MakalaSiasa

JARIBIO LA MAPINDUZI 1982: Waliopanga njama walivyonyongwa

July 31st, 2018 2 min read

Na WANDERI KAMAU

JUMATANO, Agosti 1, 2018, Kenya  itaadhimisha miaka 36 tangu kutokea kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi mnamo 1982.

Ni tukio la kwanza ambalo limewekwa katika kumbukumbu ya historia ya Kenya hadi sasa, kwani ilikuwa ni mara ya kwanza kutokea.

Majaribio hayo, ambayo yalitokea Jumapili yalilenga kumpindua Rais Mstaafu Daniel arap Moi.

Mapinduzi hayo yalianza baada ya kundi la Wanajeshi wa Kitengo cha Hewa (Kenya Airforce) kuteka Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Eastleigh, Nairobi saa kumi za usiku.

Saa 12 alfajiri, kiongozi wa kundi hilo, Hezekiah Ochuka na Sajenti Pancras Oteyo Okumu waliteka studio za Kituo cha Habari cha Kenya (KBC) wakati huo ikiitwa Voice of Kenya (VOK), ambapo walitangaza kwamba jeshi lilikuwa limeipindua serikali.

Chini ya uelekezi wa Bw Ochuka, Koplo Bramwel Injei Njereman alikuwa akiendeleza mpango wa kuilipua Ikulu ya Nairobi, makao makuu ya polisi wa kitengo cha GSU na Kambi ya Jeshi ya Laikipia.

Saa 12 alfajiri, kiongozi wa kundi hilo, Hezekiah Ochuka na Sajenti Pancras Oteyo Okumu waliteka studio za KBC, ambapo walitangaza kwamba jeshi lilikuwa limeipindua serikali. Walifanya hivyo kwa kumlazimsha mtangazaji Leonard Mambo Mbotela.

Kwa hayo, Koplo Njereman akawaamuru marubani watatu kuendesha ndege mbili aina ya ‘F-5E Tiger’ na ‘Strikemaster’ ambazo zingetumika katika mashambulio hayo. Hata hivyo, marubani hao waliapa kutofanya hivyo. Walirusha bomu hizo katika msitu wa Mlima Kenya na kurudi Nanyuki.

Mapinduzi hayo yalikuwa yamepangwa kuwiana na michezo ya wanajeshi ambayo ilikuwa ikiendelea mjini Lodwar. Wakati huo wanajeshi wengi walikuwa wamehudhuria michezo hiyo. Hilo lililenga kuhakikisha kwamba mapinduzi hayo hayangekabiliwa na upinzani mkubwa.

Lakini kulikuwa na mipango ya kuwakabili wanamapinduzi hao iliyokuwa ikiendelea kichinichini.

Wanajeshi waliokuwa wakiendeleza mipango hiyo ni Luteni Jenerali John Sawe (Kamanda wa Jeshi nchi nzima) na Meja Jenerali Mahmoud Mohamed, Brigedia Bernard Kiilu na Meja Humphrey Njoroge. Walikubaliana Jen Mohamed kuongoza operesheni hiyo.

Kwanza, walivamia KBC ambapo waliwateka wanajeshi waasi. Kundi pia lilimshurutisha mtangazaji Mbotela kutangaza kwamba Rais Daniel Moi alikuwa asharudi mamlakani.

Hata hivyo, wanamapinduzi hao walifanikiwa kuidhibiti nchi kwa karibu saa sita chini ya uongozi wa Ochuka.

Waliposhindwa, walitorokea Tanzania ila wakarudishwa Kenya ili kufunguliwa mashtaka. Wengine waliohusishwa na mapinduzi hao ni kiongozi wa ODM Raila Odinga na babake, Jaramogi Oginga Odinga.

Inasemekana kuwa sababu kuu ya kutofaulu kwa mapinduzi hayo ni kwa kuwa wanajeshi wengi hawakutekeleza majukumu binafsi ambayo walikuwa wamepewa kutekeleza.

Matokeo ya mapinduzi hayo ni kuwa wanajeshi zaidi ya 100 na watu 200 walifariki, ambapo baadhi hawakuwa Wakenya.

Watayarishaji wa mapinduzi hayo baadaye walikamatwa na kufunguliwa mashtaka katika mahakama za kijeshi. Wengi wao walinyongwa baada ya kupatikana na hatia.

Kando na Ochuka, wengine walionyongwa ni Bramwel Injeni, Koplo Walter Ojode na Pancras Okumu. Watu 900 walifungwa gerezani. Watu wengi walionyongwa walizikwa katika Gereza Kuu la Kamiti.