Michezo

Jepkosgei kutumia New York City Half Marathon kujiandaa kwa Haspa Marathon

February 15th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya wanawake ya mbio za kilomita 21, Joyciline Jepkosgei atatumia mbio za New York City Half Marathon mnamo Machi 17 kujipiga msasa kabla ya kujitosa katika mbio za kilomita 42 wakati wa Haspa Marathon Hamburg mnamo Aprili 28.

Jepkosgei amekuwa akisubiriwa kwa hamu kubwa kuingia ulingo wa mbio za kilomita 42 baada ya kuweka rekodi sita mpya mwaka 2017 katika mbio za kilomita 10 (dakika 30:05), kilomita 15 (45:37) na kilomita 20 (saa 1:01:25) akishinda taji la Sportisimo Prague Half Marathon katika Jamhuri ya Czech kwa saa 1:04:52 mwezi Aprili. Alifuta sekunde moja katika rekodi yake ya Nusu-Marathon akishinda Valencia Half Marathon kwa saa 1:04:51 nchini Uhispania mwezi Oktoba mwaka huo.

Pia, akitimka katika mbio za kilomita 10 za Birell Prague Grand Prix mwaka 2017, aliweka rekodi mpya ya dakika 29:43.

Makali yake yalipunguzwa na ugonjwa mwaka 2018, ingawa alishiriki katika Nusu-Marathon za Dunia mjini Valencia mwezi Machi na kumaliza katika nafasi ya pili kwa saa 1:06:54 nyuma ya Muethiopia Netsanet Gudeta (1:06:11) na mbele ya Mkenya mwenzake Pauline Kaveke (1:06:56).

Jepkosgei alipanga kushiriki marathon yake ya kwanza kabisa Desemba 8, 2018 mjini Honolulu, lakini akajiondoa siku chache kabla ya mbio hizo kutokana na jeraha la mguu.

Sasa anasema yuko tayari kutumia New York Half Marathon nchini Marekani kuona ubora wa mazoezi yake akilenga macho yake katika Hamburg Marathon nchini Ujerumani.

“Meneja wangu na kocha wangu wote wamenieleza kwamba mbio za Hamburg zinakimbiliwa katika sehemu tambarare inayowezesha mkimbiaji kuenda kwa kasi ya juu,” Jepkosgei aliambia tovuti ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) mnamo Februari 14.

“Nataka kukamilisha mbio za kilomita 42 mjini Hamburg kwa saa 2:22. Hata hivyo, bado nina miezi miwili ya maandalizi. Nitasubiri kuona jinsi mwili wangu utakubali mazoezi. Nikisalia na wiko moja kabla ya mashindano, nitajua fomu yangu na kisha kuweka lengo langu la mwisho.”

Mbio za mwisho za Jepksogei kabla ya kuelekea Hamburg zitakuwa mjini New York mwezi ujao.