Makala

Je, waitambua densi ya bale? Deeja Atieno atakufunza

October 16th, 2020 3 min read

Na DIANA MUTHEU

Taifa Leo Dijitali ilipomtembelea Deeja Atieno,30, alikuwa akinyoosha misuli kabla ya kwenda jukwaani kuwatumbuiza kundi la watu waliokuwa wakifanya mafunzo katika majengo ya uvumbuzi ya SwahiliPot Hub, kaunti ya Mombasa.

Deeja anatambulika kwa aina moja ya densi ya kimataifa maarufu kama bale. Alielezea kuwa alijitosa katika densi hii baada ya kupata changamoto zilizomlazimu kuacha masomo akiwa katika mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha Kenyatta (KU), pale ambapo alikuwa anasomea kozi ya Hisabati na Sayansi ya Kompyuta.

Kupitia densi hiyo, mwanadada huyo anasema kuwa ameweza kujichumia kipato kwa kuwafunza watoto na watu wazima jinsi ya kucheza bale kupitia kampuni yake kwa jina D-Mwanzo.

Zaidi, ameweza kuonyesha tajriba yake katika video kadhaa za muziki na amepanda ngazi kiasi cha kuhusishwa katika filamu kadhaa zilizotayarishwa na maprodusa kutoka eneo la Pwani.

“Tangu utotoni, nilipenda kucheza densi. Baada ya kuacha masomo mwaka wa 2011, niliungana na wenzangu tukaanzisha kikundi ambapo tulijifunza bale kwani tulitamani kufanya aina tofauti ya densi,” akasema Deeja.

Bale ni aina ya densi inayochezwa kwa ustadi huku muziki ukiambatana na hatua sahihi zilizowekwa rasmi na ishara.

Kulingana na historia, bale ni aina ya densi ambayo ilianzia wakati wa ufufuo wa Italia katika karne ya 15, ikaimarishwa na kuchezwa katika tamasha nchini Ufaransa na Urusi.

Hadi wa leo, densi hiyo imekuwa aina ya densi ya kiufundi iliyoenea na msamiati wake unatokana na lafudhi ya Kifaransa.

Deeja Atieno akiwatumbuiza watu kwa densi ya bale katika majengo ya SwahiliPot Hub, Mombasa. PICHA/ DIANA MUTHEU

Deeja alisema kuwa ilimchukua muda wa miaka miwili kuijua densi hiyo kwani alihitajika kufanya mazoezi ili mwili wake uwe mwepesi wa kujikunja na mwili mzima uweze kunyumbulika vilivyo.

“Bale inanipa motisha wa kufanya mazoezi bila kuacha,” akasema Deeja huku akiongeza kuwa dhana iliopo kuwa watu wazima hawawezi aina hiyo ya densi, si kweli.

“Watu wengi husema kuwa bale ni ya watoto, haswa wasichana ambao bado misuli yao inaweza kunjika kwa urahisi. Licha ya changamoto kuwa mtu itamchukua mtu mzima muda ili aweze kuwa mwepesi, anaweza kucheza densi hii baada ya kufanya mazoezi ipasavyo,” akasema.

Kulingana na Deeja, mtu yeyote ambaye angependa kucheza bale anafaa kuvalia sare maalum na kufuata masharti yote ili kuepuka ajali ndogo ndogo ambazo zaweza kumuathiri pakubwa.

Baadhi ya vifaa maalum vinavyotumika katika bale ni pamoja na ‘barre’ ambayo ni chuma kinachotumika kufanya mazoezi ya kunyorosha misuli.

Sare maalum ni kama vile‘ballet slippers’ ambavyo ni viatu vilivyo na kamba spesheli na mcheza densi mwenyewe anahitajika kuvifunga.

Pia, kuna suruali maalim ya kuvalia na sketi au rinda liitwalo ‘tutu’.

“Kama huna uwezo, waeza kuvalia nguo za kawaida lakini ziwe za kubana kidogo ili zisikutege unapocheza densi. Pia, valia soksi ambazo hazitelezi sakafuni kwa urahisi kama huna viatu hivyo,” akasema Deeja huku akiongeza kuwa licha ya kuwa mwanadensi, anahifadhi desturi na mahitaji ya dini yake kwa kujisitiri vilivyo.

“Hata hivyo, nimesutwa sana na baadhi ya watu wakisema kuwa naenda kinyume na dini. Naifuata dini vilivyo hata katika harakati zangu za kujichumia riziki na kufanya ninachokipenda,” akasema Deeja.

Sheria zingine muhimu ni kama vile, kusafisha sakafu kabla ya kudensi ili kuepuka ajali baada na kufunga nywele vizuri katikati ili zisiathiri mazoezi au densi. Pia, mapambo kama vile shanga hazihitajiki.

“Katika densi hii, nafasi au uwanja unaotumika si lazima uwe mkubwa,” akasema.

Densi hii si ya watu matajiri pekee kama inavyodhaniwa. Kila mtu anaweza kuicheza. PICHA/ DIANA MUTHEU

Deeja ambaye pia ni mwanabiashara kuwa kucheza bale kumemsaidia kuimarisha afya yake kwa kuwa anafanya mazoezi mara kwa mara. Pia, anasema kuwa aina hii ya densi imemsaidia kupunguza msongamano wa mawazo.

“Densi hii imenipa nafasi ya kuielewa akili na mwili wangu zaidi,” akasema.

Alisema kuwa katika harakati za kucheza densi, amewahi kupata majeraha magotini na miguuni na kuwasihi watu wote wenye malengo ya kuanza bale wafuate maagizo.

Deeja anasema kuwa janga la corona lilimuathiri pakubwa pale ambapo shule ambazo alikuwa akitoa mafunzo ya bale zilifungwa.

“Miezi za kwanza baada ya kazi kukwama nilipatwa na msongamano wa mawazo, nikawacha kufanya mazoezi hadi nikaongeza uzani. Hata hivyo, nilijirudi na kuamua kufanya mafunzo mtandaoni,” akasema Deeja huku akiongeza kuwa fani hiyo ya densi ina uwezo wa kumchumia mtu hela iwapo itakubalika zaidi nchini.

“Densi hii si ya watu matajiri pekee kama inavyodhaniwa. Kila mtu anaweza kuicheza,” akasema.

Licha ya changamoto hizo, mwanadensi huyo ameweza kujiinua kimaisha kwa kujitosa katika upishi pamoja na wenzake wanne, pale ambapo hafunzi bale wala kuicheza.

Kupitia kampuni ya La Kwetu ambayo inahusika kupika na kusambaza vyakula vya aina tofauti tofauti, aliweza kupata fedha zaidi za kukimu mahitaji yake msimu wa corona.

“Msimu wa corona umenifunza kutilia maanani jambo lolote ninalolifanya na pia kuvumbua mbinu mpya ya kuendeleza biashara zangu,” akasema Deeja huku akiongeza kuwa atazidi kushirikiana na watu wengine wanaocheza hata kutoa mafunzo ya bale ili kuhakikisha densi hiyo inajulikana kote nchini.