Makala

Je, unajua maziwa ya ngamia ni kinga kwa magonjwa hatari?

March 19th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KATIKA nyakati hizi ambapo watu wengi wamekuwa wakilalamikia ongezeko la magonjwa yasiyoeleweka, wataalamu wa afya wametaja maziwa ya ngamia kama mojawapo ya ‘kinga’ bora kwa maradhi tofauti.

Wataalamu wanasema kuwa maziwa hayo yana madini muhimu ambayo huimarisha uwezo wa mwili wa mwanadamu kujikinga dhidi ya maradhi hatari.

Kulingana na Dkt James Nyanjom, ambaye ni daktari wa maradhi ya mifupa, maziwa hayo yana madini aina ya lactoferrin, ambayo huisaidia damu ya mwanadamu kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na maradhi hatari.

“Wakati mtu anabuni mazoea ya kutumia maziwa ya ngamia, huwa anaogeza uwezo wa damu yake kukabiliana na maambukizi ya maradhi hatari. Hivyo, maziwa hayo huwa yana manufaa sana kumwezesha mwanadamu kuboresha uwezo wake wa kujilnda dhidi ya maradhi hayo,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Dijitali.

Maziwa hayo pia yana usaidizi mkubwa kwa watu wanaougua maradhi ya kisukari.

Kulingana na Dkt Nyanjom, tafiti nyingi zimeonyesha kwamba maziwa hayo yana protini ambazo huwa zinapunguza kiwango cha sukari kilicho katika damu ya mtu anayeugua maradhi hayo.

Mtaalamu huyo anasema kuwa watu wanaokunywa vikombe viwili vya damu hiyo kila siku huwa wanapunguza kiwango cha sukari katika damu yao, kuliko wale ambao huwa hawayatumii.

Anasema hilo hupunguza uwezekano wao kupata madhara hatari yanayotokana na maradhi hayo sugu.

Hata hivyo, anasema kuwa wale wanaotumia maziwa hayo lazima wafanye mazoezi ya kutosha.

“Matumizi ya maziwa ya ngamia pekee hayawezi kupunguza athari kamili za maradhi hayo. Lazima wale wanaoyatumia wafanye mazoezi ya kutosha ili kuongeza umahsusi wake kwenye miili yao,” akaongeza.

Manufaa mengine ya maziwa hayo ni kumsaidia mtu kudumisha ubora wa ngozi yake. Hili ni kupitia chembechembe za asidi maalum iitwayo alpha-hydroxy, ambayo husaidia ngozi ya mwanadamu kulainika.

Inatajwa kuwa nguzo muhimu kwa watu ambao wanapenda sana kudumisha ubora wa ngozi zao, bila kutumia mafuta, kwani mengi yamekuwa yakitajwa kuwa na kemikali hatari kwa ngozi.

Maziwa hayo yanatajwa kuwa na madini ya kuzuia ngozi kuzeeka kwa kuondoa ugumu na kuongeza unyevunyevu.

“Kwa hilo, ngozi za watu wanaotumia maziwa hayo kwa wingi huwa zinalainika sana. Wengi huwa hawazeeki haraka, licha ya kuwa na umri wa juu. Ni kiungo muhimu sana cha kudumisha ubora wa ngozi,” akasema.

Maziwa hayo pia yametajwa kuwa tiba bora kwa maradhi yanayohusiana na akili.

Kulingana na Dkt Nyanjom, maziwa hayo yana madini maalum ambayo humsaidia mtu kupunguza mawazo yake.

“Watu ambao hutumia maziwa hayo kwa wingi huwa na uthabiti mkubwa wa kimawazo. Ni vigumu kuwasikia wakijihusisha kwenye mivutano isiyofaa,” akasema.