Jasiri wa Kenya watamba miereka ya Tong-Il Moo-Do

Jasiri wa Kenya watamba miereka ya Tong-Il Moo-Do

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MABINGWA watetezi Kenya walikabiliwa na upinzani mkali licha ya kujiongezea idadi ya medali kwenye mashindano ya Mombasa Open Tong-IL Moo-Do International Martial Arts yaliyokamilika jana usiku.

Tukienda mitamboni kukiwa kumebakia vitengo kadhaa mashindano kufika tamati, timu ya taifa Jasiri ilikuwa ikipishana na wapinzani wao wakuu Ufilipino kwenye jedwali la medali.Katika siku ya pili na mwisho ya miereka hiyo iliyoandaliwa ukumbi wa Aga Khan Academy, Kenya iliendelea kuwa kileleni ikiwa na dhahabu sita, fedha tisa na shaba 15.

Ilifuatiwa na Ufilipino iliyokuwa na medali sita za dhahabu, nne za fedha na mbili za shaba.Burkina Faso walikuwa nafasi ya tatu kwa medali mbili za dhahabu na moja ya shaba huku Angola ikiwa na medali mbili za dhahabu.Japan na Marekani zina medali moja ya dhahabu na moja ya fedha.

Ethiopia na Zambia zina medali moja moja ya fedha hali Korea Kusini na Ivory Coast zina medali moja moja ya shaba.Katika siku ya ufunguzi Jumamosi, Jasiri ilishinda medali tatu za dhahabu, tatu za fedha na mbili za shaba katika kitengo cha Forms.

Katika kitengo cha Novices Bracket A, Samson Mambo wa Jasiri alinyakuwa medali ya dhahabu baada ya kupata pointi 9.132 akifuatiwa na mwenzake Andrew Wanje aliyepata fedha. kwa kuwa na alama 8.866 points hali Godwin Ogene Ifeanyi kutoka Nigeria akapata medali ya shaba kwa kuwa na pointi 8.733.

Katika Individual Bon Kids B, Kenya ilinyakuwa medali zoite tatu kupitia kwa Gideon Bwire, dhahabu (6.900), David Mwangi, fedha (6.550) na Joseph Clement, shaba (6.100).Jasiri pia ilitawala shindano la Individual Bon Kids A ambapo Mark Bakari alipata dhahabu (7.150), Akelo Hafswa, fedha (7.150) na Emmanuel Wafula, shaba (6.500).

Katika kitengo cha spurring, Neville Yugis Ephraim alifuzu kwa nusu fainali katika shindano la Bantam A baada ya kumshinda Mkenya mwenzake Suleiman Hamadi 2-0.Mwengine aliyefuzu kwa nusu fainali ni Santos Mharjude Delos aliyeshinda 8-2 dhidi ya Fredrick Munga Omollo.

Ephraim atapambana na Athman Bakari hali Delos atapambana na Mkongo Daniel Mantondo Chon.Wakenya wawili nao wamefuzu kwa nusu fainali katika shindano la Bantam B. Washington Burmer alimshinda Mkongo Barthelemy Yuk Song 8-0 na George Itumo kumshinda Mkenya mwenzake Khamisi Mkuruto 7-2.

Pia katika kitengo cha Fly A, Wakenya wana uhakika wa kushinda medali mbili kati ya tatu. Raymark Bais alimshinda Muethiopia Mihret Asega Yitayih 8-1 huku Edwin Musungu Otota akimshinda Suleiman Hamadi 2-0. Bais anakutana na Festus Baraka hali Otota atapambana na Luckson Miti kutoka Zambia.

Katika kitengo cha Fly B, Wakenya Mohamed Yahya na Samuel Odhiambo walijiandikishia tikiti ya nusu fainali baada ya kupata ushindi wa 2-0 na 4-2 dhidi ya Bumiyo Nisubire na Collins Ndunda mtawalia.

You can share this post!

Kenya yapigiwa debe kuandaa Riadha za 2025

Raga: Kabras, Oilers juu ligi ikienda Krisi

T L