Habari Mseto

Je, KRA itateua msimamizi lini?

March 2nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU
AWAMU ya Msimamizi Mkuu wa Shirika la Kukusanya Ushuru (KRA) John Njiraini inaelekea kukamilika licha ya kuwa shirika hilo halijatangaza nafasi hiyo kuwa wazi.

Awamu hiyo ya pili ya Bw Njiraini inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii, Machi 3.

Njiraini alijiunga na KRA 2012 baada ya kuteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Fedha.

Kamishna huyo alifikisha miaka ya kustaafu (60) miezi miwili iliyopita, na kufikia sasa, KRA haijaonekana kuwa na haraka ya kutafuta atakayemrithi.

Jumatatu, Njiraini na bodi ya KRA alikataa kuzungumzia suala hilo baada ya kuulizwa na mwanahabari wa Nation.

Mahakama ya Ajira na Uhusiano wa Leba mwezi jana ilimruhusu Bw Njiraini kuendelea kukaa afisini licha ya mwanaharakati wa sheria Okiya Omtatah kushinikiza kuondolewa kwake.