Jepchirchir aongezwa kwenye orodha wa wawakilishi wa Kenya mbio za 42km Olimpiki

Jepchirchir aongezwa kwenye orodha wa wawakilishi wa Kenya mbio za 42km Olimpiki

AYUMBA AYODI na GEOFFREY ANENE

KENYA imeongeza bingwa wa Valencia Marathon Peres Jepchirchir na nambari mbili kutoka London Marathon Vincent Kipchumba katika timu yake ya michezo ya Olimpiki 2020.

Naibu rais wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Paul Mutwii alitangaza hayo hapo jana akifichua kuwa Kenya itawakilishwa na watimkaji wanne katika marathon ya wanaume na idadi sawa na hiyo ya kinadada badala ya watano katika kila kitengo.

Jepchirchir, ambaye ni bingwa wa nusu-marathon duniani na pia mshikilizi wa rekodi ya dunia ya umbali huo wa kilomita 21, anaungana bingwa wa dunia wa mbio za kilomita 42 Ruth Chepng’etich, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 Brigid Kosgei na bingwa wa London Marathon mwaka 2017 na 2018 Vivian Cheruiyot.

Kipchumba atashirikiana na bingwa wa marathon kwenye Olimpiki za mwaka 2016, Eliud Kipchoge, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42, Amos Kipruto na mfalme wa Boston Marathon mwaka 2019 Lawrence Cherono.

Alipoulizwa sababu ya kuamua kuwa na wakimbiaji wanne badala ya watano katika kila kitengo, Mutwii alisema, “Ni uamuzi ambao tumefanya na tutaamini kuwa utatuletea ufanisi.”

Mutwii alisema kuwa AK itazungumza na Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) kuona njia nzuri ya timu hiyo kujiandaa kwa Olimpiki. “Wataendelea kufanya mazoezi kivyao kabla ya mpango wa kuwaweka pamoja kutekelezwa,” alisema Mutwii na kufichua kuwa NOC-K imeomba shirikisho hilo kuandaa kambi ya mazoezi ya watimkaji wa mbio fupi haraka iwezekanavyo.

Wakimbiaji wanne waliokuwa wametajwa Januari 2020 kujaza nafasi ya yeyote kikosini atakayejiondoa ama kuumia, wametemwa. Watimkaji hao ni Valary Ayabei na Sally Chepyego (wanawake) na Titus Ekiru na Bedan Karoki (wanaume).

You can share this post!

Washukiwa wawili Thika wanaswa na lita 4,000 za pombe haramu

Difenda David Alaba kuondoka Bayern Munich baada ya...