KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jeraha la kifundo cha mguu kumnyima Neymar uhondo wa mechi mbili zijazo za Kundi G dhidi ya Uswisi na Cameroon

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jeraha la kifundo cha mguu kumnyima Neymar uhondo wa mechi mbili zijazo za Kundi G dhidi ya Uswisi na Cameroon

Na MASHIRIKA

NEYMAR Jr atakosa mechi mbili zijazo zitakazosakatwa na Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka huu kutokana na jeraha la kifungu ncha mguu.

Neymar, 30, aliondolewa uwanjani katika dakika ya 80 baada ya kuumizwa na Nikola Milenkovic akiwajibikia Brazil dhidi ya Serbia katika pambano lao la kwanza la Kundi G mnamo Novemba 25, 2022 ugani Lusail Iconic. Brazil ambao ni mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia, walivuna ushindi wa 2-0 katika pambano hilo lililoshuhudia fowadi Richarlson Andrade wa Tottenham Hotspur akifunga mabao yote mawili.

Neymar aliyekuwa katika maumivu makali, aliketi chini akiwa amefunika uso wake kwa mikono alipokuwa akipokea huduma ya kwanza uwanjani huku picha alizopigwa zikionesha kifundo chake mguu kikiwa kimevimba.

Mbali na Neymar, beki wa kulia, Danilo, pia atakosa mechi mbili zijazo za Brazil kutokana na jeraha la kifundo cha mguu.

Brazil wameratibiwa kuvaana na Uswisi katika mchuano wao wa pili wa Kundi G mnamo Novemba 28 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya Cameroon mnamo Disemba 2, 2022.

“Neymar na Danilo walifanyiwa vipimo vya MRI mchana wa Novemba 25 na ikabainika kuwa wana majeraha madogo kwenye vifundo vya miguu,” akatanguliza tabibu wa timu ya Brazil, Rodrigo Lasmar.

“Muhimu kwa sasa ni kuhakikisha kuwa wanapona kwa ajili ya mechi za baada ya hatua ya makundi. Hivyo, watakosa michuano miwili ijayo dhidi ya Uswisi na Cameroon,” akaongeza.

Neymar ambaye ni fowadi matata wa Paris Saint-Germain (PSG), amekuwa akitatizwa sana na mguu wake wa kulia kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita.

Alikosa kuongoza Brazil kwenye fainali za Copa America mnamo 2019 kutokana na jeraha la kifundo cha mguu wa kulia kabla ya kuwa nje kwa wiki kadhaa katika mwaka wa 2021 kutokana pia na tatizo lilo hilo.

Neymar alikabiliwa visivyo mara tisa akichezea Brazil dhidi ya Serbia na akachangia kupigwa kwa mipira ya ikabu mara nne zaidi kuliko mchezaji yeyote mwingine katika fainali za Kombe la Dunia kufikia sasa mwaka huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Gachagua, Mudavadi wajipanga kwa 2027

DARUBINI YA WIKI: Toleo Nambari 13 | Novemba 27, 2022

T L