Jeraha kumweka Coutinho nje kwa miezi mitano na kuweka Liverpool katika hatari ya kutopokea Sh5 bilioni kutoka kwa Barcelona

Jeraha kumweka Coutinho nje kwa miezi mitano na kuweka Liverpool katika hatari ya kutopokea Sh5 bilioni kutoka kwa Barcelona

Na MASHIRIKA

PHILIPPE Coutinho, 28, anatarajiwa kusalia nje kwa kipindi cha miezi mitano kuuguza jeraha la goti – habari ambazo ni mbaya zaidi kwa klabu za Barcelona na Liverpool.

Nyota huyo raia wa Brazil ambaye kwa sasa anatarajiwa kufanyiwa upasuaji, aliumia wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyowakutanisha waajiri wake wa sasa Barcelona Eibar mnamo Disemba 29, 2020 na kukamilika kwa sare ya 1-1.

Coutinho aliingia katika sajili rasmi ya Barcelona mnao Januari 2018 baada ya kuagana rasmi na Liverpool kwa kima cha Sh20 bilioni.

Hata hivyo, Barcelona walilipa kwanza arbuni ya Sh15 bilioni kwa maagano kwamba wangekamilisha salio la Sh5 bilioni kwa awamu.

Baada ya kuchezea Barcelona mara 100, yalikuwa maagano kwamba miamba hao wa Uhispania wangelipa Liverpool Sh2.5 bilioni kabla ya kukamilisha salio la Sh2.5 bilioni kwa awamu moja ya mwisho.

Hata hivyo, nyota ya Coutinho ilikataa kung’aa jinsi ilivyotarajiwa kambini mwa Barcelona ambao walimtuma kwa mkopo hadi Ujerumani kuchezea Bayern Munich katika msimu wa 2019-20.

Mechi dhidi ya Eibar ilikuwa ya 90 kwa Coutinho kuchezea Barcelona, kumaanisha kwamba angesalia na michuano mitatu pekee ya ziada ya kusakatia waajiri wake kabla ya Liverpool kutia kapuni Sh2.5 bilioni.

Hata hivyo, huenda Liverpool wasipokee sasa Sh5 bilioni za ziada kwa minajili ya mauzo ya Coutinho kutokana na jeraha ambalo kwa sasa huenda litamweka nje hadi mwishoni mwa msimu huku tetesi za kuondoka kwake ugani Camp Nou mwishoni mwa Mei au mwanzoni mwa Juni 2021 zikishika kasi.

Iwapo Coutinho atateua kujiunga na Inter Milan, PSG, Juventus au Bayern, basi ndoto ya kuvalia jezi za Barcelona mara 100 haitatimia na tukio hilo litawatia Liverpool kwenye hasara.

You can share this post!

Manchester United sasa unyo kwa unyo na Liverpool kileleni...

COVID-19: Manchester City kukosa masogora watano wa haiba...