Makala

Je, nini maana ya ugonjwa wa sciatica?

November 18th, 2020 4 min read

Na MARY WANGARI

Je, sciatica ni nini? Kwa mujibu wa Dkt Brian Rono, Mtaalam wa Viungo na Upasuaji, sciatica inayofahamika pia kama uchungu wa sehemu ya chini ya mgongo, ni hali inayotokea wakati kuna shinikizo kwenye neva za misuli.

“Uchungu wa sehemu ya chini ya mgongo unahusisha msisimuko wa misuli kwenye uti wa mgongo. Hali hiyo pia inahusu hisia ya kudungwadungwa kwenye makalio au uchungu mkali unachomokeza mgongoni.

“Hali hii hutokea wakati mizizi ya neva inaposhinikizwa hali inayosababisha umbo la mifuko ya neva kufura au kubadilika hivyo kusababisha uchungu mkali unaochomoza katika sehemu ya chini ya mgongo, wayo wa mguu, sehemu ya ndani au nje kwenye magoti,” anafafanua daktari huyo.

Mtaalam huyo wa afya jijini Nairobi, anaeleza kuwa maradhi hayo husababisha uchungu mkali mgongoni, kwenye miguu na hata huweza kusababisha kufa ganzi.

Takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia 80 ya watu kote duniani wanaugua ugonjwa huo usiobagua jinsia wala umri huku ukiathiri wake kwa waume wenye umri wa miaka 20 na zaidi.

Ingawa ugonjwa wa sciaticva unafahamika vilevile kama uchungu wa sehemu ya chini ya mgongo, wataalam wanatahadharisha dhidi ya kukanganyikiwa kuhusu matatizo ya uchungu kwenye mgongo na hali hiyo.

Si maumivu yote ya mgongo ambayo ni sciatica kulingana na wataalam kutoka Kituo cha Kitaifa kuhusu Teknolojia ya Bayolojia ambacho ni tawi la Taasisi ya Afya America.

Tafiti zimeonyesha kuwa sciatica inaweza kupitishwa kijeni ambapo hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Masuala mengineyo yanayochangia ndwele hiyo ni pamoja na hali ya kikazi inayohusisha kusimama au kuketi katika hali fulani kwa muda mrefu kama vile madereva wa trela na wanaoendesha mashine.

Dkt Rono, anatahadharisha kuwa kuendelea kushinikizwa kwa mishipa ya neva kwa muda mrefu bila matibabu kunaweza kusababisha mgonjwa kupooza.

Isitoshe, dalili hizo zinaweza kuwa zikijirejelea hata baada ya mgonjwa kutibiwa na kuonekana kupona hali inayodhihirisha ni kwa nini ni muhimu kuzingatia mikakati ya kujikinga dhidi ya gonjwa hilo.

Kuna visababishi anuai vya sciatica jinsi vilivyoorodheshwa ifuatavyo:

Sciatica husababishwa na nini?

Misuli kukazwa kupita kiasi – Misuli ya sehemu ya chini ya mgongo ni nguzo inayowezesha utekelezaji wa shughuli za kila siku. Matatizo hayo hutokea wakati misuli inapofanyishwa kazi kupita kiasi au inapokuwa dhaifu.

Jeraha kwenye viungo – Kuna viungo maalum vinavyowezesha sehemu ya chini ya mgongo kuwa imara.

Sehemu hiyo inapojeruhiwa kutokana na kusongeshwa kwa nguvu au kushinikizwa kwa muda mrefu huweza kusababisha sciatica.

Mapozi duni ya kusimama au kuketi – Kwa mfano kujipinda unapoketi mbele ya televisheni ukitazama au kuketi ukiwa umepinda mgongo husababisha misuli kuchoka, pamoja na kushinikiza nyonga na viungo vinavyofunika mifupa ya uti wa mgongo.

Dhuluma – Dhuluma za muda mrefu kama vile kupigwa au mateso husababisha misuli kupoteza usawa kama vile kujikaza kunakofaa na kuidhoofisha hali ambayo inaweza kusababisha uchungu vilevile.

