Jared Mwanduka: Mwanzilishi wa programu ya LearnsoftERP inayorahisisha kazi shuleni

Jared Mwanduka: Mwanzilishi wa programu ya LearnsoftERP inayorahisisha kazi shuleni

Na MAGDALENE WANJA

HATA kabla ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) mnamo mwaka 2016, Jared Mwanduka tayari alikuwa amevumbua mfumo wa kidijitali wa kurahisisha shughuli za kusimamia shule.

Alianza kwa kulenga shule za upili huku akifikiri shule za msingi hazingekumbatia mfumo huo kwa urahisi.

Haikuwa rahisi yeye kupata wanunuzi ambao walihitaji mfumo huo.

“Haikuwa rahisi jinsi nilivyotarajia kwani katika mazingira ya kawaida, wamiliki wa shule walisita kukubali kujaribu mfumo mpya,” akasema Mwanduka.

Bahati nzuri ilibisha pale ambapo rafiki yake wa muda alimwelezea kwamba kuna rafiki yake ambaye ni mwalimu mkuu na ambaye angehitaji huduma hiyo.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa biashara hiyo.

“Nilifurahia sana na nilipochapisha habari hizo kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii, nilipata wateja wengine ambao walitaka huduma yangu,” akasema Mwanduka.

Mnamo mwaka 2018, alipata kazi katika kampuni ya Coseke (K) Limited kama mhandisi wa programu.

“Katika kampuni hiyo, nilijifunza mengi na niliweza kupanda ngazi katika vyeo mbali mbali kazini hadi kiwango cha meneja wa kiufundi,”alisema.

Mwaka huo huo alianzisjha kampuni yake na kuipa jina Learnsoft Beliotech Solutions.

“Lengo langu lilikuwa ni kuniwezesha kufanya biashara yangu ya awali na kuwezesha shule za msingi na za upili kuendesha shughuli muhimu kwa urahisi,” anaongeza kusema Mwanduka.

LearnsoftERP ni programu ambayo huwezesha shughuli ya usajili wanafunzi, usimamizi wa mitihani, usimamizi wa matumizi ya fedha ikiwemo mishahara.

Jared Mwanduka alivumbua mfumo wa kidijitali wa kurahisisha shughuli za kusimamia shule. PICHA | MAGDALENE WANJA

Programu hiyo inauzwa kwa kima cha kati ya Sh45,000 na Sh200,000.

Kupitia programu hiyo, walimu wanaweza kukamilisha kazi zao kwa muda mfupi zaidi haswa mitihani ya wanafunzi.

Kufikia sasa, kampuni yake ina wafanyikazi 22 ambao hutekeleza shughuli mbali mbali.

Ndoto ya Mwanduka ni kufanya biashara hiyo katika nchi mbali mbali.

  • Tags

You can share this post!

Fahamu jinsi unavyoweza kuhifadhi mazingira kwa kutumia...

Wanaraga Kabras Sugar tayari kuchezesha densi...

T L