Michezo

Je, Kenya ni taifa la wanariadha wapenda pufya?

June 2nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) imempiga marufuku ya miaka minne Mkenya Mikel Kiprotich Mutai kwa hatia ya kutumia dawa haramu za kusisimua misuli.

Mwanariadha mwingine mzawa wa humu nchini aliyekabiliwa na shoka la kamati hiyo ni Japhet Kipchirichir Kipkorir.

Marufuku ya Mutai yanaanza kutekelezwa Machi 20, 2020 na matokeo yote yam bio alizoshiriki kuanzia Disemba 15, 2019 sasa yamefutiliwa mbali.

Kwa mujibu wa shirika la kupambana na pufya duniani (WADA), Mutai alikuwa ametumia Norandrosterone baada ya chembechembe za dawa hiyo haramu kupatikana kwenye sampuli za damu yake.

Mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Paul Tergat amesema jinamizi la matumizi ya pufya humu nchini litadhibitiwa iwapo watakaopatikana wataadhibiwa kwa kiwango sawa na wahalifu wengine na kufungwa jela.

Rais huyo wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Kenya (Nock) ametaka pia watumiaji wa pufya kuadhibiwa vikali zaidi ili kuepusha Kenya na hatari ya kupigwa marufuku.

 “Yasikitisha kuwa visa vya matumizi ya pufya vinaongezeka katika riadha yetu. Yatupasa kufanya matumizi ya pufya kuwa kosa la jinai,” akasema Tergat.

Mwezi jana, Mkenya mwingine, Vincent Kipsegechi Yator, alipigwa marufuku ya miaka minne kwa hatia ya kutumia dawa zilizoharamishwa michezoni.

Kenya iko katika kategoria ya kwanza (A) ya mataifa ambayo wanamichezo wao wanatumia sana dawa haramu ili kujipatia ufanisi kwa njia za mkato. Nigeria, Ethiopia, Bahrain, Morocco, Ukraine na Belarus ni mataifa mengine katika kategoria hiyo.

Kenya imekuwa ikimulikwa sana na WADA pamoja na IAAF kutokana na kukithiri kwa visa vya matumizi ya pufya miongoni mwa wanariadha wake tangu 2012. Tangu mwaka huo, zaidi ya watimkaji 40 wamepigwa marufuku wakiwemo Asbel Kiprop, Sammy Kitwara, Jemimah Sumgong na Rita Jeptoo.

Wanariadha wazawa wa Kenya na raia wa Bahrain, Albert Rop na Ruth Chebet pia walipigwa marufuku mwaka huu kwa hatia ya kutumia pufya. WADA imefichua kuwa wanariadha 138 kutoka Kenya wamewahi kutumia pufya kati ya 2004 na Agosti 2018.