Jaribio la kupiga breki Wapwani KPA lazua joto

Jaribio la kupiga breki Wapwani KPA lazua joto

Na WINNIE ATIENO

VIONGOZI wa Pwani wamekashifu vikali ripoti ya seneti inayotaka Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) kutengea jamii zenye asili ya nje ya Pwani nafasi zaidi za ajira kuliko Wapwani.

Viongozi wa kidini, watetezi wa haki za kibinadamu na wanasiasa wameungana kwa kauli moja kupuuzilia mbali agizo hilo la kamati ya seneti lililotolewa baada ya kubainika kuwa idadi ya waajiriwa katika bandari ambao ni Wamijikenda imezidi idadi inayokubaliwa kisheria.

Kamati ya Seneti inayosimamia masuala ya utangamano wa kitaifa, ilitoa agizo kwamba KPA itengee jamii zenye asili ya nje ya Pwani nafasi zaidi za ajira kuliko Wapwani ili kuleta usawa wa kijamii.Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko alikashifu walionakili ripoti hiyo akisema walikosea kwa kutaja Wamijikenda kama kabila.“Kwanza Wamijikenda si kabila.

Ni mkusanyiko wa makabila tisa. Wasijaribu kutuletea siasa za kugawanya Wakenya, wakati huu ni wa kuunganisha Wakenya,” akasema.Kulingana naye, jamii za Pwani zimekuwa zikitengwa hata katika nafasi za ajira kitaifa hivyo basi hawafai kudhulumiwa wanapoonekana kupata nafasi kwani idadi yao pia ni ndogo kijumla.

“Tujiulize tuko na wakurugenzi wangapi katika taasisi za serikali ambao ni wa jamii za Wamijikenda. Tume gani inasimamiwa na Mmijikenda? Wasituanzishe maanake tukianza hawataweza. Tutafungua madaftari tufanye utafiti na tuweke bayana” alisema Bi Mboko.

Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, alisema bandari hiyo ni rasilimali muhimu kwa Wapwani kwa hivyo wana haki kufaidika kutokana nayo.“Na tukisema Mpwani hatumaanishi mpwani sababu ya kabila. Ikiwa umeweka rasilimali yako hapa, unaishi hapa wewe ni Mpwani,” akasema.

Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa katika Seneti, waajiriwa kutoka jamii za Wamijikenda ni 2,274 kati ya watu 6,470 walioajiriwa KPA kijumla.Wamijikenda wanajumuisha makabila ya Wadigo, Wachonyi, Wakambe, Waduruma, Wakauma, Waribe, Warabai, Wajibana na Wagiriama na wengi wao wanapatikana katika Kaunti za Kilifi na Kwale.

Idadi ya Wataita ambao pia ni mojawapo ya jamii za asili ya Pwani ni 496.Mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali alisema katika mazungumzo na Wizara ya Fedha na ile ya Uchukuzi, wabunge 39 wa Pwani walikubaliana kwamba Pwani itatengewa nafasi zaidi za ajira.

Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Kiislamu, Sheikh Juma Ngao alitilia shaka utoaji wa ripoti hiyo wakati huu ambapo nchi inajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwaka ujao.Kulingana naye, Wapwani wana haki ya kuajiriwa katika bandari ya Mombasa sawa na jinsi jamii nyingine wanavyoajiriwa kwa wingi katika mashirika yaliyo maeneo yao.

Kwa upande wake, Bw Julius Ogogoh ambaye ni mtetezi wa haki za kibinadamu alisema hali katika KPA sio tofauti katika mashirika mengine ya umma nchini.Kulingana na Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa iliyopitishwa mwaka wa 2008, ni marufuku kwa jamii moja kushikilia zaidi ya theluthi moja ya nafasi za kazi katika shirika lolote la kiserikali.

You can share this post!

Siku Mudavadi, Kalonzo ‘walitekwa nyara’ na wanakijiji

Mbunge adai roho ya Kingi ingali katika ODM

T L