MakalaSiasa

Je, Uhuru amefanikiwa kuzima 'Tangatanga?

April 21st, 2019 3 min read

WANDERI KAMAU na PETER MBURU

HATUA ya maafisa wa usalama katika Kaunti ya Nyeri kususia kuhudhuria hafla ya Naibu Rais William Ruto mnamo Alhamisi imeibua hofu kuwa huenda ikawa njama ya serikali kuanza ‘kuumaliza kisiasa’ mrengo wa ‘Tanga Tanga.’

Ilikuwa mara ya kwanza kwa ripoti za Dkt Ruto kukosa viongozi wa usalama eneo anapozuru, kwani siku za mbeleni wamekuwapo katika hafla zake zote.

Kulingana na wachanganuzi, tukio hilo, pamoja na hatua ya serikali kuwanyang’anya walinzi baadhi ya viongozi wanaohusishwa kwa karibu na mrengo huo ambao umekuwa ukimfanyia kampeni Dkt Ruto, ni ishara ya hatari kwa ‘Tanga Tanga’.

Baadhi ya viongozi waliopokonywa walinzi ni wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Alice Wahome (Kandara) na Kimani Ngunjiri (Bahati), Gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu na Seneta Susan Kihika (Nakuru) kati ya viongozi wengine.

Duru zilieleza Jamvi la Siasa kuwa kando na hao, kuna viongozi wengine zaidi ya 20 ambao wamepangiwa kunyang’anywa walinzi wao.

Viongozi wote waliopokonywa walinzi aidha, kisadfa, ni wa kutoka jamii ya Mlima Kenya, ijapokuwa Dkt Ruto amekuwa na uungwaji mkono zaidi kutoka jamii ya Bonde la Ufa.

Kulingana na wachanganuzi, hiyo ni adhabu kwa viongozi hao, kwani wamekuwa wakikaidi agizo la Rais Uhuru Kenyatta kutoendeleza kampeni za 2022.

“Nadhani kilicho wazi kwa sasa ni kuwa serikali imeanza kutumia asasi zake kuwanyamazisha wanasiasa ambao wamekaidi kiwazi agizo la Rais Kenyatta kutoendeleza kampeni za 2022. Hii ni dalili kuwa mengi yaja njiani. Tutawaona wanasiasa wengi wakibadilisha misimamo yao,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

Kulingana na mtaalamu huyo, kukosekana kwa walinzi katika hafla ya Dkt Ruto kunaashiria kuwa huenda maafisa wakuu wa usalama serikalini wamepokea maagizo kuwasusia viongozi ambao wanaonekana kumkaidi Rais.

“Lililo wazi ni kuwa Rais Kenyatta anataka kuthihirisha kuwa bado yumo mamlakani, na kuwa kuna athari kwa kiongozi yeyote anayekaidi maagizo yake,” asema Prof Njoroge.

Japo wengi wa viongozi hao hawajazungumza, Bw Ichungwa Jumatano alilalamika kuwa hatua ya kuwaondolea walinzi haikuwa na uwazi, maelezo yake yakikinzana na yale ya serikali.

“Walinzi wangu wote walikuwa wa kitengo cha polisi wa AP, hivyo sijui sababu haswa ni nini. Hili lingekuwa zoezi la uwazi halingetekelezwa kwa mapendeleo,” Bw Ichung’wa akasema.

Huku hayo yakijiri, Rais Kenyatta naye wiki hii alitetea vikali muafaka wa kisiasa kati yake kiongozi wa ODM, Raila Odinga, na kukashifu ukosoaji kutoka kwa Dkt Ruto na wandani wake, kwamba lengo lake kuu ni kuisambaratisha Jubilee.

Rais aliwakosoa viongozi wanaoeneza siasa kuwa Bw Odinga anataka kuvunja Jubilee kuwa ‘wasiofikiria’ na wanaojifikiria wao tu, akiwataka wananchi kufanya juhudi kuhakikisha kuwa wanawazuia viongozi wenye ubinafsi kutoongoza.

“Nashangaa sana kuwa wakati tunajadili jinsi ya kuunganisha watu, unaposoma magazeti na kusikiliza watu kwenye mazishi na harusi wakizungumza, unasikia wakisema (Raila) anataka kuwa Rais 2022 nami nataka kuendelea kuongoza.

“Hajawahi kuniambia anataka kuwa Rais, sijamwambia kuwa nataka kuendelea kuwa Rais 2022. Tumekuwa tukizungumza tu kuhusu mambo yanayoathiri watu wetu,” Rais akasema, alipokuwa katika hafla iliyoandaliwa na Bw Odinga kuhusu miundomsingi barani Afrika.

Rais alisema anaunga Bw Odinga mkono, na kukashifu wote wanaomwingilia.

Wachanganuzi wanaeleza kuwa mwelekeo huo unaashiria njama na mikakati ya kumnyamazisha kabisa Dkt Ruto na kundi hilo.

“Kwa kuwaondolea walinzi, ujumbe mkuu wa serikali (Rais Kenyatta) ni kuwa bado yu mamlakani na ana uwezo wa kuwaadhibu ikiwa watakaidi maagizo yake,” asema Oscar Plato, ambaye pia ni mchanganuzi wa kisiasa.

Bw Ichung’wa alisema kuwa hakuna aliyefahamishwa lolote kabla ya walinzi wake kuondolewa, na akalalamika kuhusu usalama wake. Kulingana na Bw Ichung’wa, kiongozi yeyote ana haki ya kufahamishwa mabadiliko yoyote yanayofanywa na serikali kuhusu usalama wake.

“Nilikuwa nje ya nchi nilipofahamishwa kuwa walinzi wangu wamebadilishwa bila kufahamishwa. Hili ni tishio kwa maisha yetu. Huu pia ni ukiukaji wa sheria kwani ulinzi ni haki ya kila mbunge,” akalalama Bw Ichung’wa.

Viongozi wengine ambao walipokonywa walinzi, hata hivyo, wamekuwa kimya kuhusu hilo mbele ya umma, huenda kwa hofu kuwa watapokea adhabu zaidi.

Asasi za usalama hazijatoa habari za kuridhisha kuhusu ripoti za walinzi wa viongozi hao kuondolewa, japo waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alitaja hatua hiyo kuwa mchakato wa mageuzi yanayoendelea katika idara za polisi, katika kitengo cha kulinda viongozi mashuhuri.

“Mtu hafai kulalamika kwa kuwa hatua hiyo imeanza na yeye, wala haijaanza na mwingine. Tuwache kuingiza siasa katika zoezi hili linalofanywa na idara ya polisi,” akasema Dkt Matiang’i.

Siku mbili tu baada ya walinzi wao kuondolewa, Dkt Ruto mnamo Jumapili, Aprili 14 alizuru Kaunti ya Nakuru (ambapo Bi Kihika na Bw Ngunjiri ni waathiriwa wa hatua hiyo) lakini hakusema lolote.

Wakati huo ambapo aidha alifungua kituo cha polisi, wakuu wa usalama kaunti hiyo walikuwapo na wakampokea akiendeleza siasa za kumvamia Bw Odinga, kinyume na Alhamisi alipokuwa katika Kaunti ya Nyeri.