Michezo

Japo Tottenham hawakujisuka upya, wanayo makali ya kuridhisha uwanjani

November 12th, 2018 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

KATI ya klabu maarufu zaidi za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ni Tottenham Hotspur ndiyo iliyokosa kabisa kujishughulisha sokoni katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji.

Jitihada zao za kumsaka sogora mwenye uwezo mkubwa wa kuimairisha safu yao ya ulinzi ziliambulia pakavu waliposhindwa kumshawishi mchezaji yeyote kulijaza pengo la beki Kyle Walker aliyeyoyomea Man-City mnamo Julai 2017.

Licha ya hayo yote, Tottenham walizidi kutamba katika mapambano yote msimu huo wa 2017-18 na wakatinga ndani ya mduara wa tatu-bora katika EPL. Isitoshe, walibanduliwa kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA baada ya kuzidiwa maarifa na Juventus kwa jumla ya mabao 4-3.

Ufanisi huu ulikuwa wa kuwatia moyo sana vijana wa Tottenham ambao bado wanatiwa makali na kocha Mauricio Pochettino anayehusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Real Madrid mwakani.

Baada ya kupiga jumla ya mechi 12 za ufunguzi wa msimu huu, Tottenham wanazidi kudhihirisha ubabe wao katika soka ya Uingereza.

Kufikia mwishoni mwa wiki jana, walikuwa wanafunga mduara wa nne-bora kwa alama 27. Hii ilikuwa baada ya kuwapepeta Crystal Palace 1-0 uwanjani Selhurst Park.

Ikumbukwe kwamba Palace, ambao ? kwa sasa wananolewa na kocha Roy Hodgson waliwahi kuwakaba koo Arsenal kwa sare ya 2-2 katika mchuano mwingine wa EPL uliowakutanisha Selhurst mwishoni mwa Oktoba 2018.

Jinsi mambo yalivyo, dalili zote zinaashiria kwamba Tottenham wana kila nafasi na uwezo wa kutinga tena mduara wa tatu-bora msimu huu kwa kuwapiga kumbo washindani wao wakuu kirahisi.

Tayari vijana hawa wa Pochettino wamesajili ushindi mara tisa na kupoteza michuano mitatu. Tottenham ndicho kikosi cha pekee hadi kufikia sasa ambacho hakijaambulia sare katika mechi yoyote ya EPL.

Ufanisi huu umewachochea kudumisha pengo la alama chache mno kati yao na viongozi Man-City, Chelsea na Liverpool. Licha ya kujivunia masogora wale wale waliowachochea kutia fora katika kampeni za EPL na UEFA msimu jana, Tottenham wamezidiwa maarifa na Watford, Liverpool na Man-City kufikia sasa.

Kinachowaponza kwa sasa ni kushuka kwa viwango vya ubora wa masogora tegemeo kufu ya Victor Wanyama ambaye ameingiwa na kutu miguuni baada ya kupata msururu wa majeraha.

Udogo wa pengo la alama kati ya Tottenham na vikosi vingine saba kileleni mwa jedwali la EPL ni jambo linalotarajiwa kuzidisha ushindani katika jitihada za kuwania nafasi nne za kwanza.

Huku nidhamu ikiwa nguzo ya mafanikio yao, tayari kiota kikubwa cha matumaini kimejengeka miongoni mwa mashabiki ambao matarajio yao ni kuwaona vijana wa Pochettino wakilitia kibindoni taji la EPL kwa mara ya kwanza mwaka huu tangu 1961.

Hotspur wameonekana kujivunia ufufuo mkubwa chini ya Pochettino. Kwa pamoja na Man-City, uthabiti wa Tottenham msimu huu ni uhakika unaopania kuwakosesha usingizi wapinzani wakuu kufu ya Arsenal, Chelsea, Liverpool na Man-United wanaojivunia huduma za Paul Pogba na Alexis Sanchez ambao ni baadhi ya wachezaji mahiri zaidi duniani.