Habari za Kitaifa

Jenerali Kahariri aapishwa kuwa Mkuu wa Majeshi

May 3rd, 2024 1 min read

NA PCS

RAIS William Ruto amewataka wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kuhakikisha vikosi vinadumisha uadilifu na nidhamu ya hali ya juu.

Akihutubu Ijumaa asubuhi katika Ikulu ya Nairobi baada ya hafla fupi ya kuapishwa kwa mkuu mpya wa majeshi (CDF) Jenerali Charles Muriu Kahariri, Dkt Ruto alisema KDF ina historia pana ya kufanya kazi kwa kujitolea kikamilifu, umakinifu kazini na nidhamu ambayo imefanya Kenya kutambulika kimataifa.

“Jeshi letu la KDF lina historia ya weledi, uaminifu na kujitolea. Ninawasihi wanajeshi kuhakikisha historia hiyo nzuri inasalia hivyo,” akasema Dkt Ruto.

Wengine walioapishwa ni Luteni Jenerali John Omenda (Naibu Mkuu wa Majeshi-VCDF), Meja Jenerali Fatima Ahmed (Kamanda wa Jeshi la Wanahewa) na Meja Jenerali Paul Otieno (Kamanda wa Jeshi la Wanamaji).

Rais alisema wakuu wapya wa KDF wanapaswa kutumikia nchi na raia bila kujiingiza kwa ukabila na miegemeo kwa misingi ya kijamii.

“Nitawaunga mkono mnapotekeleza majukumu yenu na pia wananchi wanawaunga mkono kikamilifu,” alisema.

Aidha aliwataka wakuu hao wa jeshi kuwa na msimamo thabiti wanapoongoza wanajeshi wenzao, lakini wadumishe uadilifu wanaposimamia wadogo wao kazini.

Akizungumzia suala la mafuriko nchini, Rais Ruto alisema serikali inafanya kila iwezalo na imeelekeza jeshi kuongoza timu ya vitengo mbalimbali ndani na nje ya KDF kukabiliana na athari hasi za mafuriko.

Alisema mafuriko hayo yanashuhudiwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema uwezo wa KDF ni muhimu mno katika kufanikisha operesheni hiyo.

Waliohudhuria sherehe hiyo ni Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa Ulinzi Aden Duale, miongoni mwa wengine.

Mabadiliko katika jeshi yalifanywa kufuatia kifo cha Jenerali Francis Ogolla mnamo Aprili 18, 2024.