Kimataifa

Jenerali aliyejaribu kupindua serikali ya Bolivia Jumatano akamatwa

Na MASHIRIKA June 27th, 2024 2 min read

SURCE, BOLIVIA

POLISI nchini Bolivia walimkamata kiongozi wa jaribio la mapinduzi, saa chache baada ya Ikulu ya Rais katika mji mkuu wa La Paz kuvamiwa na wanajeshi.

Wanajeshi na magari ya kivita yalishika doria kwenye uwanja wa Murillo Square ambapo kuna majengo muhimu ya serikali. Gari moja la kivita lilivunja lango kuu la ikulu ya rais, na kuruhusu askari kuingia kabla ya kujiondoa baadaye.

Kiongozi wa mapinduzi Jenerali Juan José Zúñiga, ambaye yupo chini ya ulinzi, alisema alitaka kurekebisha demokrasia japo anamheshimu Rais Luis Arce kwa sasa, kutakuwa na mabadiliko ya serikali.

Jenerali Zúñiga alivuliwa wadhifa wake siku ya Jumanne, baada ya kutoa maoni ya uchochezi kuhusu rais wa zamani wa Bolivia, Evo Morales, wakati wa mahojiano.

Wakati wa kutoa hotuba kwa wananchi, Rais Arce alilaani jaribio hilo la mapinduzi, akitoa wito kwa umma kujipanga na kulinda demokrasia.

“Haturuhusu tena majaribio ya mapinduzi kuchukua maisha ya watu wa Bolivia,” alisema Rais Arce.

Maneno yake yalijitokeza wazi, huku waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wakiingia mitaani kuunga mkono serikali.

Bw Arce pia alitangaza kuwateua makamanda wapya wa kijeshi na kuthibitisha ripoti kwamba Jenerali Zúñiga ameachishwa kazi baada ya kumkosoa waziwazi kiongozi wa zamani wa Bolivia, Evo Morales.

Bw Morales pia alilaani jaribio la mapinduzi na kutaka mashtaka ya jinai kuanzishwa dhidi ya Jenerali Zúñiga na wasaidizi wake.
Afisi ya mwendesha mashtaka wa umma tayari imeanzisha uchunguzi wa jinai.

Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la Bolivia, Makamu Juan Arnez Salvador, pia alikamatwa.

Sababu halisi za Jenerali Zúñiga kuanzisha mapinduzi bado hazijabainika. Jenerali Zúñiga alifutwa kazi baada ya kuonekana kwenye televisheni, akisema atamkamata Bw Morales iwapo atawania tena wadhifa huo mwaka ujao, licha ya rais huyo wa zamani kuzuiwa kufanya hivyo.

Bw Morales alilazimishwa kuondoka madarakani mwaka wa 2019 na wakuu wa kijeshi ambao walisema alikuwa akijaribu kubadili matokeo ya uchaguzi wa urais.