Jamvi La Siasa

Je, Joho atarejesha nyota ya Pwani katika siasa za kitaifa?

March 16th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

Kwa muda mrefu, viongozi wa kisiasa katika ukanda huo wamekuwa wakikosolewa kwa kukosa kulipa eneo mwonekano na usemi katika siasa za kitaifa, kama walivyofanya waziri wa zamani Karisa Maitha na mwanasiasa Ronald Ngala.

Kando na Bw Joho, viongozi wengine kutoka eneo hilo ambao wamekuwa na mwonekano mkubwa wa kitaifa katika eneo hilo ni Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi, Waziri wa Uchumi wa Baharini Salim Mvurya, waziri wa zamani Chirau Ali Mwakwere kati ya wengine wengi.

Licha ya wanasiasa hao kuhudumu katika nyadhifa kubwa kubwa serikalini, wamekuwa wakilaumiwa kwa kutoinua usemi, ushawishi na mwonekano wa kisasa wa ukanda huo katika siasa za kitaifa.

“Ukweli ni kuwa, Pwani imekuwa chini ya kivuli cha kisiasa cha maeneo mengine nchini kwa muda mrefu. Kinyume na maeneo mengine kama Luo Nyanza, yaliyo na viongozi wao maalum kama Raila au Ukambani, linaloongozwa na Kalonzo Musyoka, Pwani haijakuwa na kiongozi au msemaji maalum kisiasa. Kando na marehemu Maitha na Ngala, viongozi wengine ambao wamefanikiwa kushikilia nyadhifa kubwa kubwa wamefeli kuirejesha nafasi iliyokuwa katika enzi za Bw Maitha na Ngala,” asema Bw Katana Kazungu, ambaye ni mdadisi wa masuala ya kisiasa ya eneo hilo.

Hata hivyo, anasema kuwa kuna matumaini eneo hilo linaweza kurejesha ushawishi wake wa kisiasa, ikiwa Bw Joho atafanikiwa kutwaa uongozi katika chama cha ODM.

Hata hivyo, Bw Joho anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Bw Oparanya, kwani tayari kuna wanasiasa ambao wamesema watampigia debe kuchukua uongozi kutoka kwa Bw Odinga, ikiwa atafanikiwa kuteuliwa kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Baadhi ya wanasiasa wanaoonekana kuwa katika kambi ya Bw Joho ni wabunge Junet Mohammed (Suna Mashariki), Babu Owino (Embakasi Mashariki) na Seneta Ledama Ole Kina (Narok).

Kambi ya Bw Oparanya imetajwa kuwashirikisha Seneta Edwin Sifuna (Nairobi), Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi na mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi.

Wadadisi wanasema kuwa ikiwa Bw Joho atafanikiwa kuchukua uongozi wa ODM na kuungana na viongozi kama Bw Kingi, Bw Mvurya, Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba eneo hilo linaweza kurejesha usemi wake wake katika siasa za kitaifa.