Umri – Kudhoofika kutokana na umri pamoja na masuala ya kurithishwa kiukoo yanaweza kusababisha mabadiliko ya kudhoofisah mifuko ya mifuka (inayofahamika pia kama maradhi ya kudhoofika kwa mifuko ya mifupa) na kudhoofika kwa nyonga za uti wa mgongo (kunakofahamika kama maradhi ya kudhoofika kwa nyonga)

Kulingana na wataalam wa afya, kuzeeka kwa kawaida husababisha kupungua kwa uzani wa mifupa, nguvu na mshikamano wa misuli na viungo athari zinazoweza kupunguzwa kupitia mazoezi ya viungo vya mwili mara kwa mara, mbinu inayofaa ya kuinua na kusogesha mizigo, lishe bora na uzani unaofaa mwilini na kuepuka uvutaji sigara.

Ugonjwa huo unapozorota zaidi kama vile mifuko ya neva inapoanza kufura, wataalam wanapendekeza vipindi vya mazoezi ya kimatibabu ili kuimarisha na kulainisha misuli pasipo kulazimika kufanyiwa upasuaji.

Saratani, maradhi ya figo, mfuko wa mkojo, mfuko wa uzazi na mayai ya kike ni miongoni mwa masuala mengineyo yanayosababisha sciatica.

Matibabu ya sciatica yanajumuisha:

Kupumzika kutokana na shughuli za kuchosha – Epuka kuketi, kuinama, kujipinda, kuendesha gari, mashine au mitambo au kuinua vitu vizito kwa muda mrefu.

Matibabu ya barafu – barafu inapogusishwa katika sehemu ya chini ya mgongo kwa dakika 15 kila baada ya saa 1-2 husaidia kupunguza uchungu na kuwashwa kwa misuli.

Wataalam pia wanatahadharisha dhidi ya kutumia joto kwa saa 48 baada ya kupata jeraha.

Matibabu ya kuzuia maumivu (NSAIDs): kama vile aspirin, advil, aleve, ibuprofen miongoni mwa dawa nyinginezo kuambatana na ushauri wa daktari.

Mazoezi ya viungo vya mwili – Epuka mtindo wa kukaa tu bila kufanya mazoezi, fanya mazoezi rahisi ya kusogesha viungo vya mwili na kuvilainisha (hasa misuli ya miguu na mgongo) ambayo inaweza kusaidia kupunguza kiwango na muda wa maumivu hayo pamoja na kujirejelea kwa maumivu ya sciatica.

Unapofanya mazoezi, hata hivyo, tahadhari usijihusishe na mazoezi ambayo badala yake yatakuzidishia maumivu.

Mtindo wa kulala – Badilisha mtindo wako wa kulala ili kupunguza shinikizo kwenye sehemu ya chini ya mgongo wako.

Hakikisha kitanda chako ni imara na kinachoweza kukustahimili vyema na pia lalisha kichwa chako kwenye mto.

Endapo unapendelea kulala chali, jaribu kulala ukiwa umeweka mto chini ya magoti yako.

Ikiwa unapenda kulala kwa ubavu, lala ukiwa umeweka mto katikati ya mapaja yako.

Iwapo unapenda kulala kwenye ubavu ukiwa umejipinda, kuweka taulo iliyokunjwa chini ya kiono chako kutakufaa mno.

Mbinu nyinginezo za kujikinga kutokana na sciatica ni pamoja na mazoezi ya kimatibabu ya kuimarisha mifupa ya sehemu ya tumbo, nyonga na mgongo ili kuzuia maradhi hayo kujirudia.

Umuhimu wa kutilia maanani mapozi ya mwili ama unapolala au kuketi hauwezi ukasisitizwa vya kutosha tunapozungumzia kuhusu kupunguza maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo.

Hata hivyo, ni muhimu zaidi mgonjwa kumwona daktari anapoanza kuona dalili hizi:

Homa mwilini isiyoweza kufafanuliwa, maumivu makali yanayoendelea kwa zaidi ya wiki moja, uvimbe au kugeuka rangi kwenye mgongo au uti wa mgongo, hisia ya kudungwadungwa, uchungu au kufa gazi kunakosambaa kwenye miguu au magoti, miguu kuwa dhaifu, matatizo ya kwenda haja au kwenye kibofu, maumivu mgongoni kutokana na kugongwa, kuanguka pamoja na kupoteza uzani kwa njia isiyoweza kueleweka.

[email protected]