Habari Mseto

Jela maisha kwa kuua mpango wa kando’

May 30th, 2019 1 min read

Na MWANGI MACHARIA

MWANAMKE amehukumiwa maisha gerezani kwa kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mumewe.

Cecilia Waruguru Muriithi alipokezwa adhabu hiyo na Mahakama ya Naivasha kwa kumuua Susan Wanjiku Kihiu, 22, ambaye alikuwa akisomea kozi ya uanasheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Wawili hao walikuwa majirani, na Bi Muriithi alimuua mnamo Juni 30, 2013 katika mtaa wa Kingori mjini Maai Mahiu, akidai alikuwa mpenzi wa pembeni wa mumewe.

Mauaji hayo yalitatiza sana familia ya marehemu, ambaye alikuwa mwerevu na alipata alama ya ‘A’ kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) kabla ya kujiunga na chuo hicho.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Richard Mwongo alisema mshtakiwa alipatikana na hatia ya kutekeleza mauaji hayo na alipojitetea, hakushawishi korti kwamba hakuhusika.

Jaji huyo alisema marehemu alidungwa kisu mara kadhaa, akachomwa kwa kemikali au maji moto, kisha mwili wake ukatupwa kwenye uwanja ambao si mbali na nyumbani kwao.

“Kutotoa adhabu kali kwa mshtakiwa kutawasilisha ujumbe mbaya kwa wanawake na wanaume ambao wapenzi wao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi na wasichana au wavulana maarufu kama ‘mpango wa kando’. Adhabu nyepesi pia itatoa taswira kwamba mauaji ndiyo tiba kwa wanaohusika kwenye mipango ya kando.

“Ni kutokana na sababu hizi na kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, ndipo namhukumu mshtakiwa kifungo cha maisha gerezani. Hata hivyo, hukumu hii itaangaziwa upya baada ya miaka 20 iwapo mshukiwa atadhihirisha kwamba amebadilika,” akasema Bw Mwongo.

Bi Muriithi alipewa siku 14 kukataa rufaa kuhusu uamuzi huo.

Wakili wake, David Gichuki alikuwa ameiomba mahakama kutompa mteja wake adhabu kali.