Habari Mseto

Jela maisha kwa kubaka mtoto aliyetumwa jiko la kupika chapati

January 7th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME wa umri wa makamo aliyemzuilia msichana aliyetumwa na mama yake kumuomba jiko la makaa wakapike chapati kisha akambaka amepewa zawadi ya kuishi jela milele.

Mwathiriwa aliyebakwa alikuwa na umri wa miaka 10. Samuel Kipesa Nyangaresi ameanza kutumikia kifungo cha maisha kwa kumtendea unyama mtoto huyo.

Hakimu mkazi Hosea Ng’ang’a aliyepitisha hukumu alisema “mshtakiwa angeonyesha uadilifu na kumpa mlalamishi jiko wakapike chapati.”

“Badala ya kumpa mlalamishi jiko la makaa, uliamua kumtendea unyama ambao hatasahau maishani mwake,” alisema Ng’ang’a.

Mshtakiwa huyo alipungia mkono chapo cha mwaka mpya na kupelekwa gerezani kula maharangwe na ugali maisha yake yote.

Mahakama ilielezwa na mashahidi watano akiwamo baba yake binti huyo kwamba mlalamishi alikawia katika nyumba ya mshtakiwa hata ikabidi baba yake kuenda kuangalia kilichokuwa kinaendelea.

“Mlalamishi alikutwa na baba yake akivaa nguo kisha mshtakiwa akapatwa na mshtuko,” alisema hakimu.

Bw Ng’ang’a alisema upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya Kipesa.

“Hii mahakama imekupata na hatia ya ubakaji. Tabia hii ya uhayawani haikubaliki kamwe katika jamii ya wastaarabu. Mlalamishi ni mtoto mdogo na ataishi na kofu hili la kubakwa maisha yake yote. Ataishi kuwachukia wanaume,” alisema hakimu.

Mahakama iliongeza kusema ni jukumu la wanaume kuwalinda na kuwatunza wasichana badala ya kuwadhulumu kimapenzi.

“Ili iwe funzo kwa wanaume wengine wenye tabia kama yako hii mahakama imekuhumu kifungo cha maisha gerezani,” alisema Ng’ang’a.

Kipesa alikabiliwa na shtaka la kumbaka mtoto huyo mnamo Januari 31 2018 katika eneo la Mpopong mjini Narok.

Mshtakiwa alikabiliwa na shtaka lingine la kumtendea madharau mlalamishi kwa kumshika sehemu zake nyeti. Hata hivyo alipatwa na hatia kwa kosa la ubakaji.

Akijitetea  mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo akisema alisingiziwa tu na maadui zake majirani ambao hawali walikuwa wamedai (Nyangaresi) alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama yake mlalamishi.

“Baba yake mlalamishi alikuwa amedai nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe jambo lisilo na ukweli. Madai haya ya uwongo yaliimbuliwa ili nisukumwe jela maisha,” alisema Nyangaresi akijitetea.