Makala

Je, ushirikina husababisha ajali za barabarani?

June 2nd, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

AJALI za mauti barabarani zimekuwa kero kubwa kwa familia nyingi hapa nchini ambapo nyingi hutazama makaburi ya wapendwa wao kwa macho ya huruma huku wakiwaza mbona usafiri ukawaletea majonzi.

Wengine wengi wamebakia tu kuangalia majeraha yao kwa huzuni wakijaribu kusahau masaibu yao barabarani ambako ajali iliwatunuku vilema.

Huku serikali ikihimizwa iwe na uwajibikaji wa kuwafurusha madereva na makanga watukutu barabarani ambao kwa mienendo yao isiyofaa huhatarisha maisha ya abiria na watembeao kwa miguu, baadhi ya madereva sasa wanadai ushirikina unachangia janga hili.

Wengine wanadai kuwa baadhi ya barabara za hapa nchini zimevamiwa na majini ambayo husababisha ajali hizo.

Kwa mfano, baadhi ya madereva wa magari na pia wa bodaboda ambao wamenusurika katika ajali eneo la kati wanadai kuwa katika sehemu tofauti za barabara za eneo hilo kwa mfano, huwa na nyanya wazee ambao hujitokeza ghafla barabarani wakiwa uchi na kusababisha ajali hizo.

Madai haya yalitolewa na walionusurika katika ajali iliyowaua watu wanne na kuwajeruhi vibaya wengine watatu katika eneo la Kambiti katika Kaunti ya Murang’a Kusini hivi majuzi.

Nyanya mzee akiwa uchi

Joseph Karanja ambaye alinusurika ajali hiyo iliyohusisha trela na gari la abiria aina ya Nissan aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa alimsikia dereva akipiga duru kuwa ameona nyanya mzee akiwa uchi akijitosa mbele ya gari lake.

“Alipiga duru akikemea nyanya huyo aondoke haraka ama akanyangwe lakini tukajipata tumeangukiwa na lori hilo,” akasema.

Makanisa yanaombwa yapange ibada za maeneo yanaodaiwa kusakamwa na majini hayo ili kuyatakasa ili watu wanusurike ghadhabu ya mapepo hatari ya kuwasajili walio hai kwa maisha ya kuzimu.

Aidha, wahudumu wa bodaboda katika mji wa Sabasaba waliambia Taifa Leo kuwa ni ukweli kuna nyanya mzee ambaye amekuwa akijitokeza mbele yao katika eneo la Gakarati na ambapo katika kipindi cha miezi sita iliyopita, watu sita wamepoteza uhai wao katika ajali eneo hilo.

Lakini Kamanda wa polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua anapuuzilia mbali madai hayo akisema ni ya kuudhi na pia ya kutafuta vijisababu kwa madereva watukutu kuendelea kuua watu kwa uendeshaji mbaya wa magari.

“Madereva wengi hasa wa pikipiki katika eneo hilo hujitokeza kwa barabara bila ya kuzingatia usalama wowote na ndipo huwa wakitoka kwa barabara za kuwaunganisha na barabara kuu huwa wanakumbana na magari na kuwaua papohapo,” akasema.

“Madereva waache visingizio vya kusema wanaona mazingaombwe barabarani. Ndio kuna Shida za barabara mbovu, madereva kukaidi sheria za barabara na raia nao kuwa na utovu wa kinidhamu katika shughuli zao barabarani, lakini tusiwe wa kukwepa uhalisia wa mambo kuwa ajali nyingi zinatokana na maamuzi mabovu ya madereva, ulevi na umang’aa,” akasema.

Alisema tayari ameagiza misako itekelezwe dhidi ya wahudumu wa bodaboda ambao hawajatimiza masharti ya sheria za barabarani.

Majini barabarani

“Ikiwa kuna majini barabarani, hawa madereva wa matatu na bodaboda ni wao. Hawawezi kusingizia roho za kuzimu na wao ndio wanaua watu kwa kutozingatia sheria za barabarani,” akasema.

Maeneo yanayotajwa kukubwa na majini hayo ni Kiganjo-Naromoru, Kibirigwi-Sagana, Limuru-Uplands, Blue Post-daraja ya Sagana, na Nyeri-Nyahururu. Maeneo mengine Kiriaini-Murang’a, Makongeni Kuelekea Garissa kutoka Thika, Makutano-Embu na pia Kiambu-Muthaiga.

Kulingana na ripoti za Trafiki katika eneo la Kati, maeneo hayo yamekuwa kichinjio kwa watu 980 kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita huku wengine 510 wakipata majeraha mabaya na mamia ya wengine kunusurika mauti na majeraha mabaya.

Aidha, aina mbalimbali za mifugo 136 wamekufa katika barabara hizo kwa kipindi hicho wakiwemo ng’ombe sita.

Lakini mbona hatari ya ushirikina ionekane kuaminiwa hivyo na wenyeji hao?

Ushirikina unaogopwa sana katika maeneo mbalimbali ya hapa nchini na mara kwa mara visa vya raia wakiwafurusha washukiwa wa ushirikina zimeripotiwa.

Katika maeneo ya Kisii na Pwani, washukiwa huwa wanachomwa hadharani na kundi

lla vijana.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, kundi lingine limechipuka ambalo limeapa kutekeleza sheria kali za Sharia dhidi ya wachawi.

Kuua washirikina

Kundi hilo kwa jina Wakombozi wa Mwea limeapa kuwasaka washukiwa wa ushirikina na kuwaua hadharani kwa kuwapiga mawe huku maafisa wa polisi wakililinganisha na makundi ya kigaidi na kutangaza hali ya kutotoka nje katika maeneo yanayolengwa na kundi hili.

Wiki iliyopita, kundi hili lilimuua mzee wa miaka 52 kwa jina Githaka Kirombo kutoka kijiji cha Kirogo kwa madai kuwa amewaroga watu wanne katika kijiji hicho.

Shirika la Afya duniani (WHO) limeonya kuwa barabara za Kenya ni miongoni mwa hatari zaidi kwa uchukuzi.

Aidha, Shirika lingine la Uingereza Transport Research Laboratory (TRRL) linadai kuwa Kenya ni miongoni mwa nchi tano mbaya duniani katika visa vya ajali za barabarani.

Katika ripoti yake ya kila mwaka, Shirika hili linadai kuwa kwa mwaka Wakenya 3, 000 huaga dunia kutokana na ajali hizo.

Ripoti hiyo inasema jumla ya watu 1.17 million huaga dunia kila mwaka ulimwenguni huku asilimia 70 ikiwa ni kutoka nchi zinazoendelea. Hapa Kenya, WHO inaonya kuwa, kati ya magari 100,000 ni lazima 510 yahusike katika ajali mbaya na ambazo huzua mauti.

“Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Kenya ina hatari kubwa ikilinganishwa na Afrika Kusini ambayo kati ya magari 100, 000 ni magari 260 ambayo huhusika katika ajali mbaya. Nchini Uingereza, ni magari 20 pekee kati ya 100, 000 ambayo huua watu,” ripoti hiyo yasema.

Asilimia 65 ya vifo hizo hapa Kenya zinadaiwa kuwahusisha watembeao miguu asilimia 35 ikiwa ni vifo kwa walio chini ya miaka 18.