Afya na Jamii

Je, wafahamu kuogelea kunasaidia kudumisha mwili wa ujana

May 9th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wengi wa mwambao wa Pwani aghalabu si wageni wa kuogelea.

Wakubwa kwa wadogo huwa ni wajuzi wa kuogelea, ikizingatiwa kuwa maeneo yao yamebahatika kupakana na Bahari Hindi.

Utawapata wakazi hapa wakitenga muda wao kila siku au wiki kufika baharini na kujivinjari kwa kuogelea.

Wale wanaoishi bara pia hutenga nafasi katika likizo zao kuzuru Pwani ya Kenya ili kujipata fursa ya kuogelea, iwe ni kwenye ufuo wa Jomo Kenyatta, maarufu Pirates Public Beach, Kaunti ya Mombasa, kwenye fukwe za Mambrui, Mjanaheri na Malindi (kaunti ya Kilifi), Diani na Vanga kule Kwale, au fukwe za Shela na Wiyoni (Kaunti ya Lamu).

Pia kuna waja wengine, iwe ni Pwani au bara, ambao wamejijengea mabwawa yao ya kibinafsi ya kuogelea ilmradi wajifurahishe kuogelea.

Yaani uogelea kwa wengi huzingatiwa kuwa suala la kujivinjari au kupitisha muda tu.

Lakini je, wafahamu kwamba kuogelea kunasaidia kudumisha mwili wa ujana?

Katika mahojiano na Taifa Leo, wataalamu na washauri mbalimbali wa afya na saikolojia walifichua kuwa uogeleaji ni jambo muhimu na lenye manufaa chungu nzima.

Mwanamke akisimama kando ya bwawa la kuogelea mjini Mpeketoni. PICHA | KALUME KAZUNGU

Miongoni mwa manufaa au faida hizo ni kuwaepusha waja dhidi ya kuzeeka haraka katika maisha yao.

Daktari na Mtaalamu wa Afya katika kituo cha Afya cha Bluenile Mkoroshoni Medical Centre, Kaunti ya Kilifi, Duncan Amani Chai, anafafanua kwamba mazoezi ya mwili kwa jumla huwa ni mazuri.

Dkt Chai anataja uogeleaji kuwa miongoni mwa njia bora zaidi za mazoezi kwa mwili wote wa binadamu na hata mfumo wa moyo na mishipa.

Anaeleza kuwa kadri binadamu anavyozeeka, mifupa huwa inapungua kiuzito, jambo ambalo linaifanya kuwa dhaifu zaidi na kukabiliwa na uwezekano mkubwa wa kuvunjika.

Anaweka wazi kuwa punde mtu anapotinga umri wa miaka 35 hivi, huanza kupoteza asilimia karibu 0.5 ya ukubwa wa mifupa karibu kila mwaka.

Anasema ni kupitia kupungua huko kwa uzito ambapo huongezeka zaidi, hasa kwa wanawake wanapofikia umri wa kutoweza kuzaa na kwa upande wa wanaume, baada ya kuwa na umri wa miaka kama 50 hivi.

Dkt Chai anaendelea kufafanua kuwa ingawa madini ya calcium na vitamini D hufahamika kuwa muhimu kwa afya ya mifupa ya binadamu, tafiti nyingi zimeonyesha kuwa mazoezi kama vile uogeleaji yanaweza kupunguza hali hiyo.

“Watu wapende kuogelea. Kuna utamu wake, hasa kwa wale ambao hawapendi kuzeeka haraka katika haya maisha. Mazoezi, ikiwemo kuogelea huzuia kupungua kwa uzito wa mifupa na udhaifu wake kunakotokana na umri mkubwa. Unapokuwa na hulka ya kuogelea itamaanisha hata iwapo umri wako unasonga, bado utasalia kuwa na mifupa mizito na imara, hivyo kudumisha ujana wako tu,” akasema Dkt Chai.

Anaongeza kwa kusema, “Mazoezi yanaaminika kusaidia kuitunza mifupa yetu. Huifanya kuwa imara kwa kuiweka katika shinikizo la mazoezi. Sisi wataalamu wa afya tunaamini pakubwa kuwa kila msukumo au shinikizo kwa mfupa wakati wa mazoezi hutuma taarifa kwenye seli za mifupa na hivyo kuifanya iwe imara tena.”

Daktari Mtaalamu wa Mifupa mjini Malindi, Bi Loice Midze, alisema mbali na kudhibiti ujana, kuogelea pia kuna faida nyingine chungu nzima.

Dkt Midze anasema mazoezi, ikiwemo uogeleaji mara nyingi huifanya mifupa kupeleka taarifa kwa misuli ya mwili ambayo kama imeimarika ipasavyo husaidia pia kuimarika kwa ujenzi wa mifupa kwa jumla.

Bi Midze anasema suala la kuogelea yaani manufaa yake kiafya ni kuimarisha maungo.

Anasisitiza kuwa mbali na mifupa, mazoezi pia huwa ni mazuri kwa moyo, mapafu na ubongo.

Analinganisha kuogelea na mazoezi mengine kama vile kukimbia, ambapo huwezesha kalori nyingi kuungua, hivyo kumwacha mja na siha njema.

“Mojawapo ya faida kubwa za kuogelea ni kwamba hufanya kazi kwa mwili wako wote kuanzia juu kichwani hadi kwenye vidole. Pia huongeza mapigo ya moyo wako bila wewe kujitutumua kupita kiasi. Ni kupitia uogeleaji ambapo pia misuli hujengwa, kukupa nguvu na hata kujenga ustahimilivu hata zaidi,” akasema Bi Midze.

Anashikilia kuwa wakati misuli ya mja inapopata mazoezi mazuri, mfumo wake wa moyo na mishipa pia huwa mzuri.

“Kuogelea hufanya moyo wako na mapafu kuwa na nguvu. Kuogelea ni kuzuri. Hii ndiyo sababu waogeleaji huwa wana takriban nusu ya hatari ya kifo wakilinganishwa na wasioogelea. Kuogelea kunaweza kusaidia kupunguza shinikizo la damu,” akasema Bi Midze.

Wataalamu wa afya pia wanasema kuogelea ni muhimu, hasa kwa watu walio na majeraha au maradhi mbalimbali kama vile ugonjwa wa yabisi na hali nyingine za afya kuzorota.

Kuogelea ni chaguo bora la mazoezi kwani pia kuna uwezo wa kusaidia binadamu kupunguza baadhi ya maumivu au kuboresha ahueni yako kutokana na jeraha.

Watalamu wanasema watu walio na osteoarthritis wanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa maumivu ya viungo na ugumu kupitia kujituma katika uogeleaji.

Kwa upande wake, Mwanasaikolojia wa Lamu, Bw Andrew Masama, anataja faida nyingine za kuogelea, akisema huwa mbinu bora ya kuwasaidia watu waweze kulala vizuri usiku.

Anafafanua kuwa ikiwa watu hawapendi kufanya mazoezi mengine, kama vile kukimbia, pia wanaweza kufanya mazoezi ya kuogelea kuwa chaguo zuri, hasa ikiwa wanatafuta kuboresha usingizi wao.

“Najua msongo wa mawazo umeathiri wengi hadi kufikia wengine kukosa usingizi. Iba ipo. Jitose katika kuogelea. Ni dhahiri kabisa kwamba watu wazima wenye tatizo la kukosa usingizi wanaweza kuchagua kuogelea mara kwa mara kama mazoezi yao. Uogeleaji ni tiba ya shida hiyo. Kuogelea hufanya ubora wa maisha na usingizi huimarika,” akasema Bw Masama.