Makala

Je, ni kukata kitambi au kumaliza kitambi?

February 28th, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

WATU wengi siku hizi wanapambana na tatizo la kuwa na kitambi kinachosababishwa na mkusanyiko wa mafuta tumboni.

Sababu ya kuwa na mafuta mengi tumboni ni kula vyakula visivyostahili, kutumia vyakula vya wanga kupita kiasi, kutokunywa maji ya kutosha kila siku, kula chakula kizito muda mchache kabla ya kwenda kulala.

Sababu nyingine ni kukaa muda wa saa nyingi kwenye kiti, kutofanya mazoezi, kuwa na msongo wa mawazo au kula vyakula vinavyopikwa kwa kuvitumbukiza ndani ya mafuta mengi.

Unachoweza kufanya kuondoa kitambi

Asali na limau

Chukua asali kijiko kimoja na juisi ya limau vijiko viwili, changanya ndani ya glasi moja ya maji ya uufutende na unywe yote mara tu ukiamka asubuhi.

Maji fufutende

Kunywa maji ya joto la aina hii kama lita moja hivi wakati tumbo likiwa tupu hasa asubuhi unapoamka. Hii inasaidia kusafisha mwili na kuondoa mafuta yasiyohitajika.

Tangawizi

Chemsha chai ya tangawizi, epua na usubiri ipoe kidogo, ongeza asali na pilipili ya unga. Kunywa kila siku asubuhi mapema ukiamka tu. Asali inasaidia kuyeyusha mafuta wakati pilipili itauongezea nguvu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

Siki ya tufaa

Siki ya tufaa (apple cider vinegar) inasaidia kupunguza njaa na kukufanya ujisikie umeshiba kwa kipindi kirefu. Kunywa kijiko kikubwa kimoja cha siki ya tufaa mara moja kwa siku, kila siku wakati unakula chakula cha usiku.

Mdalasini

Mdalasini hufanya kazi ya kuchoma mafuta mwilini. Chukua kijiko kidogo kimoja cha mdalasini ya unga na uweke ndani ya glasi moja ya maji ya moto na uache kwa dakika tano hivi. Ongeza kijiko kidogo kimoja cha asali ndani yake na ukoroge vizuri, kisha unywe mchanganyiko wote asubuhi unapoamka.

Juisi ya limau

Kunywa maji ya limao kila mara kunasaidia kuondoa mafuta tumboni kwa haraka. Ongeza juisiya limau vijiko viwili ndani ya glasi moja ya maji, koroga vizuri na unywe asubuhi ukiamka kila siku.

Kitunguu saumu

Ili kupunguza mafuta tumboni katakata vipande vidogo vidogo punje tatu h za kitunguu saumu na unywe na maji vikombe viwili asubuhi.

Tango

Tango lina asilimia 96 ya maji na asilimia zinazobaki ni nishati. Tumia kachumbari yenye tango ndani yake kila siku au kula tu tango moja kila siku ili kupunguza mafuta tumboni kwa haraka.

Chai ya kijani

Chai ya kijani maarufu ‘Green tea’ hufanya kazi ya kuondoa sumu mwilini jambo linalosaidia pia kuchoma mafuta yaliyozidi. Kunywa chai hii kila siku pia kunasaidia ngozi kukua pia kulifanya tumbo kukaa sawa bila kuwa na mafuta mengi.