Jenerali Badi awaangushia shoka maafisa 13 wa NMS

Jenerali Badi awaangushia shoka maafisa 13 wa NMS

Na COLLINS OMULO

IDARA ya Kusimamia Huduma Jijini Nairobi (NMS) imehamisha maafisa wake huku wengine wakishushwa vyeo na kupewa barua za kuonywa kuhusu utendakazi wao.

Mabadiliko hayo yametokea mwaka mmoja baada ya kubuniwa kwa NMS chini ya afisi ya Rais Uhuru Kenyatta.

Jumla ya ya maafisa 13 wa NMS wamehamishiwa idara nyingine au kushushwa vyeo huku wengine wakipewa onyo kali.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa mabadiliko hayo yamefanywa na uongozi wa Meja Jenerali Mohamed Badi kufuatia mvutano ambao imekuwepo ndani ya NMS.

Inadaiwa kuwa baadhi ya maafisa wamekuwa wakizozana, kuhujumu NMS na hata kufuja fedha za umma.

Wakurugenzi watano pamoja na naibu mkurugenzi wa NMS Kang’ethe Thuku wameathiriwa pakubwa na mabadiliko hayo yaliyofanywa jana.

Mabadiliko hayo pia yalifanywa katika idara za Fedha, Mazingira, Maji, Kawi, Afya, Usimamizi na Utoaji wa Kandarasi.

Wakuu wa idara ya Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) walipewa barua za kuonywa huku wakitishiwa kuhamishwa au kushushwa vyeo iwapo wataendelea kukiuka kanuni za kazi.

NMS ilibuniwa mnamo Machi, mwaka jana kusimamia baadhi ya majukumu ya serikali ya Kaunti ya Nairobi. Majukumu yaliyotengewa NMS ni afya, uchukuzi, miundomsingi, mipango ya kaunti na huduma za maendeleo.

“Wakurugenzi waliohamishwa, kushushwa vyeo au kukaripiwa wanadaiwa kutumia nyadhifa zao kuajiri na kutoa kandarasi kwa jamaa au rafiki zao,” akasema afisa ambaye aliomba jina lake libanwe kwa kuhofia kusutwa.

Mkurugenzi wa Kuajiri Wafanyakazi wa NMS Dominic Gicheru, Alhamisi iliyopita, alitakiwa kukabidhi afisi yake kwa afisa anayejulikana kama Bw Kibet baada ya kuhamishiwa idara tofauti nje ya NMS.

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa maafisa walioangukiwa na shoka pia wanadaiwa kushirikiana na wafanyabiashara walaghai ambao Rais Uhuru Kenyatta aliagiza waepukwe.

Idara ya kusimamia uzoaji taka ndiyo inadaiwa kusheheni idadi kubwa ya walaghai ambao wamekuwa wakipewa kandarasi za kukusanya takataka katika mitaa mbalimbali jijini.

“Ni ukweli kuna mabadiliko ambayo yamefanyika. Hii ni kwa sababu baadhi ya walioathiriwa wamekuwa wanahujumu Mkurugenzi Mkuu (Meja Jenerali Badi) kwa kuwapa wafanyabiashara walaghai kandarasi ya kukusanya takataka,” akasema afisa huyo.

Meja Jenerali Badi hakujibu arafa yetu tuliyomtumia tukitaka kujua kilichomsukuma kufanya mabadiliko hayo.

Baadaye tulifahamishwa kuwa Badi ni mgonjwa na hiyo ndiyo sababu hakuwepo wakati Rais Kenyatta alipokuwa akizunguka na kiongozi wa ODM Raila Odinga wakikagua miradi jijini Nairobi wiki iliyopita.

Mkuu wa mawasiliano wa NMS Tony M’Barine alisema kuwa hakuna barua rasmi ambayo imetolewa kuthibitisha mabadiliko hayo.

Bw M’Barine pia alisema kuwa hakuna ripoti ambayo imetolewa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuthibitisha kuwa kumekuwa na ubadhirifu wa fedha ndani ya NMS.

Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali iliyotolewa Februari, mwaka huu, ilionyesha kuwa kulikuwa na ufujaji wa sehemu ya Sh294 milioni zilizotolewa kwa NMS kukabiliana na virusi vya corona mnamo Juni, mwaka jana.

Miongoni mwa dosari zilizogunduliwa ni kushindwa kutumia Sh64 milioni kwa ajili ya vibanda vya kutenga waathiriwa wa corona, kutolewa kwa Sh32 milioni kutoka akaunti ya KCB kiholela na kutumia Sh120 milioni kulipa marupurupu wahudumu wa afya bila kuwa na bajeti.

You can share this post!

BI TAIFA APRILI 5, 2021

Maelfu kuenda Uingereza kabla ya marufuku kuanza