 12.

Haya ni makala ya nne Kenya kushiriki Olimpiki na kuambulia patupu bila hata kushinda seti moja.

Timu ya taifa iliandikisha matokeo hayo katika makala ya Sydney 2000 (Australia), Athens 2005 (Ugiriki) na Tokyo 2020 (Japan).

Itakumbukwa kuwa baada ya toleo la Athens 2005 Malkia walikosa Olimpiki kwa miaka 16  – nchini Uchina 2008, Uingereza 2012 na Brazil 2016.