Jeraha kumnyima Neymar fursa nyingine ya kucheza dhidi ya Barcelona kwenye kivumbi cha UEFA msimu huu

Jeraha kumnyima Neymar fursa nyingine ya kucheza dhidi ya Barcelona kwenye kivumbi cha UEFA msimu huu

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Neymar Jr hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Mauricio Pochettino wa Paris Saint-Germain (PSG) katika mchuano wa mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya UEFA dhidi ya Barcelona.

PSG watakuwa wenyeji wa Barcelona leo uwanjani Parc des Princes, Ufaransa na watajitosa dimbani wakipania kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakisajili ushindi wa 4-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliochezewa ugani Camp Nou, Uhispania mnamo Februari 16, 2021.

Neymar ambaye ni raia wa Brazil, alikosa pia kuunga kikosi kilichotegemewa na PSG katika ushindi huo wa ugenini kutokana na jeraha la paja.

“Neymar alirejelea mazoezi mepesi wiki moja iliyopita nab ado anajitahidi kuhakikisha kwamba anarudi katika ubora wa fomu ya kuweza kuwajibishwa tena uwanjani,” ikasema sehemu ya taarifa ya PSG.

Kwa upande wao, Barcelona wanaotiwa makali na kocha Ronald Koeman watakuwa bila huduma za mabeki Gerard Pique na Ronald Araujo.

Pique alipata jeraha baya la goti kwenye mechi ya nusu-fainali ya Copa del Rey iliyowashuhudia wakiwabandua Sevilla kwa jumla ya mabao 3-2 mnamo Machi 3, 2021 uwanjani Camp Nou. Kwa upande wake, Araujo alirejea kambini kuanza mazoezi mepesi wiki moja iliyopita baada ya kupona jeraha la kifundo cha mguu.

Kiungo wa zamani wa Liverpool aliyechezea Bayern Munich kwa mkopo mnamo 2019-20, Philippe Coutinho, pia atakosa mechi ya leo kwa upande wa Barcelona kutokana na jeraha la goti.

Barcelona waliopepetwa 8-2 na Bayern kwenye robo-fainali za UEFA mnamo 2019-20, wanajivunia rekodi ya kusonga mbele zaidi ya hatua ya 16-bora ya kipute hicho katika kila mmojawapo wa misimu 13 iliyopita.

Mnamo 2016-17, walipigwa na PSG 4-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora jijini Paris kabla ya miamba hao wa Uhispania kushinda mchuano wa marudiano kwa mabao 6-1 katika uga wao wa nyumbani wa Camp Nou.

“Nafahamu ugumu wa kibarua kilichopo mbele yetu. Hata hivyo, tunajiamini sana kwa sababu kikosi kinajivunia wanasoka walio na uwezo wa kupepeta PSG nyumbani na kutuongoza kuingia robo-fainali za UEFA kwa mara nyingine muhula huu,” akasema Koeman.

“Kupoteza 4-1 nyumbani kunatuweka katika ulazima wa kuwafunga wapinzani wetu mabao matano bila jibu nyumbani kwao. Japo ni suala zito, hakuna kisichowezekana katika mchezo wa soka,” akaongeza mkufunzi huyo raia wa Uholanzi.

Pochettino aliwahi kuwaongoza Tottenham Hotspur kutinga fainali ya UEFA mnamo 2018-19 ila wakazidiwa ujanja na Liverpool. Mbali na kukosa huduma za Neymar, kocha huyo hatakuwa pia na mshambuliaji Moise Kean ambaye kwa sasa ameshauriwa kujitenga baada ya kuambukizwa Covid-19. Moise anachezea PSG kwa mkopo kutoka Everton wanaoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Neymar aliwaongoza PSG kutinga fainali ya UEFA kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 2020 japo wakapokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Bayern jijini Lisbon, Ureno. Nyota huyo wa zamani wa Barcelona amefungia PSG jumla ya mabao 12 kutokana na mechi 17 za mashindano yote ya hadi kufikia sasa msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jombi ‘afilisisha’ shugamami

MKU na UNITAR zaingia kwenye mkataba wa ushirikiano wa...