Habari Mseto

Jela miaka 5 utakapokosa kufichua visa vya ufisadi

October 25th, 2020 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

ITAKUWA hatia kukosa kuripoti vitendo vya ufisadi na maovu ya kiuchumi endapo bunge litapitisha sheria iliyopendekezwa na Mpango wa Maridhiano (BBI) ya kupiga vita ufisadi.

Kulingana na Mswada wa Maadili na Uadilifu (2020) uliopendekezwa, unakabiliwa na tishio la kufungwa jela miaka mitano au faini ya Sh5 milioni au zote, kwa kuficha ufisadi.

Hatia hiyo inahusu kuwa na ufahamu kuhusu au kushuku kutekelezwa kwa hatia inayohusu ufisadi na kukosa kuripoti kuhusu jambo hilo.

Mswada huo unadhamiria kuanzisha hatia ya kuficha ufisadi na unatoa wajibu wa kuripoti kuhusu ufahamu au shaka yoyote kuhusu matukio ya ufisadi au maovu ya kiuchumi.

Aidha, mswada huo unasema kuwa mtu yeyote anayesaidia au kuwezesha ama atakayehusika katika kitendo chochote cha ufisadi na uovu wa kiuchumi ana hatia ya kosa hilo na iwapo atashtakiwa, atapigwa faini isiyozidi Sh5 milioni au kufungwa jela kwa muda usiozidi miaka mitano au yote.

Adhabu hiyo pia itatolewa dhidi ya mtu yeyote anayefahamu kuhusu nia ya kutekeleza uhaini na kisha kukosa kutoa habari na maelezo yote kwa vyombo vya serikali au kufanya juhudi nyinginezo zinazofaa kuzuia utekelezaji wa hatia hiyo.

Mashirika hayo yanajumuisha Tume ya Maadili na Kupiga Vita Ufisadi (EACC), na hakimu au afisa anayesimamia kituo cha polisi.

Ili kufanya kosa la ufisadi kuwa kitendo cha kujutia mno, sheria hiyo iliyopendekezwa inatoa adhabu kwa maovu ya kiuchumi na ufisadi.

Inapendekeza kifungo cha maisha kwa matendo ya ufisadi kama vile unyakuzi wa ardhi kwa njia ya udanganyifu.

Kwa sasa, sheria hiyo inapendekeza faini isiyozidi Sh1 milioni au kifungo cha jela kwa muda usiozidi miaka 10 au zote mbili.

Isitoshe, mswada huo unaitisha marekebisho ya katiba kuwezesha faini ya lazima kuwa mara tatu zaidi ya manufaa au hasara.

Ikiwa kitendo kilichohusisha hatia hiyo kilisababisha faida na hasara kwa mali ya umma, mswada huo unapendekeza faini ya lazima ambayo ni sawa na mara tatu ya kiwango cha manufaa na kiwango cha hasara.

Mswada huo vilevile unataka marekebisho ya katiba kufanya faini ya lazima kuwa sawa na mara tatu zaidi.