Michezo

Je, wanyama atajiunga na Wolverhampton Wanderers?

August 8th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Wolverhampton Wanderers inapigiwa upatu kuvua Mkenya Victor Wanyama kutoka Tottenham Hotspur katika siku ya mwisho ya kipindi kirefu cha uhamisho kitakachofungwa leo Agosti 8 saa moja usiku saa za Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Uingereza, kiungo huyu, ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Harambee Stars, anaorodheshwa na kampuni za bahati nasibu kuwa nafasi 3/1 kujiunga na mabingwa hawa mara nne wa Kombe la FA.

“Bournemouth, West Ham, Galatasaray na Southampton zinakamilisha orodha ya timu ambazo Wanyama anaweza kujiunga nazo kabla ya kipindi cha uhamisho kufungwa Alhamisi,” ripoti kutoka nchini Uingereza zinasema.

Wanyama alitua nchini Uingereza katika klabu ya Southampton mwaka 2013 akitokea Celtic nchini Scotland kwa Sh1.5 bilioni. Alipata umaarufu mkubwa Southampton na kununuliwa na Tottenham mnamo Juni 23 mwaka 2016 kwa kandarasi ya miaka mitano ya Sh1.3 bilioni.

Hata hivyo, Wanyama, ambaye ni Mkenya wa kwanza kusakata soka kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, amesumbuliwa na majeraha, hasa ya magoti, katika misimu 2017-2018 na 2018-2019 na kufanya Spurs kutafuta njia ya kumuondoa katika kikosi chake kwa sababu ya mchango wake kupunguka uwanjani.

Nafasi zake katika timu ya Spurs zinatarajiwa kupungua hata zaidi baada ya waajiri hawa wake kununua kiungo Mfaransa Tanguy Ndombele kutoka Lyon.

Wanyama pia alihusishwa na uhamisho hadi Fenerbahce nchini Uturuki.

Aidha, Wanyama alielekea mahakamani Agosti 7 kulalamikia kampuni ya Menengai Group kutumia picha zake kujinufaisha kibiashara bila idhini yake.

Mnamo Juni 21, kampuni hiyo ilichapisha ujumbe wa kutakia Harambee Stars kila la kheri katika Kombe la Afrika (AFCON) lililofanyika kutoka Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri.

Ilitumia picha kubwa ya Wanyama na anahisi haikuitumia tu kutakia Stars mema bali kujipigia debe kibiashara.