Habari

Je, wanafunzi wanafaa kuadhibishwa ama kwa kuzabwa kofi au kiboko?

July 31st, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha ameibua mjadala mkali kuhusu pendekezo lake kuwa “kama mtu binafsi wala sio kama waziri ninaunga mkono wanafunzi watundu kuzabwa shuleni.”

Profesa amesema kuwa wakati kiboko kilikuwa kinatumika kama chombo cha kurekebisha mienendo na tabia kwa wanafunzi, adabu za kimsingi zilikuwa zinawaingia wanafunzi vyema.

Kwa sasa, Katiba ya nchi imezima adhabu ya kiboko sio tu kwa watoto walio shuleni au nje ya shule, bali kwa kila binadamu.

Leo hii, ukikutwa na kosa la kumuadhibu mwanafunzi kwa kiboko, utakabiliana na hatari hata ya kufungwa maisha gerezani iwapo utashtakiwa kwa kukiuka sheria za watoto nchini.

Hata hivyo, Prof Magoha – kama mtu binafsi – anapinga hali hii akisema adhabu ya kuzaba kwa utaratibu bora, ni njia moja ya kuadhibu mtoto na kumweka katika mkondo ulio sawa hasa ikiwa anayetekeleza adhabu hiyo atawajibikia jukumu hilo kwa mtazamo wa kurekebisha wala sio wa kuumiza.

Ni hali ambayo imempata Prof Magoha akiungwa mkono na baadhi ya viongozi wa kidini ambao wamependekeza kurejeshwa kwa adhabu hiyo kufuatia kuchipuka kwa magenge ya ujambazi yanayoendeshwa na wanafunzi katika baadhi ya shule za msingi na pia za sekondari.

Jumapili iliyopita, akihubiri katika kanisa la Mugwandi eneo la Kangaita, Kaunti ya Kirinyaga, Padri Charles Kinyua alisema hali hiyo imetokana na walimu kuzimwa kuwadhibu wanafunzi kwa kuwacharaza viboko wanafunzi watukutu.

“Walimu wametiwa hofu ya kuwakosoa wanafunzi vilivyo na walipoambiwa ni kukiuka haki za mtoto kwa kumwadhibu kwa kiboko, ndipo tulikubali enzi ya utukutu wa kila aina,” akasema Padri Kinyua.

Kubembeleza

Alisema hofu yake ni kuona walimu wakibembeleza wanafunzi watukutu kwa njia za kuwaongelesha maneno ambayo hata hayatiliwi maanani kama ushauri.

“Dawa ya mtoto mtukutu ni kiboko ili uchungu huo umwonyeshe hali ya dunia ilivyo. Tusiporejesha kiboko shuleni, tusiwe tukilalamika wakati tunawapoteza watoto hao katika hamaki ya raia na pia risasi za polisi,” akasema.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu, Bi Sabina Chege anasema kuwa mjadala wa kurejesha kiboko kama njia mojawapo ya kuwaadhibu watundu unafaa kuendelezwa na maoni yote yachukuliwe ili iamuliwe kama ni njia moja ambayo inaweza kuwanusuru wanafunzi kutokana na athari mbovu za kimaisha.

Mtangulizi wa Prof Magoha katika wizara hii ya Elimu, Bi Amina Mohamed kabla ya kuhamishiwa hadi Wizara ya Michezo na Turathi za Kitaifa alikuwa ametangaza wazi kuwa serikali haikuwa na nia ya hivi karibuni ya kurejesha adhabu hiyo.

“Leo hii hata unipokeze sheria za kuleta adhabu ya kiboko shuleni, sitaitekeleza kwa kuwa ni adhabu ya kuhujumu haki za kibinadamu hasa zile za watoto,” akasema Bi Mohamed.

Hii ilikuwa baada ya Mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa kutangaza kuwa alikuwa mbioni kuwavutia wabunge wengi wapitishe sheria ya kiboko shuleni akisema kuwa ndio dawa ya kuzima utundu wa wanafunzi katika shule za sekondari kuchoma mali za shule hasa katika muhula wa pili.

Waziri Mohamed alijibu kuwa kuna njia nyingi za kurekebisha tabia za watoto pasipo kuwacharaza viboko akiitaja adhabu hiyo kama iliyopitwa na wakati.

“Kinyume na maoni hayo ya kutumia kiboko kurekebisha tabia za watoto, kuna njia nyingi za kisasa ambazo zinaweza zikatumika,” akasema.

Bi Chege naye anasema kuna haja ya kupanua mjadala wa adhabu pasipo tu kushikilia kiboko ndicho adhabu ya uhakika ya kuzima umang’aa. Kinyume na kiboko, amependekeza kuwa vinara wa wanafunzi mashuleni wawe wakichaguliwa kwa umakinifu zaidi ili kuzima visa ambapo “wanafunzi wakora ndio huwa maarufu kwa wenzao.”

Alisema kuwa enzi yake akiwa katika kamati ya bunge kuhusu elimu alikuwa akipokea habari kamati hiyo muhimu kuwa “wanafunzi wakora huwa ni ‘maceleb’ miongoni mwa wanafunzi wengine na wakati wa kuchagua vinara hao, wakora hao ndio huishia kupewa kura nyingi na hatimaye hao ndio huongoza wenzao kutekeleza kila aina ya utundu shuleni.

“Kuna mtindo wa kushabikia ukora wa binadamu hapa nchini na wanafunzi hawajaachwa nyuma. Katika uchaguzi wa vinara wao, wale ambao wanafahamika kuwa na tabia zisizofaa na ambao huwa ni weledi wa kukiuka sheria na kutekeleza utundu mwingineo hupendwa na wanafunzi hadi kuchaguliwa katika nyadhifa za uongozi na huishia kuwaongoza wenzao kwa njia zisizofaa,” akasema.

Alisema kuwa wakati wanafunzi hao wametekeleza uhalifu kama wa kuchoma shule au kuandaa mgomo, ‘maceleb’ hao vinara wa wanafunzi huwa hawawezi kuwajibika katika kusaka washukiwa “kwa kuwa hata wao ndio walihusika katika njama hizo.”

Na ikiwa hawakuhusika, akaongeza, vinara hao ‘maceleb’ huwa hawawezi wakasaidia katika uchunguzi kwa kuwa wanajua vile wanapendwa na wanafunzi wenzao kiasi kwamba hawawezi wakawasaliti waliohusika.

Bi Chege alisema mtazamo huo wa kimaisha umegeuza maisha ya kijamii kuwa hatari kuliko hata yale ya mahabusu katika jela za hapa nchini.

“Katika jela, mahabusu huwa na viberiti kwa kuwa ni wazi kuwa huvuta sigara wakiwa kizuizini hicho cha serikali. Lakini hujawahi kusikia kisa ambapo wamechoma mabweni yao huku wanafunzi ambao tunawachukulia kama wema kuwaliko mahabusu hao kila uchao wanatutwika hasara ya kuchoma mabweni yao,” akasema.